Katika migogoro ya ardhi, yapo mambo mengi ambayo hujitokeza. Yumkini hii yote huwa ni katika kusaka haki.
 Liko jambo moja ambalo ni muhimu watu kulijua hasa wale ambao tayari wamejikuta katika migogoro ya ardhi.


 Mara nyingi imekuwa ikitokea pale mtu fulani ana mgogoro wa ardhi na mtu mwingine kumwendea polisi na kumshitaki kwa jinai ya kuvamia ardhi yake (criminal trespass).
 Ni kweli jambo hili lipo kisheria, lakini haliko moja kwa moja kama ambavyo watu wamekuwa wakilichukulia kama tutakavyoona baadaye.

Jinai ya uvamizi wa ardhi
Nimesema hapo juu kuwa jinai ya uvamizi wa ardhi huitwa criminal trespass. Kosa hili huhesabika limetendeka pale ambako mtu huingia katika ardhi ya mtu mwingine bila ruhusa, au mamlaka yoyote ya kisheria kutoka kwa mmiliki au penginepo huku akiwa na nia mbaya.
 Mtu anapokuwa amefanya hivi tayari huhesabika ametenda jinai ya uvamizi wa ardhi. Ardhi kwa maana hii hapa hujumuisha nyumba, shamba, kiwanja na kila kitu ambacho huitwa ardhi.
        
Kesi ya madai ya uvamizi ardhi
Hapo juu nimeeleza kosa hili la uvamizi ardhi lakini katika upande wa jinai. Yafaa tujue kuwa kosa hili pia ni madai. Kwa hiyo, kama hapo juu tumeona anayevamia ardhi ya mtu anaweza kufunguliwa kesi ya jinai, basi tuelewe kuwa kwa kosa hilohilo waweza fungua pia kesi ya madai.
Tofauti ya kesi ya madai na jinai katika kosa hili ni kuwa katika kesi ya jinai mtuhumiwa akipatikana na hatia, basi atatakiwa kwenda jela au adhabu nyingineyo wakati katika kesi ya madai mlalamikiwa akipatikana na hatia, atatakiwa kulipa fidia kwa mtendewa.


Kwa hiyo, uamuzi wa kesi gani mlalamikaji afungue uko mikononi mwake. Aidha, yawezekana pia kufungua kesi zote mbili kwa pamoja yaani Mahakama fulani ukafungua kesi ya madai na Mahakama nyingine ukafungua kesi ya jinai kwa wakati mmoja.
 
Usipoteze muda kumfungulia jinai ya uvamizi  unayegombea naye ardhi
Hapo juu nimeeleza kuwa kuvamia ardhi ni jinai lakini yafaa tujue kuwa jinai hii huwezi kumfungulia kila mmoja. Kabla ya 1980 ilikuwa mtu yeyote aliyevamia ardhi yako basi unaweza kumfungulia jinai ya uvamizi ardhi.


Lakini baada ya mwaka huo mwelekeo wa sheria ulibadilika. Mabadiliko yaliekeza kuwa ikiwa mtu fulani ana mgogoro wa ardhi na mtu mwingine, basi hakuna mtu kati ya watu hao anayeweza kumfungulia mwenzake jinai ya uvamizi wa ardhi.
Kwa mfano, A analalamika kuwa sehemu anayoishi B ni sehemu yake. Kutokana na hilo, A anaamua kwenda moja kwa moja eneo hilo kwa B na kukaa au kukaguakagua na kuondoka. Kwa mazingira kama haya B hawezi kumshitaki A kwa kuvamia ardhi yake.


Mfano mwingine ni kati ya K na Y. Hawa kila mmoja anaamini kiwanja fulani ni cha kwake. Siku moja K anapeleka mafundi wake na kuanza kujenga, kitendo ambacho hakimridhishi Y na kuamua kumfungulia kesi ya jinai ya kuvamia eneo lake. Kwa kesi kama hii Y hawezi kushinda na  kimsingi hakutakiwa kabisa kufungua kesi hiyo.
 
Isemavyo Mahakama kuhusu jinai ya uvamizi
Katika kesi ya Kibwana dhidi ya Jamhuri, TLR 321 Mahakama chini ya Jaji Kiongozi Mnzava ilisema kuwa katika kesi inayohusu umiliki wa ardhi, Mahakama haipaswi kuendelea kusikiliza kesi ya jinai. Iliendelea kusema kuwa iwapo kuna ubishi wa nani anamiliki mahali fulani, basi shauri hilo haliwezi tena kuwa la jinai isipokuwa wahusika washauriwe wakafungue kesi ya madai.


  Kutokana na hayo yote niliyosema hapo juu, basi nishauri kuwa watu wasipoteze muda kufunguliana kesi za jinai katika mazingira ya uvamizi ardhi, kwani kufanya hivyo ni kupoteza muda kwa kuwa kamwe hutafanikiwa katika shauri la namna hiyo.
 
Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, ndoa, kampuni tembelea sheriayakub.blogspot.com