Wako watu wengi wameathirika kutokana na matendo yanayotokana na uzembe, kutojali au makusudi ya madaktari.
Wapo waliopata vilema vya muda kutokana na uzembe huo, wapo waliopata vilema vya maisha na wapo waliouawa na madaktari.
Ajabu ni kuwa ukifanya tathmini ya haraka utaona kuwa watu wote waliopata madhila kutoka kwa madaktari huhusisha madaktari wa serikali, katika hospitali za serikali. Si rahisi kukuta jambo la ajabu la kitabibu limehusisha hospitali binafsi. Swali langu ni kuwa, umekuwa ukichukua hatua gani pale daktari anapokusababishia tatizo, iwe ugonjwa wa kudumu, ulemavu wa muda au wa kudumu au hata kifo cha ndugu au jamaa? Lakini kama hujachukua hatua, je, umekaa kimya ukiwa umeridhika au umekaa kimya kwa kuwa hujui jambo la kufanya?
Inaruhusiwa kumshitaki daktari
Wapo wanaodhani kuwa madaktari hawashitakiwi kwa kutomhudumia vema mgonjwa. Hili si kweli, daktari ni mtumishi sawa na watumishi wengine na kosa lolote la uzembe, kutojali au makusudi analofanya na kusababisha madhara kwa mgonjwa sheria inaruhusu kumchukulia hatua daktari huyo. Sawa na mtumishi mwingine akitenda kosa kazini anaadhibiwa, ndivyo ilivyo kwa madaktari pia.
Kwa mujibu wa sheria daktari amepewa wajibu wa hali ya juu kuhakikisha anatumia taaluma yake, weledi na uadilifu katika kutoa huduma ya tiba na kuepuka kabisa hatua au namna yoyote inayoweza kuleta madhara kwa mgonjwa.
Matakwa haya kwa daktari ni ya kisheria, si hiyari. Kwa hiyo watu waelewe kuwa suala la daktari kutoa matibabu kwa umakini ni lazima. Jambo lolote likiwa la lazima (mandatory) katika sheria maana yake ni kuwa kutofanyika kwake hutoa haki ya mtendewa kushitaki. Hivyo ndivyo ilivyo kwa madaktari. Kwa namna yoyote anapokosa umakini katika kutoa tiba basi ni ruhusa kwa mtendewa kushitaki.
Madhara anayosababisha daktari
Miaka ya nyuma wapo watu Hospitali ya Taifa ya Muhimbili walifanyiwa upasuaji huku kila mmoja wao akifanyiwa sehemu isiyohusika. Ni kisa maarufu, kila mtu anakumbuka, ambapo mmoja alifanyiwa upasuaji wa goti wakati akiwa na tatizo la kichwa na mwingine akafanyiwa kichwa akiwa anaumwa goti.
Mwaka jana msanii mmoja wa sanaa za maigizo (bongo movie) alifariki dunia katika mazingira ya kutatanisha baada ya kupigwa picha – miale (X-ray) na kusomewa kuwa ana matatizo ya utumbo na kuanza kupatiwa matibabu ya utumbo katika Hospitali ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam.
Hali ilizidi kuwa mbaya akapewa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako madaktari bingwa walithibitisha kuwa aliyesoma picha – miale (X-ray) alikosea, tatizo la mgonjwa halikuwa utumbo na kuwa amepoteza muda mwingi katika matibabu yasiyohusika, hivyo amechelewa, jambo ambalo lilisababisha kifo chake.
Matukio ya Mwananyamala ni mengi, huo ni mfano tu. Kisa kingine cha hivi karibuni ni kile kilichotokea Mkoa wa Tabora (Urambo), ambako daktari alimfanyia upasuaji wa tumbo mwanamke na kusahau kitambaa ndani ya tumbo la mama, hali iliyosababisha aanze kuoza utumbo hadi kizazi kuoza na kuharibika kabisa. Mungu mkubwa, mama huyo alinusurika kifo. Visa vya namna hii vya kusahau visu, mikasi, vitambaa kwa kina mama wakati wa kujifungua navyo havina idadi nchini. Inasikitisha sana.
Namna ya kumshitaki daktari
Natoa ushauri na hamasa kuwa imefikia wakati sasa tuwashitaki hawa madaktari na serikali yao ili kwa kulipa fidia kubwa wawe makini na wapate funzo, na hii itakuwa salamu muafaka kutoka kwa raia. Nimesema hapo juu kuwa daktari akisababisha madhara kwa uzembe, kutojali au makusudi kwa mgonjwa anashitakiwa.
Namna nzuri ya kushitaki ni kuomba kulipwa fidia ya fedha kutokana na madhara uliyopata au aliyopata ndugu yako. Kwa kuwa suala ni kutaka kulipwa fedha, basi ikiwa unataka ulipwe kuanzia shilingi moja mpaka shilingi milioni 100, basi fungua shauri hilo Mahakama ya Wilaya au Mahakama ya Hakimu Mkazi, wengi huiita Mahakama ya Mkoa. Na ikiwa unataka ulipwe zaidi ya shilingi milioni mia moja mpaka bilioni au trilioni na kuendelea, basi shauri hilo lifunguliwe Mahakama Kuu. Hii ni kwa mujibu wa sheria.
Hakikisha mahakama utakayofungua shauri kama ni ya wilaya iwe ni ile ambapo tukio hilo lilitokea.
Kama lilitokea wilaya fulani, basi Mahakama ya Wilaya hiyo ndiyo ina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo. Na kwa upande wa Mahakama Kuu, fungua Mahakama Kuu iliyo katika kanda ambako lilitokea tukio. Hiyo ni kwa mujibu wa sheria pia. Katika kushitaki, mshitakiwa namba moja atakuwa daktari aliyesababisha madhara. Pili, itaunganishwa hospitali husika kama mshitakiwa namba mbili na tatu, itaunganishwa halmashauri ya wilaya husika kama mshitakiwa wa tatu. Kisheria shauri la namna hii huwezi kumfungulia daktari peke yake bila kuwaunganisha hawa waajiri wake.
Hii ni kwa sababu yale mamilioni ya fedha unayodai inabidi yalipwe na hospitali husika au halmashauri, kwa sababu wao ndio wanaomjua huyo daktari. Katika kesi iliyotolewa hukumu hivi karibuni na Jaji wa Kanda yaTabora, Jaji Amir Mruma, Halmashauri ya Wilaya ya Urambo imeamrishwa kumlipa Mwamini Adam kiasi cha shilingi milioni 25 kutokana na uzembe wa daktari uliomsababishia madhara. Hii ndiyo sheria na ndivyo ilivyo, tuchukue hatua sasa.