Na Bashir Yakub, JAMHURI MEDIA
Huwa nawaambia kila siku kuwa jambo hadi likukute ndipo utajua kuwa lipo. Na nyote si mnajua kuwa kutokujua sheria si kinga/hoja/udhuru. Hautafikishwa mahakamani ukasema nilikuwa sijui, halipo hilo.
Kanuni ya 37 ya GN. No.60/2023 Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Kuhusu Usajili wa Laini za Simu inakataza mtu kumiliki laini ya simu zaidi ya moja kutoka mtandao mmoja kwa ajili ya matumizi ya kupiga, ujumbe na mtandao.
Kosa hili adhabu yake ni kifungo kisichopungua mwaka mmoja jela au faini isiyopungua Sh milioni tano au vyote kwa pamoja.
Kwa kipindi hiki tulichomo yawezekana kosa hili ni kati ya makosa yanayotendwa na wengi.
Kwa mujibu wa sheria hii kampuni pekee ndiyo yenye uwezo wa kumiliki laini za simu kufikia hadi 30. Mtu binafsi hata laini mbili za mtandao mmoja ni kosa.
Hili si kosa la madai, ni jinai tuelewane hapa. Hili jambo ni ‘serious’. Wengi mnazo laini hadi tano, ni basi tu siku yenu haijafika.
Nyongeza ya adhabu nilizotaja hapa juu, kanuni inasema pia ukikutwa na hatia utatakiwa kulipa Sh 75,000 kwa kila siku uliyomiliki laini au kila siku unayoitumia.
Kwa hiyo upige hesabu kama umemiliki miaka miwili basi ni Sh 75,000 mara kila siku katika hiyo miaka miwili. Sikwambiii kama unayo miaka mitano au zaidi.
Hii ni nyongeza ya zile adhabu za juu. Yaani baada ya kupewa zile adhabu za juu sasa unahesabiwa hizo siku unazokaa nayo ili ulipe.
Mathalani mtu anakutafutia kosa hapa hawezi kukukosa. Haya mambo yapo tukipata muda tuelezane tu kama hivi. Kuna muda unaweza kudhani ni utani lakini wapo watu tayari wameadhibiwa kwa makosa haya.
Nisisitize kuwa kwa mujibu wa sheria zetu kutokujua jambo fulani kama ni kosa si sababu ya kuachiliwa huru.
Sheria inamtaka kila mtu kuijua. Kwa hiyo katika kosa lolote usitarajie kuwa ukikamatwa utasema nilikuwa sijui. Kauli hii ya nilikuwa sijui haikubaliki katika sheria.