Dar es Salaam
Na Mwandishi Wetu
Harakati za uchaguzi wa Klabu ya Yanga zimeanza kwa kishindo na tayari majina kadhaa makubwa yamejitosa kutaka kumrithi Mwenyekiti, Dk. Mshindo Msolla.
Hakuna ubishi uchaguzi wa mwaka huu utakuwa na utamu wa aina yake kama uchaguzi mwingine uliopita wa klabu hiyo kongwe.
Pamoja na mafanikio ya Yanga katika msimu huu, wanachama wanapaswa kuwa makini zaidi kipindi hiki cha uchaguzi na kufanya uamuzi sahihi zaidi.
Wanachama wa Yanga wanapaswa kujua viongozi watakaowachagua ndio hao watakaokwenda kukaa mezani na mdhamini wao, GSM, na kuamua kuhusu katiba yao pamoja na lile suala kubwa la umiliki wa klabu wa asilimia 51 za wanachama na 49 za mwekezaji.
Wanayanga wanatakiwa kuepuka kuingia katika mtego uliowanasa watani zao, Simba, jambo linalofanya hadi sasa kushindwa kumalizia mchakato wa mabadiliko pamoja na kuwa na Bodi ya Wadhamini.
Najua tayari kuna makundi mbalimbali yanayotaka kuweka watu wao kwenye nafasi za uongozi. Ni wajibu wa kila mwanachama wa Yanga kusikiliza kwa makini sera za wagombea hao ili kufanya uamuzi sahihi siku ya kupiga kura.
Wapo watu wenye nguvu ya fedha wanaotaka kuchukua nafasi za uongozi kwa ajili ya masilahi yao binafsi, hao ni wa kuwaogopa. Kwa sababu fedha hizo za leo zitakuja kuigharimu klabu kwa muda mrefu zaidi.
Tunahitaji kuona Yanga ikiwa taasisi inayojitegemea. Hiyo itawezekana kwa kupata viongozi bora wenye maono na nguvu ya kujadiliana kwa uwazi na wadhamini, bila ya kuwa na hofu yoyote kwa masilahi mapana ya klabu.