Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Zanzibar
Watanzania wameshauriwa kuacha tabia ya kuchapisha picha na video za faragha mtandaoni kwa kuwa ni kinyume na maadili ya kitanzania lakini pia mhusika anaweza kupata madhara ya kisaikolojia kutokana na udhalilishaji anaoweza kuupata mtandaoni.
Mkurugenzi Msaidizi wa Usalama Mtandao wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Stephen Wangwe amezungumza hayo wakati akitoa mafunzo ya usalama mtandao kwa wanafunzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST) Oktoba 25, 2022 .
Amesema kuwa, matukio ya picha na video za faragha mtandaoni yanazidi kuongezeka na asilimia kubwa zinawekwa bila idhini ya wahusika baada ya kusalitiwa na watu waliowaamini au baada ya kupoteza kifaa cha TEHAMA kilichohifadhi picha hizo.
“Tunapaswa kufikiri kwanza kabla ya kupiga, kurekodi, kutuma na kusambaza matendo ya faragha katika mtandao ili kulinda heshima binafsi na kulinda maadili ya kitanzania”, amezungumza Mhandisi Wangwe
Ameongeza kuwa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, inazungumza wazi kuwa uchapishaji wa picha au video za faragha mtandaoni (ponography) ni kosa kisheria na adhabu yake ni faini si chini ya milioni 20, au kifungo kisichopungua
miaka saba au vyote kwa pamoja.
Mhandisi Wangwe ametoa rai kwa jamii kulinda faragha zao kwa kuhakikisha faragha inabaki kuwa faragha lakini pia kuhakikisha wanalinda vifaa vyao vya TEHAMA kwa kuweka password imara na ikiwezekana zaidi ya moja ili ikitokea kimepotea basi iwe ngumu mtu kufungua au kuona kilichopo ndani.
Naye Mtaalamu wa Usalama Mtandao, Bw. Yusuph Kileo amesema kuwa udhalilishaji wa kimtandao unaongezeka katika jamii na madhara yake ni makubwa sana kwa wahusika ikiwa ni pamoja na msongo wa mawazo au hata vifo hutokea.
“Ni kosa kisheria kudhalilisha watu kwa njia ya mtandao na faini yake si chini ya milioni tano, kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja lakini pia ni muhimu jamii kuhakikisha hatutengenezi mazingira ya kufanyiwa udhalilishaji
mtandaoni”, amesisitiza Kileo.
Rashidi Salim Abdallah , mwanafunzi wa TEHAMA wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar amesema kupitia mada zilizotolewa na wataalamu wa usalama mtandao wamejifunza kujiuliza nini faida ya vitu wanavyoposti mtandaoni
na kuepuka vishawishi vya kuwaamini na kuwatumia picha za faragha watu wanaokutana nao na kuanzisha mahusiano mtandaoni.