Mpenzi wangu utaniponza, 

Kwa mambo unayoyafanya,

Mpenzi unatuchonganisha, 

Mimi na yule ni rafiki,

Wewe watupambanisha, 

Mpenzi utaniumiza.

Wajaribu kunidanganya, 

wanambia yule wangu mwana,

Kumbe pembeni ni wako bwana,

Mpenzi utaniumiza,

Yule ulisema yule kaka, 

Kumbe mafuta ulinipaka,

Pembeni huwa hekaheka, 

Na vitanda kuvunjika.

Shemeji shemeji huku mwazima taa, 

Ushemeji wa urongo miye sitaki,

Huyo ni shemeji wako mwazimia nini taa?

Shemeji shemeji huku mwazima taa.

Ni wimbo wenye hisia ya mapenzi uliosheheni utamu na uchungu; ubaya na hiyana; na mafunzo kwa jamii. Una sifa zote za utunzi wa shairi: mistari, vina, urali, kituo na ujumbe kamilifu. Ni utaratibu wa kuigwa na kutumiwa na wasanii wa muziki wa leo. Wimbo almaarufu ‘Shemeji Shemeji’.

Nimechagua kuanza na wimbo huu miongoni mwa nyimbo nyingi nzuri, tamu na zenye ladha kusikia masikioni, ili kushitua hisia na kumbukumbu za wasanii wa muziki, wapenzi wa muziki wa dansi, ndugu, marafiki na jamii ya Watanzania katika kumuenzi mtunzi mmojawapo maarufu wa muziki nchini, hayati Salum Abdallah Yazide (SAY).

Ijumaa hii ya Novemba 19, 2021 sawa na Ijumaa ya Novemba 19, 1965, ni miaka 56 tangu mwanamuziki wetu kipenzi, Salum Abdallah, alipofariki dunia kwa ajali ya gari huko Morogoro. Ni busara kukumbuka fikra, mawazo na kazi zake njema alizozifanya na kutuachia.

SAY alizaliwa Mei 5, 1928 akiwa ni mtoto wa kwanza miongoni mwa watoto watano wa baba Abdallah Yazide; Mwarabu na mfanyabiashara wa mjini Morogoro, mwenye asili ya Hadhramaut, Bara Arab na mama Mluguru na mkulima mwenyeji wa Morogoro. Kwa maana hiyo, Salum na dada zake; Aisha, Nuru, Jamila na Zainab ni maafkaste.

Aliponyanyukia umri wa kuanza masomo, alipelekwa Shule ya Msamvu na Madrasa mjini Morogoro na Dar es Salaam. Masomo yaliyomwezesha kuchukuana na watu, na kutumia lugha ya Kiswahili, Kiarabu na Kiluguru kwa ufasaha na kidogo Kiingereza katika shughuli mbalimbali za mawasiliano.

Akiwa chipukizi wa umri wa miaka 11 alianza kupenda muziki wa dansi, kusikiliza sahani za santuri na kuimba. Nyimbo za kutoka Kongo, Kenya, Latin Amerika, Afrika Kusini na za hapa nyumbani zilimpagawisha. Mitindo na midundo ya Borelo, Chacha, Charanga, Twist, Rhumba na Samba ilisisimua akili na hisia za mwili wake. Tamaa ya kuwa mwanamuziki ikamjaa.

Miaka ya 1939 – 1950 kilikuwa ni kipindi cha mafunzo na kuhitimu muziki. Shule na Madrasa ikawekwa pembeni. Biashara ya hoteli aliyopewa na baba yake akaipa kisogo. Alimudu kujitengenezea gitaa la nyuzi tatu na kulicharanga. Baba yake alichukia mwenendo huu na kulivunja gitaa.

Salum alitoroka nyumbani na kwenda Mombasa akiwa njiani kwenda Amerika Kusini kujifunza muziki. Mazingira ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia (1939 – 1945) yalimkwamisha. Baba yake alipata habari zake na akatuma nauli. Salum alirudi nyumbani na akanunuliwa Santuri.

Baadaye mwaka 1947. Salum na vijana wenzake wakaunda kikundi cha dansi, kilichojulikana ‘LAPALOMA’. Akaanzisha Cuban Marimba Band mwaka 1952, bendi yenye tafsiri ya vionjo vya muziki kutoka Cuba (kule Latin America) na marimba ya kienyeji ya hapa nchini.

Salum alikuwa na uwezo wa kutunga na kuimba nyimbo pamoja na kupiga ala zote za muziki. 

Angalia wimbo ufuatao kwa makini na hatimaye jipatie jibu:

Niliona ajabu ndugu zangu mitaani,

Kuku watatu wanapigana barabarani,

Wa kwanza mweupe na wa pili mweusi,

Na wa tatu mwekundu wastani.

Kuku mweupe anampiga kuku mweusi,

Kuku mweusi anampiga kuku mwekundu,

Na mwekundu anampiga yule mweupe,

Nambieni mwenye nguvu pale ni nani?

Wimbo huu ulitia fora na kupendwa na wananchi wengi nchini.

Hadi sasa nyimbo za Salum zinatumbuiza watu sehemu mbalimbali. Mathalani; Idd Mubarak (Mkono wa Idd), Mheshimiwa Nyerere (Muungano), Beberu, Wanawake Tanzania na Walimwengu. Miongoni mwa nyimbo hizo  moto na maarufu ni Mpenzi Ngaie (Ngoma Iko Huku).

Wapenzi twawaimbia,

Maneno yenye murua,

Marumba twawaletea,

Mpate tulia.

Mpenzi wangu Ngaie,

Fika uone Kisangani,

Mpenzi wangu Ngaie,

Ngoma iko huku,

Njoo ufurahi,

Ngoma iko huku, Cuban Marimba Kisangani,

Ukitaka rhumba, rhumba liko huku, 

Ukitaka chacha, chacha liko huku,

Ukitaka samba, samba liko huku,

Ukitaka twist, twist liko huku.

Salum Abdallah katika uhai wake alioa mara mbili, bi. Zubeda, baadaye bi. Pili. Hakujaliwa kupata mtoto. Usiku wa Alhamisi majira ya saa moja hivi akiendesha gari lake nje ya mji wa Morogoro kuwachukua wafanyakazi wake, ghafla taa za gari zilizima na gari kugonga ukingo wa daraja na kutumbukia mtoni. 

Usiku ule alipelekwa hospitalini na kuonekana kibofu cha mkojo kimepasuka. Hakupata tiba, siku ya Ijumaa adhuhuri Salum alifariki dunia na kuzikwa Jumamosi ya Novemba 20, 1965 majira ya alasiri.