Umasikini ni kitu kibaya mno. Haya ndiyo yaliyonijia kichwani kabla na wakati wote ziara ya Rais Barack Obama wa Marekani.
Pamoja na shangwe ya Watanzania ya kumpokea, kwa namna fulani kulikuwapo matukio mengi ya Watanzania kudhalilishwa. Udhalili tulioupata si wa matusi wala kupigwa, lakini ni wa kutokana na hali yetu duni ya kiuchumi.
Mbwembwe zote zilizofanywa na Wamarekani katika anga na ardhi ya Tanzania, hazikutokana na amri ya Mungu. Ni matokeo yao ya kutokwa na jasho jingi kujijenga kiuchumi. Ni matokeo ya ukwasi walioupata kwa heri na kwa shari. Ni faida ya yale mema na mabaya waliyoutendea ulimwengu wa wanyonge.
Hakuna anayeweza kukana kwamba ukwasi wa Marekani umechangiwa kwa kiwango kikubwa mno na nguvu za mababu na mabibi zetu waliokamatwa, wakapigwa bei kama mbuzi na kisha wakapelekwa Marekani wakiwa watumwa. Inakisiwa kwamba Waafrika zaidi ya milioni 30 walikufa na kutupwa kwenye Bahari ya Atlantic. Watumwa walifanya kazi nyingi za suluba mashambani, viwandani – walijenga reli, walishurutishwa kujenga majengo makubwa makubwa, na kwa kweli walifanya kila aina ya kazi ngumu alimradi tu kuijenga Marekani.
Hapo awali nimeanza na kauli ya kuulaani umasikini. Umasikini si kitu cha kujivunia. Si kitu cha fahari. Si kitu cha kuomba kikawa jirani yako. Umasikini ni udhalili. Umasikini ni unyonge. Ukiwa masikini utafanyiwa majaribio mengi, yakiwamo yasiyokuwa ya kiutu.
Kwa ukwasi kama wa Marekani, taifa hilo linaweza kuwa na kiongozi mbumbumbu kabisa, lakini udhaifu huo ukafunikwa na utajiri wa nchi yake. Anaweza asiwe na jambo lolote la maana, lakini akizungumza kwenye hadhira atapigiwa makofi. Atashangiliwa. Atamiminiwa sifa. Akitoa nukuu ambayo masikini alishawahi kuitoa miongo mingi iliyopita, yeye tajiri ndiye atakayepewa sifa kwa kutoa neno la “busara”.
Ninachotaka kusema hapa ni kwamba ujio wa Rais Obama, licha ya ukweli kwamba ni heshima kwa taifa letu, bado umetuachia mambo kadha wa kadha tunayopaswa kujifunza na kuyapatia ufumbuzi. Funzo moja kubwa ni la adha za umasikini na namna ya kukabiliana nao.
Ujio wake uliwafanya baadhi ya watumishi wa umma, tena idara, taasisi na maeneo nyeti kabisa, wapate likizo ya lazima. Nafasi zao zikashikwa na Wamarekani. Kuanzia anga hadi kwenye nchi kavu, Wamarekani walitamba. Maofisa wetu wa Usalama wengi wao walikuwa wa kutumwa wafanye hili au lile! Mawaziri wetu waliotakiwa kukutana naye walichujwa kana kwamba walikuwapo waliohofiwa kumwambukiza TB! Mgeni anachagua akutane na nani. Hii ni dharau.
Wahudumu katika hoteli alimofikia waliondolewa kana kwamba walikuwa wakiugua upele. Wakatakiwa wapumzike hadi hapo bwana mkubwa atakapoondoka. Polisi wetu walipotaka kuingia maeneo nyeti, bila kujali sare na vitambulisho walivyovaa, walikaguliwa kana kwamba ndiyo wageni!
Barabara alizopita mgeni wetu zilisafishwa kwa maji na sabuni. Tukayaona magari ya usafi ambayo hapo kabla hatukuwahi kuyaona. Mashimo kwenye lami ambayo mara zote yalionekana kuwa ni matokeo ya uzembe wetu, yakazibwa ili bwana mkubwa asitikisike. Nusu saa kabla ya kutua kwa Rais Obama, anga ya Dar es Salaam ikafungwa. Hapakuwapo ndege ya kuruka wala kutua! Iliyoruhusiwa ni Air Force One pekee! Pwani ya Dar es Salaam kukaondolewa meli zilizosubiri kushusha shehena bandarini. Nafasi yake ikashikwa na manowari zilizokuwa na ndege vita za Marekani.
Waandishi wa habari tukatengwa kama wenye ukoma. Walijua kwa maneno hatutawaelewa -walichoamua kufanya ni kuweka maandishi kabisa. “Eneo hili ni kwa waandishi wa habari wa Marekani”. Hatukuruhusiwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Kila mwandishi aliyekuwa mahali ambako mkubwa huyo alifika, alitakiwa awe ameshajisaidia kabla!
Kwenye kuuliza maswali tukapangiwa maswali mawili tu! Fikiria utitiri wa wanahabari wa Tanzania na vyombo visivyo idadi, tukapewa nafasi ya kuuliza maswali mawili. Hata hayo mawili yalionekana mengi! Tukapewa nafasi moja ya kuuliza swali. Matokeo yake mitaani kwa wananchi wasiojua, wanahabari tumeyavaa matusi! Tumeonekana waoga na tusiokuwa na weledi wa kuuliza maswali kwa ung’eng’e! Eti ndiyo maana hatukuonekana tukiuliza! Tuliokuwa karibu tunajua wapi tulifungwa gavana.
Mara kadhaa tulipopata simu tulijaribu kuwaeleza wasomaji na watazamaji wetu hali ya mambo ilivyokuwa. Tukafikia hatua ya kujitetea kwamba kilichotukuta, ndicho kinachowakuta hata wenzetu wa Uingereza, Ujerumani na katika taifa lolote analozuru mbambe huyo wa dunia. Utetezi wetu unaonekana mwepesi. Hauna nguvu za kuwashawishi wananchi kuamini kuwa Rais Obama ni kiumbe kingine, na Marekani ni kama sayari nyingine!
Waliotuzonga kwa shutuma nasi tukawauliza, ilikuwaje wakaondolewa mitaani? Ilikuwaje wengine wasitokee makazini kwao? Ilikuwaje barabara zikafungwa na wao wakakubali? Ilikuwaje wakashindwa kumwona Rais Obama kama walivyowahi kumwona Madiba akitoka Uwanja wa Ndege wa Dar e Salaam (wakati huo) hadi Ikulu akiwa katika gari la wazi? Ilikuwaje kwa Obama wakaishia kushuhudia msafara tu wa magari yake?
Bwana mkubwa kaondoka. Machinga walioonekana kuwa ni uchafu mbele ya yake, wamerejea. Polisi wetu walioufyata, leo wamerejea kwenye ubabe wao, hasa ukizingatia Mtoto wa Mkulima ameshabariki wapige, na ikiwezekana waue! Pamoja na udhalimu ulioonekana kwa siku hizo mbili, kwa kweli Dar es Salaam ilipumua! Waenda kwa miguu walifurahi. Sasa binadamu kaondoka na binadamu wenzake, tumerejea kwenye maisha yetu ya kiporipori!
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika moja ya hotuba zake aliwahi kutuasa hivi, “Kusema kweli, duniani watu wanafikiri kwamba labda sisi ni masikini. Lakini umasikini mbaya kulio wote ni umasikini wa mawazo. Ni mbaya sana. Duniani kuna kujitegemea na kutegemea. Unaweza kutegemea, lakini kutegemea kokote ni kubaya sana. Kwa hali yoyote ile, kutegemea kubaya kupita kote kabisa ni kutegemea mtu mwingine kwa mawazo. Ni kwa ovyo sana kunakunyima utu wako.”
Naam, umasikini ndiyo uliotufanya Watanzania tuwe kwenye hali iliyotusibu wakati wa ujio wa Rais Obama. Ni ukweli ulio wazi kwamba nguvu, jeuri na mbwembwe zote za Marekani ni matokeo ya mambo makubwa mawili. Mosi, ni kutokana na utajiri wao – maana haiwezekani masikini akawa na jeuri ya kuwa na bajeti ya kuzuru mataifa matatu kwa wiki moja kwa kutumia Sh bilioni 160 na ushei.
Pili, inawezekana kabisa maisha haya ya Wamarekani ni matokeo ya sera na ubabe wao kwa binadamu wengine duniani. Ikumbukwe kwamba wiki iliyopita ni Marekani hao hao waliozitaka nchi kadhaa za Ulaya zizuie ndege ya Rais Evo Morales wa Bolivia, kupita kwenye anga lao. Ikamlazimu Rais huyo akwame kwa saa nyingi kwenye uwanja wa ndege. Ulikuwa ni udhalilishaji wa hali ya juu. Sasa mataifa ya Marekani Kusini yamekasirika. Uhusiano wao wa kidiplomasia umeingia doa.
Ubabe wa Marekani wa kutaka kuitawala dunia umeifanya iwe na maadui wengi kuanzia Afghanistan, Misri, Iraki, Iran, Libya na kwa ufupi ni karibu kwenye ulimwengu wote wa Kiislamu. Sera za Marekani na washirika wake kwa miaka yote zimekuwa za kukwapua mali kama mafuta kutoka mataifa mengine. Imeshiriki kuuza silaha na kuwafadhili wauaji, madikteta na wapuuzi wa kila aina. Imeulazimisha ulimwengu ufuate mfumo wake wa siasa kwa madai kwamba ndiyo demokrasi ya kweli.
Marekani imeshiriki kufanya dhuluma kwenye mataifa machanga. Kote huko imejikuta ikijikusanyia maadui wa kila aina. Ni kwa sababu hiyo, haishangazi kuona kila anapokuwa Mmarekani, kwake ni shaka tu! Shaka ya kudhurika inawafanya Wamarekani watumie kila mbinu kujihami. Wakati sisi tukiona kuwa ulinzi na unyanyapaa wao kwetu ni mbwembwe, kwao ni tofauti. Kwao ni kujihami dhidi ya maadui walioenea kila kona ya dunia.
Mwisho, kama alivyosema Mwalimu, umasikini mbaya ni umasikini wa mawazo. Tanzania tuna rasilimali zote za kutufanya na sisi tutembee vifua mbele. Tuna maziwa, bahari, madini ya kila aina, watu, misitu, ardhi ya kutosha, tuna hali ya hewa nzuri, kijiografia tupo pazuri. Je, tatizo ni nini? Ni mawazo?
Katika makala yangu wiki iliyopita, msomaji mmoja aliongeza pale palipopungua. Alisema pamoja na ukweli kwamba UZALENDO na uchapaji KAZI ni mambo muhimu ya kutuwezesha kupiga hatua kimaendeleo, bado tunapaswa kuongeza mengine. Nayo, alisema ni UADILIFU na kupiga vita aina zote za ufisadi, rushwa na uonevu. Kwa ufupi alisisitiza suala la HAKI. Sidhani kama wapo wanaopingana na nadharia hizi.
Tanzania tunaweza tusiwe na mbwembwe za manowari na ndege vita. Tunaweza tusiwe na magari au madege kama anavyotumia rais wa Marekani. Tunaweza tusiwe wanyanyasaji kama wao wanavyofanya kwa kisingizio cha usalama wao. Pamoja na kukosa yote hayo, bado tunaweza kabisa kuwa na mbwembwe za maana mbele ya walimwengu wenzetu; mbwembwe za kusema sisi si masikini.
Tunaweza kuondoa dharau kwa kuwa na maisha mazuri. Tunaweza kuwa na maisha mazuri ya kupigiwa mfano na mataifa mengine. Tunaweza kuwa na hali nzuri ya kuwafanya wenzetu wawe na kiu ya kujua siri ya mafanikio yetu. Tunaweza kuwa na taifa la watu waliosoma kiasi cha Ulaya na Marekani kutuonea wivu. Tunaweza kabisa kuwa na uchumi mzuri wa kuyafanya mataifa mengine yawe marafiki zetu; na tunaweza kuendelea kwa kila hali bila kutembeza bakuli kwa hawa wanaojiita wafadhili.
Lakini haya yote hayatawezekana, isipokuwa tu kwa kuuchukia umasikini na kuzingatia maneno ya Mwalimu:“Kusema kweli, duniani watu wanafikiri kwamba labda sisi ni masikini. Lakini umasikini mbaya kuliko wote ni umasikini wa mawazo. Ni mbaya sana.”
Kwa dhamira za dhati, na kwa kuwa na uzalendo kwa taifa letu, hasa kwa kuwa makini kwenye mikataba ya rasilimali zetu, sioni kwanini tusiwe na mbwembwe za maisha mazuri mbele ya walimwengu wengine.