DAR ES SALAAM
Na Dk. Felician Kilahama
Awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa amani tuliyonayo nchini. Hakika Mungu ni mwema.
Neno la Mungu linatutahadharisha tuwe makini (Luka 21: 34(a): “Basi jihadharini mioyoni mwenu isije ikalegea na ulafi, na ulevi na masumbufu ya maisha haya …”
Vilevile, katika (Luka 21: 10-11): “Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, njaa na tauni mahali pengi; (sasa janga la covid-19)”.
Kadhalika msitari wa 19 Neno la Mungu linatuasa kwamba: “Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu”.
Kuna msemo usemao: ‘Subira yavuta heri’. Hata hivyo, kwa mwovu ibilisi hakuna cha kuvuta heri. Kadiri siku zinavyosonga mbele, wengi tunavutwa sana na masuala kama fedha, starehe ikiwamo ulevi wa kupindukia.
Upendo kwa Mungu, muumba wetu ukielekea kupungua. Wakati huo ibilisi atajikita zaidi kwenye fedha, starehe, ulevi na mambo yake yote.
Hali ilivyo sasa inaashiria kuwa nyakati hizi ni za uovu na kuna dalili nyingi za kuonyesha kwamba shetani anajimilikisha malango ya wengi.
Kitendo cha kuchochea ulevi kwa kushusha bei ni dalili mojawapo ili shetani ajitukuze kupitia ulevi. Kadhalika, ubinafsi na kupenda fedha kupita kiasi ni dalili za shetani kuteka malango.
Hili linapingana na tahadhali kwamba binadamu tunatakiwa tufanye yote kwa utukufu wa Mungu, hivyo kututaka tuwe wa kiasi. Isitoshe watu wengi wako tayari kukiuka maadili kwa faida binafsi bila kujali masilahi mapata ya taifa letu au kumkosea Mungu.
Kutukana, kukejeli, kutumia mitandao ya kijamii vibaya, udanganyifu (kugeuza uongo kuwa ukweli; mathalani, eti ndoa za jinsi moja ‘ushoga’ ni kupendana kwa dhati? Mmmh, hatari!), wizi na ubadhirifu wa mali za umma; kutokujaliana, ndoa na familia nyingi kukosa amani ya kweli.
Hayo na mengine mengi si dalili njema kwa ustawi mzuri wa taifa letu, pia ni dalili za ibilisi ‘kujimwambafai’ na hatimaye kutaka kuisambaratisha jamii.
Yafaa tujiulize, tulikosea wapi na taifa linaelekea wapi kimaadili? Katika Injili ya Mathayo 24:24 imeandikwa: “Kwa maana watatokea Wakristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, ikiwezekana, hata walio wateule.”
Hapa Neno la Mungu linatutahadharisha tuwe macho shetani asiyateke malango yetu na kututawala. Iweje ‘wateule’ wa Bwana watumbukie huko?
Kwa kujikita katika nguvu ya fedha na kupitia fursa za ulevi na anasa; malango yanatekwa na wengi kuangamia kwa kujua au tutokujua. Pamoja na hayo yote sifa, utukufu na shukrani apewe Bwana Mungu wetu, hasa baada ya Bunge kupitisha Bajeti ya Serikali, Awamu ya Sita, hivyo kuashiria mwaka wa fedha wa Serikali kuanza rasmi Julai Mosi, 2021.
Hili ni jambo jema kwa ajili ya maendeleo yetu kiuchumi na kijamii. Pongezi kwa Wizara ya Fedha ambayo ndiyo mamlaka inayowajibika kipekee katika kusimamia mapato na matumizi halisi ya Bajeti ya Serikali.
Ingawa wizara zote pamoja na Serikali za Mitaa; wanawajibika kusimamia matumizi mazuri ya fedha za umma, Wizara ya Fedha inabaki kuwa mhusika mkuu.
Watanzania wote tuendelee kumwomba Mwenyezi Mungu ili hekima za kimbingu zitumike kufanya uamuzi sahihi kwa faida ya wengi.
Pamoja na kuyasema hayo nimekuwa na dukuduku moyoni hasa kuhusu mamlaka husika kushusha bei za vinywaji hasa vileo (intoxicating drinks).
Sijapata picha sahihi nini kimejiri mpaka kuamua kupunguza bei mfano, pombe aina ya bia. Yawezekana hatua hiyo imefanyika kuvutia wanywani wengi ili mamlaka iweze kukusanya fedha zaidi kuliko kuweka tozo kubwa na wanywaji wakawa wachache.
Ni kweli taifa linahitaji fedha za kutosha kuweza kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kuinua uchumi na hali ya maisha.
Hata hivyo, nimekuwa nikitembelea maeneo mengi nchini mijini na vijijini; lakini sijawahi kushuhudia sehemu za kuuza vileo (baa na stoo) zikiwa zimefungwa kwa kukosa wanywaji!
Eneo ninaloishi ni dogo ukilinganisha na utitiri wa baa na stoo zilizopo. Hali inatisha kwa wanywaji kuanza tangu asubuhi bila kujali saa za kazi. Je, huu ndio wakati wa Ibilisi kujikakamua?
Bei ya vileo imeshuka maana yake nini? Kwamba taifa litakusanya fedha nyingi na wakati huohuo watu wake, hasa nguvu kazi vijana, liwe ni kundi la wanywaji hivyo kujenga taifa dhaifu.
Iwapo unywaji ulikuwa unaendelea wakati bei ikiwa juu, sasa imeshuka; baa/stoo zifurike ibilisi apandishe mabega juu.
Iwapo hali halisi itakuwa hivyo litakuwa jambo la kusikitisha sana maana mamlaka husika inawaza kupata fedha nyingi lakini matokeo yake uovu ukaongezeka.
Wakati huo huo bei za mafuta (petroli na dizeli) zikapandishwa kwa kuongeza tozo kwa nia ya kutumia fedha zitakazokusanywa kujenga na kuimarisha barabara vijijini.
Nia ni njema, lakini gharama za usafiri pia zitapanda, mwisho wake ni huyo mlengwa kuumia zaidi. Ingawa tumo katika kipindi kigumu cha kujiletea maendeleo endelevu na tukiyavumilia maumivu kwa kipindi fulani na barabara vijijini zikaimarika, elimu ikaboreshwa na huduma za afya na maji zikawa nzuri, tutakuwa tumepiga hatua tarajiwa.
Pamoja na hayo, kushusha bei za vileo tutachochea ulevi na madhara kwa jamii yatakuwa makubwa.
Nyakati hizi watu wengi hasa vijana wamejitokeza kuwa watumia vileo kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Kwa mtazamo wangu, ingelikuwa heri iwapo bei za vileo zingebakia kama zilivyokuwa. Ongezeko la tozo ya Sh 100 kwa kila lita moja ya mafuta kwa lengo la kuimarisha barabara vijijini; likapata maelezo na wananchi tukaelimishwa ipasavyo kwamba maendeleo halisi yatatokana na nguvu zetu za ndani badala ya kutegemea misaada na mikopo.
Hali hiyo ingeeleweka na tukajifunga mikanda kwa minajiri ya kujiletea maendeleo endelevu kwa faida ya wote. Kimsingi tozo ya Sh 100 kwa lita moja isingekuwa chanzo kikuu cha kuumiza Watanzania.
Isipokuwa tangu zogo la covid-19 liikumbe dunia, uzalishaji wa mafuta umekuwa ukishuka na kusababisha bei katika soko la dunia kuongezeka sana.
Kwetu sisi hiki ndicho kiini cha bei kuongezeka hata kama kusingekuwapo tozo ya ziada. Bahati mbaya wengi tunaelekeza malalamiko kwenye ongezeko la tozo badala ya kumwomba Mwenyezi Mungu atujalie covid-19 iwe historia na maendeleo yetu kiuchumi na kijamii na kwa misingi ya uchumi wa viwanda; yasonge mbele ipasavyo.
Kimsingi, kupunguza bei za vileo kwa mantiki ya kupata mapato zaidi huku tukichocheo ulevi uongezeke; suala hili halijakaa vizuri, ingawa ibilisi atakuwa akishangilia bila kikomo maana wavu wake utawanasa wengi.
Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema na neema atujalie tulione hili na ikiwezekana hatua zichukuliwe kwa faida ya wote.