Wote tunajua kuwa kila atendaye kosa sharti aadhibiwe. Na kuadhibiwa huko lazima kuwe kwa mujibu wa sheria. Pamoja na kuwa mtenda kosa hustahili adhabu bado watenda kosa hutofautiana hadhi.
Hadhi hapa siyo kuwa fulani ni mkuu wa mkoa au mkurugenzi na fulani ni mkulima wa kawaida kijijini Katanakya.
Hadhi ndiyo kama hizo zilizotajwa katika kichwa cha makala. Wapo watenda makosa lakini wakiwa na umri mdogo, wapo watenda makosa wakiwa hawana akili timamu (machizi) hali kadhalika wapo watenda makosa wakiwa na akili isiyo ya kawaida kwa maana ya akili ya ulevi.
Sheria inasemaje kuhusu hawa wote kuanzia utendaji wao makosa, kushitakiwa na kuwajibika kwao? Makala yataeleza ili tujue hadhi ya kimashtaka ya makundi haya.
1. Je, mwenye ugonjwa wa akili anaweza kushtakiwa?
Jibu ni ndiyo, sheria haikatazi kumshtaki mwenye ugonjwa wa akili (chizi). Kuna tofauti kati ya kushtakiwa na kuwajibika. Kushtakiwa ni kumfungulia mashtaka na kuwajibika ni kupata adhabu baada ya kupatikana na hatia. Kwa hiyo, kushtakiwa atashtakiwa isipokuwa sheria inatoa mwongozo kuhusu kuwajibika kwake.
Kifungu cha 13 (1) cha Kanuni za Adhabu Sura ya 16 kinasema kuwa mtu hatawajibika kwa kutenda kosa la jinai iwapo wakati wa kutenda kitendo hicho alikuwa katika hali ya ugonjwa wowote unaoathiri akili yake. Hiyo ni kanuni ya jumla iliyowekwa na kifungu hicho.
Hata hivyo kifungu hicho hicho kimeweka masharti kuwa yapo mazingira ambayo mwenye ugonjwa wa akili atatakiwa kuwajibika. Kinasema kuwa mwenye ugonjwa wa akili hatawajibika kwa kutenda kosa la jinai iwapo tu wakati anatenda kosa alikuwa hajui anachokitenda, hana uwezo wa kutambua kuwa hapaswi kutenda kosa, na hana uwezo wa kuzuia kitendo hicho.
Hii maana yake ni kuwa ikiwa mgonjwa wa akili anao uwezo wa kujitambua wakati akitenda kosa, basi atapatikana na jinai hata kama ameua kwa makusudi atahukumiwa kunyongwa.
Maswali ya kitaalamu (examination) atakayoulizwa mahakamani ndiyo yatakayotoa majibu ikiwa alikuwa anajitambua wakati wa kutenda kosa au la. Hii ni kwa sababu akademia ya tiba inaonesha kuwa machizi wengi si wakati wote huwa hawajitambui.
Upo wakati huwa wanajitambua na upo wakati hawajitambui. Kutokana na hili isingekuwa sahihi kuwaacha watende walitakalo muda wote kwa kinga ya ugonjwa wa akili. Kama hili lingeachwa kungekuwa pia na uwezekano mkubwa kwa wenye akili timamu kutumia nafasi hiyo kutenda jinai huku wakitegemea kinga ya utimamu wa akili.
2. Je, ulevi ni kinga baada ya kutenda jinai?
Kifungu cha 14(1) cha Kanuni za Adhabu kinasema kuwa kulewa hakutachukuliwa kama kinga dhidi ya kosa lolote la jinai. Hii ni kanuni ya jumla. Yumkini yapo mazingira ambapo ulevi unaweza kuwa kinga baada ya kutenda jinai.
Tunaposema kinga tunamaanisha kuwa mtu atashtakiwa lakini atajitetea kuwa alikuwa amelewa au hakuwa na akili timamu, na kutokana na utetezi huo atatakiwa kuachiwa huru. Hii ndiyo maana ya kinga.
3. Ulevi kuwa kinga baada ya kutenda kosa
Ili kulewa iwe kinga baada ya kutenda jinai, sharti la kwanza ni kuwa wakati mlevi anatenda kosa iwe kweli ulevi ule ulimfanya awe hajitambui kiasi cha kutojua anachotenda.
Pili, ni kuwa ulevi ule usiwe umepatikana kwa hiari yake. Na hili ndiyo la msingi sana. Ukienda mwenyewe baa au nyumbani kwako ukanywa ukalewa, ukawa hujitambui na hatimaye kutenda jinai, ulevi haitakuwa kinga kwako abadan. Ili iwe kinga ni lazima iwe hukulewa kwa hiari yako. Hii ina maana kuwa ulilazimishwa kulewa au ulileweshwa. Kuleweshwa au kulazimishwa kulewa hapa siyo kununuliwa pombe halafu ukanywa, hapana.
Kuleweshwa au kulazimishwa kulewa ni kwa mfano umechanganyiwa pombe kwenye kinywaji kingine bila wewe kujua au umewekewa dawa za kulevya kwenye chakula, kinywaji bila wewe kujua. Hapa ndipo ulevi unapoweza kusimama kama kinga na hivyo kuondokana na hatia ya jinai.
Mazingira mengine ambapo ulevi unaweza kuwa kinga ni pale mwenye ugonjwa wa akili na kutokana na ugonjwa huo atakapojilewesha mwenyewe, na kutokana kulewa huko akatenda jinai. Ulevi utakuwa kinga kwake kwa kuwa uchizi ndiyo uliomsababisha alewe na hivyo haikuwa katika hiari ya kawaida. Kwa ujumla niseme tu hivi ndivyo ilivyo kwa hili la ulevi na kutokuwa na akili timamu.
Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.