Hivi karibuni nilihudhuria sherehe za kijana mmoja aliyefunga ndoa. Ni tukio la furaha kwa wana ndoa wenyewe, lakini pia kwa ndugu, jamaa na marafiki wa wawili hao.
Ni tukio linalowakutanisha watu wengi na huendana na shamrashamra za kila aina. Kula na kunywa pekee havinogeshi sherehe. Sharti kuwepo muziki – uwe ‘live’ au unaotoka kwenye ‘music system’. Tena basi, muziki wenyewe ili uwe na maana ni vizuri ukawa wa sauti ya kumfanya anayeshereheka umwingie barabara.
Tukiwa kwenye tukio hilo la harusi, simu ikapigwa na mmoja wa watendaji wa Serikali ya Mtaa. Naomba nisimtaje. Muda ulikuwa saa 2 usiku. Akatoa maagizo muziki uzimwe, maana ulikuwa ukileta bughudha kwa wananchi!
Kauli ile ilituchanganya na hata kutufanya tunyong’onyee. Tukajiuliza, iweje saa 2 tu usiku tuamuriwe kufunga muziki ilhali tukiwa na kibali cha polisi na Ofisi ya Utamaduni ya Wilaya kinachoturuhusu tuserebuke hadi saa 5 usiku?
Mmoja wetu akanyanyua simu, akawasiliana na mtoa amri. Sote tukawa tumenuna. Mtoa amri akawa mpole. Akatuacha tuendelee na sherehe zetu. Kwa ufupi ni kwamba hapakuwa na kosa wala usumbufu wowote kwa majirani. Ilikuwa ni yule mtawala kutaka kutuonyesha yeye ni nani.
Tukio hili ni la kweli na mimi nilikuwa miongoni mwa hao tuliopigwa bumbuwazi.
Kuna tatizo kubwa sana linalowakumba Watanzania na wasio Watanzania wakiwa ndani ya nchi inayosifika kwa umoja, upendo na mshikamano. Wazee waliposhiriki vita ya kumng’oa mkoloni walikusudia kuona manyanyaso yote dhidi ya wananchi yanakoma.
Uhuru wa nchi yetu ulilenga kuwafanya wananchi wawe wenye furaha muda wote, kwa kuwapa uhuru wa kwenda wanakotaka, pia kuchangamana alimradi tu wazingatie sheria. Katika nchi huru ni uonevu watu kupangiana au kuwekeana vikwazo vya uhuru hasa kama uhuru huo hauvunji sheria.
Vijana wengi nchini kote wana kilio kinachofanana. Nimeleta hapa tukio la harusi, lakini kuna matukio mengi ya vijana kuzuiwa kucheza disko kwa muda unaokidhi kiu yao ya ujana. Siku za wikiendi ni mahususi kwa vijana kwenda katika kumbi za starehe. Hawaendi kwa kutaka, bali kwa kusukumwa na rika. Kupenda kwao muziki si suala la hiari – ni matokeo au athari zinazotokana na ukuaji. Wakizeeka hawatataka hata kusikia kitu kinaitwa disko au dansi; tena wale wabishi wakienda maeneo hayo hawatataka muziku wa sauti ya juu.
Kuna kumbi za starehe mijini na vijijini. Vijana hukutana huko kufurahia ujana, lakini inapofika saa 4 au saa 5 usiku polisi hufika katika kumbi na kuwaamuru watawanyike kwa madai muda wa kustarehe umekwisha! Hii si sahihi. Mbaya zaidi, amri hii inawahusu wote walio ukumbini au nje ya ukumbi. Haijali mwanafunzi wala mzee.
Kuna sababu dhaifu zinazotumiwa kuhalalisha unyanyasaji huu. Mathalani, polisi hudai miziki inayochezwa hadi usiku wa manane ni kichocheo cha uhalifu, kwa hiyo wanaamini kwa kuifunga saa 5 matukio hayo yatapungua au kukoma kabisa!
Pili, ni kwamba vijana wakiachwa wacheze hadi usiku wa manane watakosa nguvu na ari ya kuwahi kazini, hivyo wataukaribisha umaskini. Tatu, sababu nyingine ni kuwa wanawapigia kelele wasiojihusisha na masuala ya muziki – wakiwamo wagonjwa.
Hoja ya tatu inaweza kuwa na mashiko, lakini dawa yake ni ndogo. Muziki, hasa nyakati za usiku unapaswa kuchezwa ndani ya kumbi zenye uwezo wa kutoruhusu sauti kutoka nje. Hilo halina ubishi.
Madai kwamba kufunga mapema sehemu za starehe kunapunguza uhalifu, hayana ukweli wowote. Kama kweli kuna wahalifu, wajibu wa vyombo vya dola ni kushughulika nao, na kamwe si haki kuwaunganisha watu wote kana kwamba walio wengi si waungwana.
Binadamu wanatafuta fedha ili waishi kwa raha mustarehe. Kijana aliyejibidisha akapata fedha anawajibika kuandaa maisha yake na jamii yake. Pia anayo haki ya kufaidi jasho lake kwa kupata anachokihitaji ndani ya misingi ya sheria.
Wapo wanaodhani starehe ni kulewa pombe tu, si kweli. Starehe ni pamoja na kuchangamana na marafiki kwa kadiri inavyowezekana bila kuingiliwa au kuwekewa vikwazo vya muda na mahali.
Vyombo vya dola vinapokuwa vinawaza kuwadhibiti wahalifu, vitambue pia haki ya raia wema ya kuwa na muda wa kutosha wa kufurahia maisha.
Hatuna budi kuachana na kasumba hii ya kulaza watu mapema kana kwamba Tanzania ni nchi ya majahili. Watanzania – watu wazima wanastahili uhuru wa kuamua matumizi ya kile walichovuna, alimradi tu kiwe ndani ya taratibu na desturi za kiungwana. Mtu aliyefanya kazi akachoka anahitaji kupumzika sehemu anayoona inamfaa, na kamwe isiwe polisi ndio waamue wapi huyo mtu apumzike na kwa muda gani.
Tusiwe taifa la kulazana mapema kama kuku wa kienyeji kwa sababu hakuna nchi iliyoendelea kwa kulazimisha watu wake walale saa 4 au saa 5 usiku. Hakuna. Wala sidhani kwa maisha ya leo kuna mtu anahitaji kukumbushwa na polisi kwamba anapaswa kulala ili awahi kazini. Maisha tuliyonayo, hata kama angekuwa na usingizi wa pono, ataamka tu mapema. Hakuna mchezo tena.
Mwito wangu kwa mamlaka zinazohusika ni kuwaacha Watanzania, hasa vijana wafurahie Uhuru ambao umeainishwa vizuri sana katika Katiba yetu ya mwaka 1977. Vijana wasibughudhiwe kwa kukamatwa kamatwa bila sababu hasa nyakati za usiku. Wajibu wa vyombo vya dola uwe kupambana na wakorofi tu. Vijana wa Tanzania wapewe fursa ya kuyafaidi maisha kwa kutembea vifua mbele ndani ya nchi yao. Kulazana saa 5 usiku kana kwamba sote katika nchi hii tu wahalifu, hakufai.