Naandika makala hii nikiwa nahudhuria kongamano la uwekezaji kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Wiki zijazo nitawashirikisha fursa za kibiashara na kiuwekezaji zilizopo Nyanda za Juu Kusini (mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya). Kwa leo nitachambua utamaduni wa kulalamika uliojengeka miongoni mwa Watanzania wengi; kiasi kwamba tunapitwa na fursa za kiuchumi zilizojaa kila kona.
Kwa muda sasa nimekuwa na utamaduni wa kutazama runinga mbalimbali za kimataifa na hasa za Afrika Mashariki. Pamoja na kutazama taarifa za habari za runinga za hapa nyumbani, huwa napenda kuchungulia kinachoendelea kwa majirani zetu pia. Nilichojifunza ni uwepo wa tofauti kubwa ya kimtazamo baina ya sisi Watanzania na majirani zetu, hususani Wakenya.
Watanzania wengi tuna fikra zenye utegemezi ilhali wenzetu Wakenya kwa sehemu kubwa wana fikra za kujitegemea. Hili utalibaini katika taarifa za habari, makala na vipindi maalum hasa vihusuvyo mambo ya uchumi. Mtanzania anapoulizwa ni nini anafikiria kuhusu tatizo lake, majibu anayoyatoa ni kama haya; “Serikali itusaidie”, “Serikali inatuonea”, “Serikali itutafutie ajira”, “Serikali ituhurumie”.
Kila Mtanzania anapokuwa na tatizo lile la kiuchumi ama la kijamii anachowaza ni msaada wa Serikali! Kila Mtanzania anapokwama amekariri kuwa anayemkwamisha ni Serikali!
Mtanzania anaweza kukamatwa ugoni na kupigwa halafu akihojiwa usishangae kumsikia akisema, “Hii Serikali ni ya rushwa sana, mimi napigwa tu halafu wenyewe hawaji kuniokoa wakati ni wajibu wao kutulinda sisi raia.” Watanzania hatuna utamaduni wa kuwajibika na tumekuwa wepesi wa kudhani mhusika wa maendeleo yetu ni Serikali.
Desemba mwaka jana, mfanyabiashara mmoja wa Kariakoo, Dar es Salaam, alihojiwa na moja ya vituo vya runinga, akitakiwa kutoa maoni yake kuhusu Krismasi ya mwaka ule. Jibu lake liliniacha mdomo wazi. Alisema, “Krismasi ya mwaka (huu) imekuwa tofauti na miaka mingine kwa sababu wateja wanaofika kununua ni wachache mno, tunaomba Serikali iingilie kati.”
Lakini kuna siku nikawa naangalia kipindi kimoja kwenye runinga ya Kenya kilichokuwa kinaangazia tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana. Vijana waliohojiwa ni takribani 12 kutoka vyuo mbalimbali nchini humo. Walipoulizwa ni nini wanafikiria ni ufumbuzi wa tatizo hilo, hakuna hata mmoja kati yao aliyetaja neno serikali!
Baadhi ya majibu yao yalikuwa “Nitafanya kila niwezalo nianzishe kilimo cha maua”, “Tutajiunga kikundi na kutafuta mtaji kwa wazazi na marafiki”. Yaani karibu wote walionesha mtazamo wa kuwajibika, wote walionesha kuwa wanafahamu kuwa mkombozi wa maisha yao kiuchumi ni wao wenyewe na si mtu mwingine ama serikali. Sasa jaribu kuuliza ufumbuzi wa tatizo hili la ukosefu wa ajira kwa vijana wetu wa vyuo vikuu Tanzania, uone watakavyotiririka kuililia Serikali.
Nimekuwa nikitafiti na kujiuliza mara kwa mara ni kwa nini Watanzania tumekuwa na utamaduni wa fikra na uamuzi tulionao! Ni mengi yapo nyuma ya mitazamo na fikra zilizotujaa Watanzania, lakini niharakishe kusema kwamba wanaharakati, wanasiasa na watu muhimu katika jamii wamekuwa wakichangia sana kukua kwa utamaduni wa utegemezi kwa kisingizio cha kupigania usawa wa kiuchumi.
Mara kwa mara nimekuwa nikiwasikia watu mbalimbali wakiwamo wanaharakati wa masuala ya kijamii, wakiwa wanasisitiza usawa wa kiuchumi miongoni mwa Watanzania. Kilio chao (sina uhakika kama wanalia kweli ama wanaigiza kwa maslahi ya kimalipo) kimekuwa ni kuona angalau Watanzania wanakuwa na ngazi zinazokaribiana kiuchumi. Wanasema na kulalamika kuwa pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho linakua kwa kasi mno.
Kinachopiganiwa na wanaharakati hawa (pengine na Watanzania wengine wenye mtazamo kama huo) ni kuona kuwa angalau wananchi wengi, kama si wote wanakuwa kwenye kada ya kati kiuchumi. Watu wa kada ya kati ni wale ambao si maskini na wala si matajiri, wanaishi maisha ya kawaida.
Si jambo baya kupigania watu wengi kuwezeshwa na kuingia katika kada ya kati, lakini kuna ‘makengeza’ katika kulitazama hili kulingana na mwenendo wa uchumi wa dunia. Lazima tukubaliane kuwa Tanzania si kisiwa na ikiwa moja ya nchi maskini inaathiriwa sana na mienendo ya pepo za mabadiliko katika ulimwengu mzima.
Kwa bahati mbaya jamii ya Kitanzania imekuzwa katika misingi ya kijamaa ambayo ilianzishwa na waasisi wa Taifa letu. Hawa walikuwa sahihi kwa zama zao, ambapo walitamani kuona wanajenga Taifa lenye usawa wa kiuchumi na kijamii.
Sitatumia muda mwingi kufafanua hili kwa sababu wengi wanafahamu namna mfumo wa Ujamaa ulivyoanguka duniani na kuziacha nchi zilizoamini katika mfumo huo kuwa katika hali ya kujisalimisha kwa mfumo wa kibepari.
Idadi kubwa ya watu bado inaota ndoto na kulilia mfumo wa kujengwa kwa jamii iliyo sawa. Lakini lazima tujiulize tunataka usawa katika daraja lipi? Je, ni daraja la kimaskini, daraja la kati, ama daraja la matajiri? Kwa bahati mbaya Ujamaa haukuamini katika uwezo na kipawa cha mtu binafsi badala yake uliamini katika vipawa vya jumuiya.
Hili linathibitishwa na ule mfumo wa kutaka njia za uzalishaji zimilikiwe na umma, vijiji vya ujamaa na vikundi vya ushirika. Hulka za Ujamaa na Kujitegemea zilijikuta (bila kukusudia) zikizimisha ujasiriamali, zikiminya vipawa vya watu na hata kuongeza utamaduni wa utegemezi.
Enzi hizo waliofurukuta kupata mali kwa njia za ujasiriamali halali walitazamwa kwa jicho baya wakiitwa kuwa ni wanyonyaji. Ujasiriamali (ulioanza kufundishwa sasa mashuleni na vyuoni) ukaonekana ni ubepari ambao ulichukiwa sana. Katika Tanzania hii hadi leo neno “bepari” linaonekana kuwa ni neno baya, kwa sababu tangu zamani watu waliaminishwa kuwa ubepari ni ‘dhambi’ hadi nyimbo za mchakamchaka mashuleni ziliimbwa kulaani ubepari.
Utajiri ulionekana hauna maana kama matajiri wamezungukwa na maskini. Kwa picha nyingine, ilikuwa inaonekana ni vema mtu uwe maskini kuliko kuwa tajiri halafu umezungukwa na maskini. Mtazamo huu ni wa kimaskini kupindukia kwa sababu huwezi kuisaidia dunia kuwa bora kwa wewe kuwa maskini. Unapokuwa maskini unaongeza mzigo kwa dunia.
Ni bora uwe tajiri na usiwasaidie maskini wanaokuzunguka (utakuwa umepunguza idadi ya maskini duniani) kuliko wewe kubaki na umaskini kwa kuuogopa utajiri! Katika enzi hizo ndipo ulijengeka utamaduni wa watu kutegemea serikali kila kitu. Watoto walisomeshwa na serikali, ajira zilitolewa na serikali, huduma na bidhaa vilizalishwa na kutolewa na serikali; vingi ya hivyo vikiwa ni bure kabisa ama kwa gharama nafuu.
Mifumo ya dunia imetuminya, hatuna tena uwezo wa kupewa kila kitu na serikali katika mfumo wa bure. Idadi ya wanaohitaji ajira ni kubwa kuliko ajira zilizopo; hata tulalamike huo ndiyo uhalisia. Mashirika ya umma yamekufa, ajira serikalini ni chache na wasomi wamekuwa wengi. Hali si kama zamani, mambo yamebadilika, elimu imeleta maana mpya ambayo Watanzania tunatakiwa kuitambua na kuzisoma alama za nyakati.
Hizi ni Zama za Taarifa (Information Age), elimu inatakiwa kumsaidia mwenye nayo kujitegemea bila hata kutegemezwa. Mambo yamebadilika, ni chaguo letu kubadilika ama ‘kukomaa’ tusibadilike. Lakini hata tukikomaa na kujifanya vichwa maji, ni kwamba dunia itatubadilisha na kutupeleka pengine tusikokuhitaji.
Hivyo tunapolilia kuwa na jamii iliyo na usawa wa kiuchumi lazima tuwe makini na tunachokitafuta. Hadi sasa dunia inaelekea kubakiwa na madaraja mawili tu ya matajiri na maskini (wenye nacho na wasio kuwa nacho), daraja la kati likiwa linazidi kutoweka kwa kasi kubwa. Nchi za Japan, China, India na Brazil zilisifika sana kwa kuweza kuwajenga wananchi wake wengi kuwa na uchumi wa kada ya kati, lakini mambo yanawaendea kombo kila kunapokucha.
Gazeti la New York Times la Aprili, 26, 2006 katika ukurasa wake wa mbele, lilikuwa na habari yenye kichwa, “Revival in Japan Brings Widening Economic Gap”. Katika aya yake ya pili habari hiyo ilikuwa na maelezo haya, “Today in country whose view of itself was once captured in the slogan, ‘100 milioni, all middle class society’ catchphrases harshly sort people into ‘winners’ and ‘losers’, and describe Japan as a ‘society of widening disparities,”.
Tafsiri isiyo rasmi ya maelezo ya aya hiyo ni, “Leo katika nchi ambayo ilikuwa na kaulimbiu kwamba watu wake wote milioni 100 ni wa uchumi wa kada ya kati imejikuta ikiwagawa wananchi wake katika makundi ya wenye nacho na wasio nacho, na sasa Japan inaweza kuelezwa kuwa ni jamii ya watu wenye tofauti kubwa kiuchumi”.
Hali iliyoikumba Japan inazikumba nchi zote nilizozitaja. Hata China ambayo hadi leo inadhaniwa kuwa imefanikiwa kuwa na watu wengi katika kada ya kati, kutokana na mfumo wa kiuchumi wa kijamii, inakoelekea itakuwa na kada mbili tu — maskini na matajiri. Hii ni kwa mujibu wa jarida la The Wall Street Journal.
Watanzania tunatakiwa kubadilisha mitazamo na fikra zetu halafu tuchague kati ya umaskini na utajiri. Baadaye hatutakuwa na kitu kiitwacho “kada ya watu wa kati”. Hivyo, sera, mipango na hata Katiba ya nchi yetu ni lazima viamue wazi wazi kujenga Taifa la kimaskini ama la kitajiri. Hata wanasiasa wanaohubiri usawa inabidi wawe wazi ni usawa katika utajiri ama katika umaskini?
Tukichagua kuwa matajiri lazima tuwaunge mkono matajiri waliopo na wanaoendelea kuibuka badala ya kuwapiga vijembe na kuwaona kama wanaotuibia na kutudhulumu.
Tukichagua kuwa sawa katika ‘ukawaida’ tutakuwa tumechagua umaskini. Maskini hawapo huru na walio huru si maskini kwa sababu walio sawa hawana uhuru na walio huru hawako sawa.
Ufike wakati Watanzania tujifunze na tujizoeshe kuwajibika kikamilifu na si kuililia Serikali wakati wote. Huku kulialia na kulalamika hebu kufike mwisho. Tujifunze kwa wenzetu na twende zaidi ya hapo, tujenge fikra na utamaduni wa kuwajibika!
Watanzania tunahitaji ushindi wa kiuchumi!
0714 07 11 39 [email protected]