Moshi
Na Nassoro Kitunda
Imekuwa ni kawaida sasa wananchi kuomba fedha kwa ajili ya matibabu. Afya ni huduma muhimu ambayo wananchi wanaihitaji sana.
Ukipitia mitandao ya kijamii, utaona namna watu wanavyoomba kuchangiwa matibabu, na ni mamilioni ya fedha ili waweze kupata huduma ya afya.
Suala la afya, limekuwa likiumiza vichwa vya Watanzania wengi hasa maskini, ambao hushindwa kumudu gharama za matibabu.
Jambo hili halijapata muafaka wa kutosha miongoni mwa jamii. Limechukuliwa kama upendo kwa watu kuwachangia fedha wapendwa wao wanapougua.
Lakini ipo hoja hapa, inatafakarisha sana. Kwa wananchi maskini itakuaje wakiugua? Na je, nani huwachangia? Hospitali zinauwezo wa kuwasamehe wagonjwa gharama? Au tunapaswa kufikiri zaidi ya misamaha ya matibabu?
Maswali haya, yanaweza yakatufanya tujadili kwa upana suala hili, ambalo linatuonyesha hali halisi ya huduma zetu za afya. Mfumo wa afya na watu wanaousimamia wanapaswa kutafakari, tutachangishana mpaka lini?
Wangapi wanapata michango? Na wakikosa michango itakuaje? Je, tuache afya iwe sehemu ya bahati nasibu?
Michango inaonyesha mfumo wa afya haupo sawa
Hii ni kusema kuwa gharama za matibabu ni kubwa ukilinganisha na maisha halisi ya Watanzania wengi. Ndiyo maana michango inaongezeka, ni dalili ya watu kushindwa kumudu huduma za afya.
Kwa hiyo, hatupaswi kuchukulia michango kama suala la kawaida, bali iwe sehemu ya kutufanya tufikiri upya kuhusu mfumo wetu wa afya.
Shida kubwa ipo pale tulipoanza kuifanya afya kuwa bidhaa. Bila fedha haupati huduma. Sasa wananchi walio wengi ambao ni maskini hawawezi kupata huduma.
Ipo mifano mingi ya walioshindwa na wanaoendelea kushindwa kulipia huduma ya afya. Tulikuwa na mjadala wa maiti kuzuiwa hospitalini na ndugu kutorosha wagonjwa kutokana na gharama.
Ndiyo maana kila kukicha matangazo yanaongezeka ya Watanzania wakiomba wachangiwe ili walipie huduma ya afya.
Kuifanya afya kuwa kama bidhaa ndiko kumehalalisha michango na ambao wanashindwa kulipa wanapata shida huko hospitalini.
Kinachoitwa sera ya uchangiaji, kwenye mfumo wa uchumi wa kibepari ndio umefanya wanyonge wahangaike kupata huduma, kwa sababu kila kitu ni fedha, dawa, vipimo, kulazwa na kumuona daktari.
Na magonjwa yamezidi kuongezeka. Kila kukicha magonjwa mapya, lakini kuongezeka kwa magonjwa pia gharama za kutibu nazo zinapanda kila kukicha.
Na Watanzania wanategemea huduma za hospitali kutibu magonjwa yao, lakini kutokana na umaskini hawawezi kujitibu kwenye hospitali hizo.
Takwimu zinaonyesha Watanzania wengi wanajitokeza hospitalini kila mwaka.
Takwimu za uchumi kwa mwaka 2018, zinaonyesha Watanzania zaidi ya milioni 40 walikwenda hospitalini kupata huduma (wagonjwa wa nje na waliolazwa).
Hii inaonyesha namna gani Watanzania wanategemea sekta ya afya, lakini wanachokutana nacho kwa maana ya gharama za matibabu ndizo zinawakatisha tama. Gharama zimekuwa mzigo mkubwa.
Ndiyo maana zinapotokea huduma za bure za afya, unakuta maelfu ya watu wakijitokeza.
Tuna mifano ya meli ya Wachina iliyowahi kuja Tanzania pale bandarini Dar es Salaam. Tuliona maelfu ya Watanzania wakijitokeza. Watu wakikanyagana na wengine wakilala palepale kusubiri huduma ya bure.
Hata madaktari bingwa katika ziara zao za huduma za bure kwenye mikoa, tunaona wananchi wakijitokeza kwa wingi kupata huduma.
Hii inaonyesha wananchi wana matatizo mengi, lakini kutokana na gharama muda mwingine wanaona ni bora wawe wanakaa na matatizo yao majumbani mwao.
Suluhu ni ipi?
Wapo wanaosema tunahitaji kuwa na mfumo wa bima ya afya kwa wote kama sehemu ya kulinda afya ya Watanzania.
Lakini watu hawa wanasahau kuwa bima ya afya si suluhu ya tatizo hili, kwa sababu hiyo bima yenyewe nayo ina matabaka ya walio nacho na wasio nacho.
Kuna bima za bei rahisi na zile bei kubwa na zinatofautiana kwenye matibabu. Kwa hiyo, bima ni mwendelezo wa hiki tunachokiona kinaitwa michango ya matibabu ya wagonjwa.
Nilimsikia Waziri wa Afya alipofanya kikao na watu wa NHIF, anawahimiza waongeze kasi katika kuandikisha wanachama wapya hasa wasiougua ili wawachangie wanaoumwa.
Lakini tunasahau kuwa hata hao wanaoumwa na wanaochangia bado hawapati tiba stahiki. Kupitia kipindi cha ‘Kurasa’ cha Kituo cha East Africa Television cha Februari 12, 2022, walionyesha wanakijiji wa Nyamalogo, mkoani Shinyanga, wakitoa malalamiko yao kuwa wamekata bima ya CHF lakini wakienda hospitalini hawapati huduma.
Wanaona bora wasubiri, wakiumwa wakalipie tu moja kwa moja. Hii ni moja ya changamoto katika bima.
Nafikiri lazima tufikirie mfumo wa taifa wa afya ambao hautasukumwa na pesa, bali ni kuwahudumia wananchi bila kujali hali ya vipato vyao.
Na hili linathibitishwa na mwananchi mmoja ambaye niliwahi kuzungumza naye juu ya suala la afya Tanzania.
Alinielezea uzoefu wake alipokuwa anamuuguza ndugu yake katika moja ya hospitali kubwa hapa nchini. Anasema kama hauna fedha ni matatizo makubwa kupata huduma hospitalini.
Mwishowe walimpoteza ndugu yao. Lakini anaonyesha fedha zimetawala sana.
Katika mjadala huo, mwananchi huyo alitoa suluhu na kusema inabidi serikali ifanye sekta ya afya kuwa bure, elimu ndiyo watu walipie, kwa kuwa unaweza kuishi bila elimu, lakini si afya.
Pia elimu unaweza kusuburi kwa kutafuta fedha na ukalipa baadaye, lakini afya haina kungojea, ukingojea unakufa.
Katika mjadala huo, alitokea mwananchi mwingine, yeyeanasema kuwa mfumo wetu wa afya kwa watu maskini, unawapa shida sana.
Yeye aliita mfumo wa afya unaongozwa na mkono wa ndugu. Anamaanisha kuwa kutokana na gharama za matibabu, ili mgonjwa ahudumiwe, inahitajika ndugu na jamaa kuchanga ndipo zipatikane fedha za kumtibu mgonjwa. Mfumo huu yeye anauita ‘Mkono wa ndugu’.
Yeye anasema kuwa hatuna budi kuitazama sekta ya afya kwa karibu sana. Wananchi watibiwe bure, maana kama tutafanya fedha ziwe sehemu ya afya zetu, wananchi maskini watashindwa tu.
Mimi pia naungana na wananchi hawa kuwa suluhu ya kudumu ni kuifanya afya iwe bure kwa wananchi wote. Wananchi wasiwe na hofu kuhusu afya zao.
Tunaweza kujadili suala la kuhudumia sekta ya afya kwa kutafuta mapato, lakini kusiwe na mjadala wa afya, lazima iwe bure, ili kuokoa maisha ya Watanzania wengi ambao tunaona kila kukicha wakiomba michango kwenye vyombo vya habari, wakiwaasa Watanzania wenzao wawachangie.
Na muda mwingine inashangaza hata wale ambao tunaona wana uwezo wa kugharamia nao wanashindwa kulipia.
Hii pia inaonyesha hakuna aliyekuwa na uwezo huo, sasa kama hata hao wenye uwezo nao wanashindwa, maskini wa kawaida itakuwaje?
Suala hili litufanye kuifanya huduma ya afya iwe bure. Sera na sheria zetu ziwekwe katika namna ya kutoifanya afya kuwa bidhaa na kila mwananchi aipate.
Rai yangu
Tusione kuwa ni suala la kawaida watu wanaokumbwa na magonjwa kuomba michango, bali tuchukue suala hili kama sehemu ya kuutafakari mfumo wetu wa afya. Kwa hali inavyoendelea hatutaweza kugharamia matibabu ya afya zetu.
Ni familia chache sana zenye uwezo wa kumudu huduma za afya. Lakini walio wengi ni wahanga wa mfumo huu wa afya wa uchangiaji (cost sharing), ambao unawaweka watu kwa mafungu na upana wa mifuko yao ya kifedha na ndio unaamua aina gani ya matibabu utapata.
Mwandishi wa makala hii ni Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge (MWECAU).
0683 961891/0659 639808 [email protected]