Uchaguzi Mkuu ulioisha wa 2015 umenipa changamoto ya kutafakari, nikichukulia kwamba Uchaguzi Mkuu ni kwa ajili ya kutafuta uongozi wa nchi, nimetafakari kuhusu uongozi na saratani vitu viwili tofauti ambavyo lakini vinafanywa kufanana hapa nchini kwetu bila kukusudia. 

Kwa jinsi chama tawala hapa nchini kilivyokuwa kimejipanga katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, 2015, haikuonesha hata kidogo kama kinafahamu kitu mabadiliko ya kisiasa katika mfumo wa uongozi wa nchi. 

CCM ni kama inaamini kwamba uongozi wa nchi maana yake ni yenyewe kubaki madarakani milele yote, basi, bila kuelewa kuwa huo ni udumavu ulio sawa na saratani ya aina fulani. 

Saratani ni aina ya ugonjwa mbaya sana ambao unasababisha mwili utengeneze aina fulani ya ukuaji usio wa kawaida, mara nyingi husababisha udumavu, ha hivyo kuyafanya maisha ya mwenye ugonjwa huo kuwa katika hatari ya maangamizi.

Kwa upande wa pili uongozi ni usimamiaji wa maendeleo, ni lazima kitu kilicho chini ya uongozi kiwe na mwelekeo wa maendeleo, vinginevyo uongozi unakuwa hauna maana ya kuwepo sababu utakuwa umejigeuza saratani ndani ya jamii.

Jamii inapodumaa, ikakosa maendeleo, tayari uongozi wake unakosa sifa ya kuendelea kuwepo na kubaki umejifananisha na saratani kwa maana ya kusababisha udumavu.

Nchi nyingi zilizoendelea zinauheshimu uongozi, heshima inayotolewa kwa uongozi wa nchi hizo inatokana na kukubalika kwa mabadiliko ndani ya mfumo wa uongozi wa nchi hizo.

Mabadiliko hayo yanajionyesha yalivyo na tija kubwa kwa nchi hizo. Kitu chenye kuendelea ni lazima kiwe na mabadiliko, pasipo na mabadiliko maendeleo hakuna, ni udumavu tu.

Marekani kwa mfano, hiyo ni nchi yenye maendeleo makubwa yaliyoifanya iwe nchi tajiri sana duniani na yenye nguvu kubwa vilevile.

Chanzo cha hayo yote ni mabadiliko katika mfumo wa uongozi wa nchi hiyo ambao sio wa kubadili tu nafasi za viongozi wa juu bali mfumo mzima wa uongozi. 

Nchi hiyo imebadili mfumo wa uongozi mara saba tangu ipate uhuru wake mwaka 1776 ikiwa na Rais wa kwanza,  George Washington,  mpaka mwaka 1827, ikiwa na Andrew Jackson,  ambacho ni kipindi cha miaka 50.

Ikumbukwe kwamba kwa nchi zetu za Kiafrika hicho ni kipindi kinachotaka kung’ang’aniwa na mtu mmoja tu akiwa madarakani!

Tangu Tanzania ipate uhuru wake, naangalia kwa upande wa Tanganyika, huu ni mwaka wa 54, haijawahi kufanya mabadiliko kwenye mfumo wa uongozi wake hata mara moja.

Kinachofanyika ni kubadili tu viongozi wa juu (marais) lakini mfumo ukibaki ni uleule, jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa udumavu wa maendeleo ya nchi yetu.

Ndiyo maana hata baada ya kipindi hicho cha zaidi ya nusu karne bado nchi yetu haioni aibu ya kujiita taifa changa huku ikideka na kuomba karibu kila kitu hata kile kilicho katika uwezo wake wa kukipata kwa nguvu zake yenyewe!

Kwa mtindo huo ambao Tanzania imeukumbatia sidhani kama kuna uwezekano wowote wa nchi hii kuachana na “uchanga” inaotamba nao na kuugeuza mtaji maalumu hata baada ya miaka elfu moja ijayo.

Hiyo ni kwa sababu nchi yetu imeyakataa mabadiliko ya msingi katika mfumo wa uongozi wake kitu ambacho ni sawa na kuukumbatia udumavu.

Hiyo inanikumbusha baadhi ya watu katika kabila la Wahaya wanaoambiwa wakatoe funza miguuni mwao, lakini wao kwa hasira wanajibu kwamba njoo ukazile, funza, ambapo matokeo yake miguu yao inalemaa na kung’oka kucha za vidole vya miguu kutokana na kuliwa na funza.

Kwa hiyo kutoyakubali mabadiliko kwenye mfumo wa uongozi wa nchi ni sawa na kuufananisha uongozi na saratani katika mwili wa binadamu. Ni kuikaribisha hatari ya udumavu na hatimaye mauti.

Uongozi wowote unaoyachukulia mabadiliko ndani yake kama uadui mara zote huishia kwenye maangamizi, kwa uongozi wenyewe na hata kwa dola linaloongozwa wakati mwingine.

Mifano ni mingi, iliyo hai na hata iliyo kwenye masimulizi ya kusadikika. Mfano katika tamthiliya ya Julius Kaizari, mfalme mmoja jasiri aliyekuwa akiyachukulia mabadiliko kama uadui kwenye utawala wake aliupuuza ushauri wa mtabiri mmoja uliomtaka ajihadhari na nyakati fulani za mwaka ambapo mtabiri alisema “Caesar beware the ides of March”.

Lakini mfalme huyo, kwa ulevi wa madaraka, akadai kwamba hizo ni kauli za woga za nakufa nakufa, akisema kwamba waoga hufa mara nyingi kabla ya vifo vyao, lakini jasiri hafi bali mara moja tu.

Matokeo ya mfalme kuupuuza ushauri wa mtabiri huyo aliyekuwa akiyaona mabadiliko mbele ya safari yalikuwa ni maangamizi mabaya sana kwa mfalme huyo jasiri.

Mfalme huyo alifikia kuwashangaa hata washauri wake muhimu aliokuwa akiwaamini kwa ushauri wao wa kuyakandamiza mabadiliko pale watu hao walipokuwa wa kwanza kumuangamiza katika kuyasafishia njia mabadiliko ya kweli.

Mifano mingine iliyo hai ni Idd Amini aliyekuwa kiongozi wa Uganda. Yeye alifikia kujiita rais wa maisha akiamini kwamba hakuna mtu mwingine ambaye angeweza kumuondoa kwenye madaraka katika nchi hiyo. 

Mwingine ni Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa Zabanga, aliyekuwa kiongozi wa Zaire, Kanali Muamar el Gadafi wa Libya na wengine wa aina hiyo.

Hao wote waliyapinga mabadiliko katika utawala wao wakiamini kwamba uongozi wao ni wa kudumu milele yote kumbe ulishageuka saratani iliyoishia kuwaangamiza wao!

Kwa mantiki hiyo tunapousema uongozi wa nchi hatunabudi kukitilia maanani kitu mabadiliko, sababu pasipo na mabadiliko ni lazima patadumaa na kukosa maendeleo. Ni sawa na mwili uliopata ugonjwa wa saratani. 

Na kwa sheria ya asili hicho ni kitu kisichokubalika, ni lazima papatikane njia ya kuliondoa tatizo hilo, na mara zote njia ya aina hiyo huwa siyo salama. Huacha tu makovu yasiyofutika katika historia ya kila mahala panapotokea tatizo la aina hiyo.

Mwisho niseme kwamba Rais John Magufuli ni Rais wa tano wa awamu ya tatu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na wala siyo rais wa awamu ya 5 kama inavyosemwa kutokana na kutoyatafakari mambo.

Tanzania ni nchi iliyopitia katika awamu tatu za uongozi mpaka sasa. Awamu ya kwanza ilikuwa ni ya serikali ya vyama vingi vya siasa ikimshuhudia rais mmoja, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, awamu ya pili ikawa ya serikali ya chama kimoja cha siasa na kuwashuhudia marais wawili, Mwalimu Julius Nyerere na Mwalimu Ali Hassan Mwinyi, baadaye ikaja tena awamu ya tatu ya serikali ya vyama vingi vya siasa ambayo imewashuhudia marais watatu mpaka sasa, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na John Magufuli. Hao ni marais watano wa Tanzania katika awamu tatu za uongozi wa nchi yetu.

 

[email protected]

0784 989 512