Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikiwa kinajiandaa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, kimesema kitaendelea kutekeleza majukumu yake kwa haki kwa kuzingatia Katiba na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emanuel Nchimbi, aliyasema hayo leo, Februari 19, 2025, wakati akifungua mafunzo kwa Watendaji wa Kata na Makatibu wa Matawi wa CCM Mkoa wa Dodoma.

Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, Dkt. Nchimbi amekemea vikali utaratibu unaoenezwa na baadhi ya makada wa CCM wa kutumia matukio ya kumbukizi za kuzaliwa na ndoa kama njia ya kuwahadaa wanachama kwa kuwalipa posho ili kupata faida katika uchaguzi.

Amesisitiza kuwa CCM ina mfumo madhubuti wa kufuatilia matukio hayo na kwamba wale wanaojihusisha na vitendo vya namna hiyo wataenguliwa katika mchakato wa kugombea.

“Chama chetu kina mfumo wa kufuatilia kila kinachotokea, na kumbukumbu hizi tutakazozikusanya zitawaengua wale ambao hawatendei haki chama na wanachama,” amesema Dkt. Nchimbi.

Aidha, Dkt. Nchimbi ameelezea kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo lengo kuu ni kuwa na watendaji wa chama wanaojua wajibu wao na kujitahidi kushinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge, na Madiwani.

“Lengo la chama chochote cha kisiasa ni kushika dola. Kwa upande wetu, dola tumeshika, lakini kushinda kunategemea wanachama wetu. Hivyo, ni muhimu kuwa waadilifu ili chama chetu kielekee ushindi,” ameongeza.

Kwa upande mwingine, Katibu wa NEC Organization, Issa Haji Gavu, amesisitiza umuhimu wa mafunzo hayo, akisema yanafanyika kwa mujibu wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia na yanalenga kuimarisha ufanisi wa chama kuanzia ngazi ya Shina hadi Taifa.

Katibu Mkuu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pili Mbaga, ameongeza kuwa mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kuleta mabadiliko na kuelekeza namna bora ya kufanya kazi kwa ufanisi, na kwamba yatasaidia kuwaleta watendaji wa kata na matawi katika mstari mmoja wa utendaji.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za chama katika kuhakikisha kinakuwa na uongozi thabiti na wenye maadili bora, ukijitahidi kudumisha umoja, haki, na usawa kwa wanachama wake.

Pamoja na mambo mengine Uchaguzi Mkuu wa 2025 unakaribia, na CCM inaelekeza nguvu zake zote kuhakikisha kuwa inapata ushindi wa kishindo, kwa kuhakikisha kuwa viongozi wake wanatenda haki, na wanajiandaa vyema kwa majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya chama hicho.