Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Chama Cha Wanaume Wazee Mkoa wa Dodoma kimewanyooshea vidole Wazazi na walezi ambao hawawajibiki katika malezi ya watoto kwenye ngazi za familia na kueleza kuwa hali hiyo inachangia kukithiri kwa vitendo vya mmonyoko wa maadili pamoja na vitendo vya ukatili hapa nchini.

Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Dodoma Mzee Peter Mavunde amezungumza hayo leo Dodoma November 23 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Mafanikio na Changamoto katika mwaka 2024 na matarajio ya Chama hicho mwaka 2025.

Amesema hali hiyo inasababishwa na wazazi na walezi kutumika muda mwingi katika shughuli za utafutaji wa kipato Kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa familia na kusahau jukumu la malezi.

Amesema ili kuondokana na hayo jamii inapaswa kuzingatia miongozo ya malezi itakayoweza kumsaidia mtoto wa kitanzania kukuwa katika misingi inayozingatia uchamungu na maadili .

“Suala la mmomonyoko wa Maadili katika jamii bado haliko sawa, changamoto za malezi mabovu ngazi ya familia ndio chanzo kiku lazima tusaidiane malezi ili kupunguza matukio ya mmomonyoko wa maadili,ni wakati wa familia kufikiri upya kuhusu namna ya kutekeleza jukumu la makuzi na Malezi ya watoto, “amesisitiza

Mzee Mavunde pia amesisitiza,”Malezi kwa sasa yamekuwa magumu Sana kwa sababu ngazi ya familia imeacha ule utamaduni wa kukemea makosa kuanzia ngazi ya msingi kabla ya Jamii kwani zamani sisi ukikosea mtu yeyote anaweza kukuadhibu na ukifika nyumbani kwenu bado unaadhibiwa, “anasema

Hata hivyo Mzee Mavunde amewataka vijana kuwakumbuka wazee wao wasiwatelekeze kwani kufanya hivyo ni kujifungia Baraka ambazo wangezipata kwa kuwahudumia Wazee.

Sambamba na hayo amesema chama hicho kitaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya watanzania katika nyanja zote ikiwemo afya,elimu na miundombinu.

Kwa kidhihirisha hilo amessema siku zote wamekuwa wakilaani uharibifu wa Miundombinu unaofanywa na watu wenye nia ovu ikiwemo ya Reli na Barabara hali inayorudisha nyuma juhudi za Serikali nyuma katika Maendeleo.

Amesema matukio ya uharibifu na wizi wa miundombinu ni matumizi mabaya ya Kodi za Wananchi .

“Suala la uharibifu wa miundombinu sisi kama wazee hatuwezi kufumbia macho tunaungana na Serikali kulaani kwani wanaofanya hivyo Wanacheza na jasho la Watanzania ambalo ni kodi,” ameeleza Mzee Mavunde

Kwa upande wake Mzee Komredi Ntemo Mohamed amesema Serikali inapaswa kuwachukulia hatua wanaohujumu miundombinu huku akiwataka wazee kutimiza wajibu wa kushiriki kikamilifu katika malezi .

Amesema wao kama wazee waliolitumikia taifa kwa muda mrefu hawapendi kuona jamii inapotea hivyo wataanza kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kushiriki kwa kuzingatia misingi ya maadili