Siku zote wachezaji wavivu ndio wanapenda kulalamika mno uwanjani. Kauli kama hii iliwahi kusikika: “Aaah! Ticha inatosha bwana, kwa leo inatosha.” Huyo ni mchezaji wa zamani wa Yanga akimwambia kocha wake kuwa muda wa mazoezi umekwisha, hivyo apulize filimbi ya kumalizia zoezi la kuzunguka uwanja.
Si simulizi, ni hali halisi, si hadithi ya kubuni kutoka kwenye kichwa cha mtu, ni tukio la kweli lilitokea kwenye Uwanja wa Kaunda, wakati huo Yanga wakiutumia kwa mazoezi. Alikuwa ni mmoja wa washambuliaji wazuri hapa nchini.
Hivi sasa ni mmoja wa maveterani wanaowalaumu wachezaji wa sasa kwa kuendekeza uvivu. Hawezi kukumbuka tukio linalomhusu, ambalo ni kielelezo cha yeye kuwa mvivu kama wachezaji ambao anawatoa kasoro akiwa amekaa na marafiki zake sehemu fulani ya Jiji la Dar es Salaam.
Wakati mwingine mchezaji wa Tanzania anaweza kuhisi kana kwamba anasakamwa kwa maneno, lakini anayekuambia ukweli ndiye anayekutakia mema maishani mwako.
Wachezaji wengi ambao wanaziwakilisha timu zao za taifa huku wakitokea Ulaya na kwingineko, wana tabia ya kucheza mechi za kutafuta nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia na zile za Mataifa ya Afrika (AFCON), kwa tahadhari kubwa. Wanazitunza nguvu zao kwa ajili ya ligi kuu za nje ambako wanalipwa fedha nyingi, kwa kufanya hivyo huonekana kama watu wasio na uzalendo kwa mataifa yao.
Samuel Eto’o aliyekuja na timu ya taifa ya Cameroon, miaka kadhaa iliyopita, alicheza soka la kutotumia akili ya ziada, alimfanyia masihara Shadrack Nsajigwa pembeni mwa uwanja.
Alikwepa kuingiza mwili kwenye matukio ambayo alihisi angeweza kuumizwa, alicheza kirafiki zaidi. Lakini Samuel Eto’o huyo huyo akaja kucheza mpira wa hali ya juu, bila ya utani wa aina yoyote ile kwenye mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Inter Milan dhidi ya Bayern Munich mwaka 2010.
Mchezaji wetu anayemwambia kocha kuwa muda wa mazoezi umekwisha hivyo apulize filimbi ya mwisho, hawezi kufanana na mchezaji ambaye anaiheshimu ajira yake ya nje ya nchi, kiasi cha kujikuta akilaumiwa kwa kukosa uzalendo.
Mchezaji wetu atachezea timu moja ya mikoani halafu atakuja kuchezea Yanga, Simba au Azam FC kwa misimu michache, baada ya hapo anaingia mtaani kufanya shughuli nyingine. Pia anageuka kuwa mkosoaji wa wadogo zake ambao pengine kama yeye angefanikiwa, kungekuwa na uwezekano wa hao wadogo kuyatumia mafanikio yake kama kioo cha kujipima na kuongeza umakini uwanjani.
Mchezaji anayemwambia kocha mzalendo kwamba muda wa mazoezi umekwisha, hawezi kuthubutu kumwambia kocha wa kutoka nje ya nchi eti apulize filimbi ya kumaliza mazoezi. Atakuwa anajitafutia sababu ya kupewa adhabu kali na pengine mwisho wa msimu anaweza kutemwa.
Uvivu umekuwa ni chanzo kikuu cha wachezaji wetu ndani ya klabu na hata timu ya taifa kukosa mafanikio. Vijana wengi wanaotamba katika timu nyingi za ligi kuu wanayo bahati ya kucheza soka katika nyakati ambazo maisha ya nje ya uwanja yamerahisishwa.
Wanaukosa ukakamavu ambao walitakiwa wawe nao kupitia mazoezi ya ziada; na siku zote chokochoko za kuwatimua makocha huanzishwa na wachezaji wavivu, wasiotaka mabadiliko katika maisha yao ya soka.
Kocha anayeonekana kuwa mkali ni yule asiyependa uvivu wakati wa mazoezi, ambaye anataka kazi yake isiharibiwe na mchezaji mmoja asiyejitambua. Hakuna mkamilifu chini ya jua, wachezaji wetu wanaoshindwa kuendana na matakwa ya makocha wakiwa bado Tanzania, watayaweza vipi maisha ya soka nje ya nchi?
Kwenye timu moja kuna beki kutoka Cameroon, anagombea namba na beki kutoka Brazil, kuna mfungaji wa magoli kutoka Nigeria anagombea namba na yule anayetoka Ufaransa.
Utashangaa sana kwenye mazoezi kama ya timu ya taifa, mchezaji anafundishwa jinsi ya kupiga pasi. Ni mchezaji mvivu tu asiyejua jukumu lake ndiye anayefundishwa hili.
Pia tukubaliane kwamba kwa mchezaji mvivu kudumu ndani ya ligi kuu ni lazima awe na roho ngumu, hata mafanikio yetu pia ndani ya soka yanatakiwa tuwe na wachezaji wenye roho ngumu.
Ila kwa ufupi, hakuna muda wa kocha kumdekeza mchezaji, na kauli yake ndiyo ya mwisho. Filimbi ya kumaliza mazoezi inapulizwa kwa mujibu wa ratiba anayoifahamu kocha mkuu. Wachezaji wavivu ni maadui wa mafanikio ya maisha yao binafsi, pia ni maadui wa soka letu kwa ujumla.