Umiliki wa ardhi hutolewa kwa masharti maalumu. Kila aliyepewa hatimiliki anajua kuwa amepata hati hiyo kwa masharti ambayo anapaswa kuyatekeleza.
Wapo ambao hudhani kuwa ukishapewa hati na masharti, basi ni hivyo hivyo tu, hauna la kufanya hata kama hujaridhika au hunufaishwi na masharti hayo.
Hii ni fikra isiyo sahihi. Sasa wapaswa kujua kuwa masharti katika hatimiliki ya ardhi yanaweza kubadilishwa kwa maombi maalumu. Masharti ni kwa ajili ya maendeleo na kwa ajili ya maendeleo waweza kuomba kubadilishiwa masharti/sharti la umiliki.
1. 1. Ni masharti yapi huwekwa katika hatimiliki?
Yapo masharti mengi. Kifungu cha 34 cha Sheria Namba 4 ya Ardhi kimeeleza masharti ya hatimiliki. Baadhi ya masharti hayo huwa ni pamoja na matumizi, kwa mfano, utaambiwa unapewa hati ya eneo hili ni kwa ajili ya biashara tu, viwanda tu, hoteli tu, makazi tu, nk.
Au utaambiwa unapewa umiliki wa ardhi kwa miaka 33, 66, au 99. Au utapewa sharti kuhusu ujenzi, kwa mfano utaambiwa eneo hili huruhusiwi kujenga jengo lisilo la ghorofa, au eneo linaruhusiwa kujengwa jengo la chini tu, au pajengwe jengo lisilo la kudumu nk.
Haya ni baadhi ya masharti unayoweza kupewa wakati unapokuwa ukipewa hatimiliki.
1. 2. Utaratibu wa kuomba kubadilishiwa masharti
Ndiyo, unaruhusiwa kuomba kubadilishiwa masharti au sharti kulingana na mahitaji yako. Unaweza kuomba muda wowote baada ya kupewa umiliki au wakati mchakato wa kupatiwa umiliki ukiendelea.
Utaratibu wake ni huu:-
(i) Utatakiwa kujaza fomu namba 27 ambayo inaeleza matumizi ya sasa na yale mapya unayoomba kubadilishiwa. Fomu hii inapatikana kwenye kanuni za Sheria namba 4 ya Ardhi, za mwaka 2011, pia zinapatikana ofisi za Ardhi na kwa wanasheria.
(ii) Fomu hiyo itaambatanishwa na nakala ya hati husika, picha za mwombaji, na ada ya maombi ya kubadilisha.
(iii) Itakuwa imesainiwa na mwombaji au wakili wake.
(iv) Itaambatana na risiti za karibuni za malipo ya kodi za ardhi au jengo.
(v) Pia utaambatanisha taarifa nyingine yoyote ambayo unaweza kuombwa kuwasilisha na mamlaka za ardhi.
(vi) Maombi hayo yatapelekwa kwa Kamishna wa Ardhi, kwani ndiye mwenye mamlaka na mchakato huu.
1. 3. Kukubaliwa mabadiliko ya masharti
Unaweza kukubaliwa maombi au kukataliwa au kubadilishwa wa kile ulichoomba. Endapo utakubaliwa basi Kamishna atakutaarifu kwa taarifa maalumu kupitia anuani na mawasiliano uliyotumia kwenye maombi.
Atakutaka kuwasilisha kwake hatimiliki halisi ili aingize mabadiliko mapya na kutia muhuri wake. Pia atakutaarifu mabadiliko mapya ya malipo ya kodi na tozo za ardhi kutokana na matumizi mapya.
1. 4. Adhabu ya kukiuka masharti
Kifungu cha 45 cha Sheria namba 4 ya Ardhi kimesema kuwa ukiukwaji wa masharti ya umiliki wa ardhi utasababisha hati ya mmiliki kufutwa. Kufutiwa umiliki wa ardhi maana yake ni kunyang’anywa ardhi.
Kwa hiyo, ni muhimu kuendana na masharti haya na panapo tatizo au hitaji la kubadili sharti kwa ajili ya maendeleo, basi omba ubadilishiwe kuliko kujibadilishia matumizi bila kufuata taratibu; jambo ambalo linaweza kugharimu ardhi yako yote.