NA BASHIR YAKUB
Jina la kampuni linajulikana. Ni lile jina ambalo kampuni yako inatumia kama
utambulisho wake. K & Company Ltd, Sote Company Ltd n.k. Jina hili laweza
kubadilishwa wakati wowote baada ya kusajili kampuni.
Sheria imeruhusu jambo hili na hakuna anayekulazimisha kuendelea na jina
ambalo unahisi halipendezi kwa kampuni yako.
1. Jina la kampuni hupatikanaje?
Katika hatua za kuunda kampuni, kutafuta jina ni moja ya hatua za awali kabisa.
Huwezi kuanza mchakato wa usajili wa kampuni kabla ya kupata jina. Na
upatikanaji wa jina ni kuwa unachagua mwenyewe jina unalolipenda au ambalo
ungependa kampuni yako iitwe.
Baada ya kuchagua jina hilo, utatakiwa ufanye maombi maalumu kwa msajili wa
makampuni kwa uhakiki. Uhakiki ni pamoja na kujua kama ipo kampuni yoyote
inayotumia jina hilo ama la. Kama kuna kampuni ambayo inatumia jina hilo basi
msajili atakujibu kuwa jina hilo lipo na hivyo utafute jina jingine. Na kama halipo
basi utaambiwa halipo na kuwa ni ruhusa kulitumia.
Hatua hii si tu unapokuwa unasajili kwa mara ya kwanza bali hata wakati wa
kubadili utapitia hatua hii.
Jambo la kuzingatia ni kuwa jina lolote utakalochagua hakikisha siyo tusi, halilengi
kuleta ubaguzi wa dini, jinsia, rangi ama kabila, lisiwe jina linalotumiwa na taasisi
za serikali, nk.
2. Hatua za kubadili jina la kampuni
Hatua ya kwanza ni kuitisha mkutano wa wanahisa (shareholders extraordinary
meeting) ili kukubaliana kuhusu kubadili jina la kampuni. Hata wanahisa wawe ni
wewe na mke wako au mtoto au rafiki bado ni wanahisa na mkutano huu
unatakiwa.
Hatua ya pili katika mkutano huo mtapitisha uamuzi rasmi wa kampuni (company
resolution) kuwa wanahisa mmekubaliana kubadili jina la kampuni. Nyaraka
maalumu ya uamuzi rasmi wa kampuni (company resolution) itaandaliwa na
kusainiwa.
Hatua ya tatu, mtajaza fomu inayoeleza kubadili jina la kampuni na ni lipi jina
jipya. Fomu hizi mtazipata kwenye kanuni za sheria ya makampuni za mwaka
2005 au kwenye mtandao (website) wa BRELA.
Hatua ya nne, chukua hiyo nyaraka ya uamuzi rasmi wa kampuni (company

resolution) pamoja na hiyo fomu mliyojaza, ambatanisha kwa pamoja kisha peleka
BRELA kwa taarifa na usajili wa jina jipya. Hapa pia utalipia ada ya kubadili.
Hatua ya tano baada ya kujibiwa na kukubaliwa jina jipya sasa unaweza kuanza
kutumia jina jipya kwenye shughuli zote za kampuni.
3. Kubadili jina hakuondoi wajibu na uwajibikaji wa kampuni
Kampuni haitaacha kudai au kudaiwa kwa kuwa imebadili jina. Madai na madeni
ya kampuni yanabaki palepale hata kama mikataba kuhusu madai na madeni
hayo imeandikwa jina ambalo halitumiki sasa.
Na siyo madeni tu bali mikataba yote na mambo yote ya utekekezaji mfano; ajira
wafanyakazi, biashara, dhamana n.k yatatakiwa kutekelezwa kama mikataba
inavyosema hata kama mikataba hiyo inasoma jina ambalo halitumiki sasa.
Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, kampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA
YAKUB BLOG
Ends