Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Serengeti

Mkazi wa Kijiji cha Nyankomogo Kata ya Rigicha, John Warioba Riana (33), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Serengeti kwa tuhuma za kumbaka mtoto wa miaka (13).

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Serengeti Jakobo Ndira,Mwendesha Mashitaka wa Jamhuri Renatus Zakeo amesema kuwa mtuhumiwa anadai kutenda kosa hilo Julai 13,mwaka huu,saa 5 asubuhi,katika kijiji cha Issenye.

Amedai kuwa mtuhumiwa katika kesi hiyo ya jinai Namba 56/2022 anadaiwa kutenda kosa hilo baada ya kumkamata mtoto huyo kwa nguvu na kumwingiza ndani ya nyumba ambayo haitumiki na kumbaka.

Amedai,kabla ya kutenda kosa hilo mshitakiwa alikutana na mtoto huyo ambaye alikuwa akitoka katika Kijiji cha Manchiweru Wilaya ya Bunda akielekea Kijiji cha Issenye Wilaya ya Serengeti.

Mtuhumiwa alimlaghai kuwa anafahamu mji anaoenda hivyo akaahidi kumpeleka,hata hivyo njiani alimkamata kwa nguvu na kumtendea ukatili huo.

Upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kesi imehairishwa hadi Agosti 22, mwaka huu, na mtuhumiwa yupo mahabusu kwa kukosa wadhamini.