Maofisa wa halmashauri za wilaya nchini waliosimamia Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2015 wameanza kuchunguzwa kwa matumizi mabaya ya fedha. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema baadhi yao wamekwisha kufunguliwa mashitaka wakituhumiwa kuandaa nyaraka za uongo kuficha upotevu wa mamilioni ya shilingi. Miongoni mwao ni aliyekuwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Jimbo la Mwanga, mkoani Kilimanjaro, Hassan Mkwizu, anayeshitakiwa kwa makosa ya kughushi nyaraka na kufuja fedha za umma. Mkwizu na Mhasibu Msaidizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Mustafa Haji na Mtunza Kumbukumbu, Monica Mkasa wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanga. Mwendesha Mashitaka kutoka Takukuru, Suzan Kimaro, amesoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Mariam Lusewa.
Kwenye hati ya mashitaka, kosa la kwanza linamkabili mshitakiwa wa pili, Mkwizu, anayedaiwa kuwa Oktoba 22, 2015 akiwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi katika halmashauri hiyo, alighushi nyaraka zenye majina ya watu 220 akidai kuwa walikuwa ni walinzi. Pia anadaiwa kuandaa nyaraka za uongo kwa lengo la kumdanganya mwajiri na kuonyesha kuwa walinzi hao walilipwa posho ya jumla ya Sh. milioni 11 kwa ajili ya kusimamia Uchaguzi Mkuu wakati akijua si kweli. Katika kosa la tatu, mshitakiwa huyo anadaiwa kufuja Sh. milioni 11 ambazo ni fedha za Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga. Mtuhumiwa alikana mashitaka yote. Shitaka la nne linawakabili washitakiwa Haji na Mkasa wanaodaiwa kumsaidia Mkwizu kutenda kosa kinyume cha Kifungu cha 30 cha Sheria ya Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007. Washitakiwa wote walikana mashitaka hayo na wako nje kwa dhamana. Kesi hiyo itatajwa Julai 19, mwaka huu. Takukuru pia imemfikisha mahakamani mfanyabiashara Abdallah Majungu, akishitakiwa kwa kosa la kumsaidia Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Mkwizu, kutenda kosa lililomwezesha kujipatia Sh. milioni 12.4. Imedaiwa kuwa fedha hizo zilitolewa na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ajli ya kukodi magari 20 na vipaza sauti 20 ambavyo vingegawanywa katika kata 20 za Jimbo la Mwanga. Kandarasi hiyo ya kusambaza vipaza sauti ilitolewa kwa mfanyabiashara huyo na nyaraka zikaonyesha kuwa amelipwa fedha na kuonyesha kazi hiyo ilifanyika, lakini Takukuru wanadai kuwa kazi hiyo haikufanyika. Takukuru wanadai kuwa matangazo ya kuhamasisha wapiga kura katika kata zote yalitolewa kwa kutumia gari la serikali lililoazimwa Idara ya Maji Wilaya ya Mwanga. Mfanyabiashara huyo amefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mwanga, Jacqueline Osujaki na kusomewa mashitaka na Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Suzan Kimaro. Mtuhumiwa alikana mashitaka yake na yuko nje kwa dhamana. Shauri hilo litatajwa Julai 19, mwaka huu. Wilayani Hai, Takukuru imemfikisha mahakamani Mhasibu wa Halmashauri
ya Wilaya hiyo, Eline Lema, akikabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wa Sh. milioni 5 za makusanyo ya ushuru wa Soko la Kwa Sadala. Inadaiwa kuwa Aprili 27, 2015 alipokea fedha kutoka kwa mmoja wa mawakala waliopewa zabuni katika soko hilo na akampa stakabadhi ya malipo yenye namba 00089902. Amefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Hai, Regina Moshi, na kusomewa mashitaka na Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Rehema Mgeta. Inadaiwa kuwa kitabu cha stakabadhi ya malipo kilichotumika hakikuwa kwenye kumbukumbu za vitabu alivyopewa na mwajiri wake. Mshitakiwa huyo hakutakiwa kujibu chochote kutokana na kosa lake kuangukia kwenye makosa ya uhujumu uchumi na mahakama hiyo kutokuwa na nguvu kisheria kusikiliza shauri hilo. Yuko nje kwa dhamana hadi Julai 23, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo.