Sehemu iliyopita, nilianza kuandika rejea ya makala niliyoiandika miaka 17 iliyopita. Nilisema kule India nako lile shirika la “Cashew Corporation of India” lililonunua korosho zetu zote lilishavunjwa. Hivyo wanunuzi binafsi walikuwa wanajinunulia korosho kiholela kwa viwanda vyao vya kubangulia korosho. Wakati wa vurugu za namna hii serikali yetu ikaruhusu soko huria kwa korosho! Matajiri wale wa India wakawatumia mawakala wale wafanyabiashara wa umoja wa korosho hapa kwetu. Endelea na sehemu ya makala hiyo na hitimisho la makala hii ya “Korosho bado ni umiza kichwa’.
Hapo sasa ikaonekana wazi wanunuzi wakuu wa korosho ni wale wale akina “Ote Dugu Moja”. Je, katika mazingira namna hiyo kweli mkulima “Mmetoa” au “Matambwe” au “Mmachinga” au “Mmakonde” atapata unafuu wowote kwa jasho lake? Hamna! Mambo yakizidi kuwa hovyo tu.
Baada ya kutoa hisia zangu hizo nadhani nieleze nini kifanyike kujinasua katika mazingira ya utatanishi namna hii. Kwanza kabisa marekebisho makubwa yafanyike toka serikalini hasa kifikra na kuiwezesha CBT kuwa na lile jukumu la kununua korosho zote za wakulima, wakaziweka kwenye maghala yao kwa matumizi ya viwanda vile vinavyofanya kazi na nyingine kuziuza kwa mnada kwa wanunuzi wote wa nje na wa ndani. Hili litawahakikishia wakulima pato lao, litawazuia madalali uchwara lukuki kwenda vijijini kulangua korosho kwa kipimo cha kopo la kimbo lijulikanalo kama “kangomba” na litahakikishia serikali kupata ushuru au kodi yake inaostahili.
Pili, mabenki yakopeshe CBT fedha za kununulia korosho kama yalivyofanya siku za nyuma enzi zile za “union”.
Tatu, CBT yenyewe ijitutumue kukarabati angalau kiwanda kimoja katika kila mkoa zinakolimwa korosho kwa wingi. Mpango namna hii utasaidia korosho za mkoa ule kubanguliwa pale pale zinapozalishwa na baadhi ya vijana wa mkoa ule wakajipatia ajira hasa akina mama kwa ule upande wa ubanguaji korosho;
Nne, kile kitengo kilichoko wizarani cha uendelezaji korosho kiondolewe tu badala yake wizara ibuni njia bora ya kulisimamia zao hili kikweli kweli.
Serikali ifufue “union” katika wilaya. Hivi vyama vya msingi vitaondoa kabisa madalali na mawakala wa wafanyabiashara wanaofurika kule Kusini msimu wa korosho. Kwa maneno mengine, soko huria liwe pale penye maghala ya CBT. CBT inaweza kufunga mikataba na wanunuzi kutoka India, Uchina, Vietnam, Singapore, Thailand na Indonesia na ikawa “exporter” mkubwa wa korosho.
Kwa njia hizi korosho haiwezi kuwa biashara kichaa, wala wakulima hawatayumbishwa, maana watajua wanamuuzia nani na wanauza wapi korosho zao. Aidha, bei ya korosho haiwezi kuyumbayumba (no fluctuations). Dira itakavyotolewa na CBT itakuwa ndiyo bei yenyewe. Hapatatokea swali la KOROSHO KULIKONI? Tena. Ugonjwa ukijulikana tiba inakuwa rahisi kupatikana.” MWISHO WA KUNUKUU.
Haya ni mawazo niliyoyatoa mwaka 2001, leo hii ni miaka 17 imepita hali imebadilika sana. Sasa kwanini Wabunge wa Kusini wasisaidiane, korosho zetu zitunufaishe wakulima wa Kusini? Mimi ninajisemea korosho limekuwa bado “umiza kichwa” kwa wana Kusini wote. Kila mtu anaumiza kichwa chake kufikiria kwa nini sisi wa Kusini hatuna zao la biashara kuliko korosho?
Hebu fikiria hali ilivyo katika Bodi ya Korosho, karibu wenyeviti wote wa Bodi wamekuwa wazawa wa kule kule Kusini (hata huyu wa sasa), na wajumbe wa Bodi ile wengi wao ni wazawa wa Kusini. Sasa iweje zao letu kubwa la biashara kule Kusini linakuwa na sokomoko namna hii? Inakuwaje hapo?
Zao hili sasa limeenea mikoa mingi hapa Tanzania, mathalani mikoa ya Tanga, Dodoma, Singida, Tabora, n.k. Vipi zao linaloelekea kuwa zao la taifa zima bado linasumbua vichwa vya Watanzania?
Tumemsikia Rais John Magufuli akiwa katika ziara yake Kanda ya Ziwa amekuwa anauliza, “Vile viwanda alivyoanzisha Baba wa Taifa kama MWATEX, MUTEX, SUNGURA TEXTLE na kile Kiwanda cha Maziwa pale Musoma viko wapi? Nani ameviua?” Hakupata jawabu lolote, na mimi nauliza, vile viwanda vya korosho kule Kusini je, nani ameviua? Jibu la hapa ni sisi Watanzania wenyewe. “Mvunja nchi ni mwananchi mwenyewe.” Methali ya Kiswahili inatuasa hivyo.
Tujisahihishe na tuwe wazalendo wa kweli. Nchi hii inajengwa na wenye moyo, lakini inaliwa au inamemenwa na wenye meno! Nabakia mzee mzalendo ‘pyua’ wa nchi hii.
MUNGU IBARIKI AFRIKA.