Wizara ya ulinzi ya Korea Kusini imewasimamisha kazi kamanda wa Kikosi Maalum Kwak Jong-keun, kamanda wa Ulinzi wa Ikulu Lee Jin-woo na kamanda mkuu wa ujasusi Yeo In-hyeong kwa kuhusika katika kutekeleza agizo la sheria ya kijeshi Jumanne usiku.

Waendesha mashtaka wamewasilisha ombi la kuwazuia makamanda hao kuondoka nchini humo wakiwemo maafisa wengine saba wakuu wa kijeshi.

Awali, Kwak alidai kwamba alipata agizo hilo kupitia vyombo vya habari na kwamba alikataa agizo la kuwaondoa wabunge kutoka katika majengo ya BungenI Jumanne.

Huku hayo yakijiri maelfu ya watu mjini Seoul wanatarajiwa kushiriki maandamano ya kabla ya wabunge kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais Yoon, polisi wamesema.

Kura hiyo imepangwa kufanyika jioni ya leo. Maandamano hayo yatafanywa katikati mwa jiji na eneo la Yeouido ambapo jengo la Bunge la Kitaifa liko.

Katika taarifa, polisi wa Seoul walisema msongamano wa magari unatarajiwa na maafisa watapelekwa kushika doria.