Siku moja kabla ya kufunguliwa kwa michezo ya Olympiki ya Majira ya Baridi
nchini Korea Kusini, Korea Kaskazini imefanya gwaride kubwa la kijeshi
kuadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa kwa jeshi la nchi hiyo.
Afisa wa Korea Kusini ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema kiasi ya
wanajeshi zaidi ya 13,000 walishiriki katika gwaride hilo lililokuwa na lengo la
kuonesha nguvu ya kijeshi ya nchi hiyo.
Gwaride hilo lililofanyika katika mji mkuu wa Korea Kaskazini, Pyongyang,
lilihudhuriwa na watu wapatao 50,000; hata hivyo, waandishi wa habari kutoka
nchi za kigeni hawakualikwa kuhudhuria hafla hiyo.
Wakati hayo yakiendelea, Korea Kusini imesema haijulikani iwapo Korea
Kaskazini iliweka silaha nzito kama makombora ya masafa marefu wakati wa
gwaride hilo lililohudhuriwa na wananchi wengi.
Wakati huo huo nchi ya Korea Kaskazini imesema haina mpango wa kukutana na
maafisa wa Marekani wakati wa michezo ya Olympiki ya Majira ya Baridi
inayotarajiwa kufanyika nchini Korea Kusini.
Tangazo hilo limekuja siku moja baada ya Makamu wa Rais wa Marekani, Mike
Pence, kusema kuwa yuko tayari kukutana na maafisa wa Korea Kaskazini wakati
wa sherehe za ufunguzi wa michezo hiyo.
Afisa mwandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini, Cho
Yong-Sam, amesema hakuna mpango wa kukutana na mwakilishi wa Marekani
kwa lengo la mazungumzo ya aina yoyote.
Serikali ya Marekani kupitia Makamu wa Rais wa nchi hiyo Mike Pence imesema
kuwa wataendelea kuishinikiza Korea Kaskazini hadi itakapoachana kabisa na
mpango wake wa nyuklia pamoja na makombora,
Makamu huyo wa Rais wa Marekani amewaambia waandishi habari kwamba
hawatoruhusu propaganda za Korea Kaskazini kuiharibu michezo hiyo ya
Olympiki ya Majira ya Baridi kwa namna yoyote ile.
Korea Kaskazini Yaonyesha Nguvu za Kijeshi
Jamhuri
Comments Off on Korea Kaskazini Yaonyesha Nguvu za Kijeshi
Previous Post
Mafanikio Yoyote Yana Sababu (9)
Next Post
Wabunge Wanapotangaza Hali ya Hatari