Korea Kaskazini leo imelipua sehemu ya barabara zisizotumika ambazo awali ziliunganisha kwenda Korea Kusini huku mataifa hayo pinzani yakitishiana siku chache baada ya Kaskazini kudai mpinzani huyo alirusha ndege zisizokuwa na rubani katika anga la mji mkuu wake, Pyongyang.

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un ameapa kukatisha uhusiano na Korea Kaskazini na kuachana na lengo la kufikia umoja wa amani wa Korea.

Katika kujibu milipuko hiyo, Wakuu wa Majeshi ya Pamoja ya Korea Kusini wamesema jeshi la nchi hiyo limefyatua risasi ndani ya sehemu za kusini mwa mpaka wakati likiimarisha utayari wake na hali ya uangalizi.

Wiki iliyopita, Korea Kaskazini ilisema ingefunga kabisa mpaka wake na Korea Kusini na kujenga miundombinu ya ulinzi kwenye maeneo ya mstari wa mbele.