- Yafanya maonesho ya makombora hatari
- Wakorea wasema wako tayari kwa mapigano
Pyongyang, Korea Kaskazini
Korea Kaskazini imeadhimisha miaka 105 ya kuzaliwa kwa mwasisi wa taifa hilo, Kim II-sung, kwa kufanya maonesho ya silaha za nyuklia.
Maonesho hayo yameelezwa kuwa ni salamu kwa Serikali ya Marekani na washirika wake walioanza kusogeza meli za kivita katika Peninsula ya Korea Kaskazini.
Taifa hilo limeitaka Marekani kuacha kufanya vitendo vya uchokozi, likisema liko tayari kujibu mapigo kwa kutumia makombora ya nyuklia.
Korea Kusini ambayo ni mshirika mkuu wa Marekani, ipo kwenye hali ya wasiwasi, ikihofu kuwa endapo vita itaanza itakuwa ya kwanza kushambuliwa kwa makombora hayo ya Korea Kaskazini.
Kufanyika kwa paredi hiyo kubwa katika Jiji la Pyongyang, kumekuja huku kukiwa na taarifa kuwa kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un, anakusudia kuamuru kufanyia majaribio baadhi ya makombora ya nyuklia.
Baadhi ya silaha zilizooneshwa, zimo mpya zenye uwezo wa kurushwa kutoka bara moja hadi jingine, hii ikiwa na maana zina uwezo wa kutua katika baadhi ya miji nchini Marekani.
Maonesho hayo ya silaha yamekuja huku kukiwa na hali ya taharuki ya kuibuka kwa vita katika ya Marekani na washirika wake dhidi ya Korea Kaskazini.
"Tumejianda kujibu mapigo," amesema Choe Ryong-hae, anayeaminika kuwa ni mmoja wa maofisa wenye nguvu na ushawishi nchini Korea Kaskazini.
Wakati wa maonesho hayo, Kim Jong-un alionekana asiye na wasiwasi na mara kadhaa alikuwa akicheka na wasaidizi wake.
"Tuko tayari kujibu mapigo ya nyuklia kwa kutumia mbinu zetu dhidi ya mashambulizi yoyote ya nyuklia,” amesema.
Maelfu kwa maelfu ya wanajeshi waliovalia nadhifu walipita mbele ya Kim Jong-un wakionesha utii na umoja. “Ungeweza kudhani ardhi ilikuwa ikitetemeka,” amesema mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Magari yaliyobeba makombora ya nyuklia ya aina mbalimbali yalipita huku yakisindikizwa na muziki kutoka Bendi ya Jeshi la Korea Kaskazini. Onesho hilo la silaha lilidumu kwa saa mbili. Ndege-vita zilitengeneza angani umbo la herufi ‘105’ kuashiria umri wa mwasisi wa taifa hilo kama angekuwa hai.
Katika maonesho hayo, kwa mara ya kwanza kulionekana kombora la ‘Pukkuksong’ ambalo lina uwezo wa kusafiri umbali wa kilometa zaidi ya 1,000.
Wataalamu wa silaha wanasema pia kulioneshwa aina mbili za makombora ya masafa marefu, lakini hawana hakika kama yalishafanyiwa majaribio.
Korea Kaskazini imeshafanya majaribio matano ya makombora yake ya nyuklia pamoja na mengine ya makombora ya kawaida kwa nyakati tofauti, hali iliyoyafanya mataifa mengi ya Ulaya na Marekani kulaani hatua hiyo.
Maonesho ya wiki iliyopita ni salamu kwa Marekani na washirika wake, yanayoashiria kiburi cha nchi hiyo licha ya shinikizo la Marekani la kutaka isitishe mpango wake wa kuwa na silaha za nyuklia.
China, kupitia kwa Waziri wake wa Mambo ya Nje, Wang Yi, imeonya kuwa machafuko yanaweza kuibuka wakati wowote, na kuongeza kuwa vita ikitokea hakutakuwapo mshindi.
Tofauti na maonesho mengine ya kijeshi, haya ya wiki iliyopita hayakuhudhuriwa na mwakilishi kutoka China.
Rais Donald Trump wa Marekani amesema; “Tishio la Korea Kaskazini lingeweza kudhibitiwa, iwapo China itaamua kusaidia (kutatua), [na] hilo ni jambo jema; kama la, tutatatua matatizo bila wao.”
Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence, alitarajiwa kuwa nchini Korea Kusini, ikiwa ni sehemu yake ya ziara ya siku 10 katika mataifa ya Asia.
Akizungumzia kupelekwa kwa makombora katika Peninsula ya Korea, Rais Trump amesema; "Tumepeleka meli-vita. Ina nguvu sana. Amefanya (Kim Jong-un) kitu kibaya. Anafanya makosa makubwa."
Hata hivyo, kuna taarifa kuwa uongozi wa Trump unajitahidi kuweka shinikizo kwa kuitumia China badala ya kutumia nguvu za kijeshi.
Siku kadhaa zilizopita, Rais Trump aliamuru kushambuliwa kwa kambi ya kijeshi nchini Syria baada ya madai kwamba kiongozi wa nchi hiyo, Bashar al Assad, aliagiza matumizi ya silaha za sumu kuua raia wasio na hatia nchini Syria.
Katika hatua nyingine, wiki iliyopita Marekani ilitumia bomu lenye uzito wa karibu tani 10 kushambulia ngome ya waasi wa Dola ya Kiislamu (IS) nchini Afghanistan. Bomu hilo lililotengenezwa mwaka 2003 limepewa jina la “Mama wa Mabomu Yote”.
Wasifu wa Korea Kaskazini:
Mji Mkuu: Pyongyang
Kiongozi: Kim Jong-un
Waziri Mkuu: Pak Pong-ju
Idadi ya watu: Milioni 24.9 (mwaka 2013)
Siasa: Itikadi ya Juche, Jamhuri, chama kimoja cha siasa
Jeshi: Ina askari zaidi ya milioni 1.2; na askari wa akiba milioni 7.7. Idadi hii inaifanya Korea Kaskazini kuwa moja ya nchi zenye idadi kubwa ya askari duniani.
Marekani: Mwaka 2013 ilikadiriwa kuwa na askari milioni 1.3; na wengine wa ziada 850,000. Idadi ya watu nchini Marekani ni milioni 325.