Serikali ya Korea Kusini imesema kuwa Korea Kaskazini imefyatua makombora ya majaribio ya masafa mafupi kuelekea baharini, huku rais mteule wa Marekani, Donald Trump, akiwa karibu kuingia madarakani.

Tukio hili limetokea wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Takeshi Iwaya, akiwa ziarani nchini Korea Kusini kwa mfululizo wa mikutano ya maafisa waandamizi.

Kaimu Rais wa Korea Kusini Choi Sang-mok, amekosoa vikali urushaji wa makombora, akisema kuwa ni kinyume na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Ameongeza kuwa Seoul itajibu kwa nguvu dhidi ya vitendo vya uchokozi kutoka Korea Kaskazini, akitaja uwezo wa usalama wa nchi hiyo na ushirikiano wake thabiti na Marekani.

Watalaamu wanakisia kuwa jaribio hili la makombora linaweza kuwa ni ujumbe kwa utawala wa Trump unaotarajiwa kuingia madarakani.