Kama tunaweza kuandika orodha ya kambi 10 muhimu kihistoria za kijeshi Afrika nzima, naweza kusema bila kusita Kongwa itakuwamo kwenye orodha hiyo.
Hata kama sisi tukilala usingizi na historia yetu, viongozi wa nchi za Afrika kamwe hawatasahau Kongwa. Na hata kama wakitaka kujifanya wamesahau, historia itawasuta na tutawakumbusha.
Hakuna viongozi wengi wakubwa wa majeshi ya nchi za Afrika ya Kusini sasa hivi ambao hawakuguswa kwa namna moja au nyingine na Kongwa.
Kongwa ina historia muhimu mno, si tu kwa Tanzania, bali kwa Afrika nzima. Hii ni moja ya sehemu ya historia inayotupa nafasi ya kujivunia kama Watanzania. Mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika ni mkubwa sana. Kambi ya kivita ya Kongwa, Dodoma, inatupa mfano mmoja wa namna Tanzania ilivyojitolea ili wengine wapate uhuru.
Mwaka 1963, Serikali ya Tanzania (Tanganyika kabla ya mwaka 1964) ilitoa sehemu ambayo ilitumiwa na serikali ya kikoloni kama shamba; kuwa kambi ya wanajeshi. Kutokana na msimamo wa serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, Rashid Kawawa, Oscar Kambona na wengine, nchi za Afrika ziliamua Tanzania iwe Makao Makuu ya Kamati ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika mwaka 1963. Kamati hiyo ilikuwa ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU).
Uamuzi huu ulionesha jinsi Tanzania ilivyokubalika kama nchi inayojali na kusaidia harakati za uhuru. Uamuzi ulifanywa na serikali ya Tanzania kufungua kambi ya wanajeshi Kongwa. Chama cha Namibia cha South West Africa People’s Organization (SWAPO), kilipeleka watu wake kwenye kambi ya Kongwa. Kuanzia mwaka 1962, Sam Nujoma alifanya makubaliano na Serikali ya Tanzania ili Wanamibia 200 waliojitolea waje Tanzania, na kutoka hapo, waende nchi nyingine kwa mafunzo ya kijeshi. Wengi wao walienda Misri kupata mafunzo hayo. Wengine walipelekwa Algeria mwaka 1963. Wengi wao walienda Kongwa walipomaliza mafunzo yao.
Wanajeshi wa kwanza kutoka Namibia kwenda Kongwa walifika Aprili 1964. Waliendelea na mazoezi na mafunzo ya kivita hapo Kongwa. Waliohitimu walianza kufundisha wengine waliopelekwa moja kwa moja kutoka Namibia. Mwaka 1965, vijana sita waliopata mafunzo ya kivita walirudi Namibia kwa siri na kuanza operesheni ya ukombozi. Miongoni mwao alikuwa Simeon Tshihungeleni na Johannes Otto Nankudhu.
Agosti 1966 kundi lingine lilipenya na kuingia Namibia. Hilo lilikuwa kundi la kwanza kufyatua risasi ndani ya Namibia Agosti 1966; wengi katika kundi hilo walikuwa Kongwa na silaha walizotumia walizipata Tanzania.
Wanajeshi kutoka Msumbiji walianza kuingia Kongwa mnamo Aprili 1964. Katika kundi la kwanza kwenda Kongwa alikuwamo Samora Machel. Machel alikuwa mmoja wa vijana waliopita Tanzania mwanzoni wa mwaka 1963 kwenda kupata mafunzo ya kijeshi Algeria. Yeye na wenzake walikuwa kati ya watu wa kwanza kuingia Kongwa na kuanza kuijenga kambi hiyo. Wanajeshi wa Mozambique Liberation Front (FRELIMO) au kwa Kireno (Frente de Libertação de Moçambique) na SWAPO waliungana pamoja na kuanza kukarabati jengo la shule na kulifanya jengo la kambi. Pia waliweka seng’enge kutenganisha kambi ya FRELIMO na SWAPO.
Ikumbukwe kwamba chama cha FRELIMO kilianzishwa Dar es Salaam mwaka 1962 baada ya Mwalimu Nyerere kuwaambia viongozi wa vikundi mbalimbali lazima waungane au waondoke Tanzania.
Ilipofika Mei 1964, wanajeshi wa SWAPO na FRELIMO wakatoka kwenye matenti na kuingia kwenye kambi mpya waliyojenga- Kongwa. Ni muhimu kukumbaka kwamba pamoja na Serikali ya Tanzania kujitolea sehemu hiyo iwe kambi ya kijeshi, wananchi wa maeneo ya Kongwa walijitolea sana kwa hali na mali kusaidia wanajeshi hao mwanzoni.
Kwa upande wa FRELIMO, kulikuwa na wanajeshi zaidi ya 250 ilipofika Septemba 1964. Kundi la kwanza lilipenya kutoka Tanzania na kuingia Msumbiji Kaskazini mwanzoni wa Septemba 1964. Risasi na bunduki walizotumia walivipata Tanzania. Huu ndio ulikuwa mwanzo wa vita ya kuikomboa Msumbiji.
FRELIMO iliondoa wanajeshi wake Kongwa na kuwapeleka kambi nyingine ya Nachingwea mwaka 1966. Nachingwea ikawa kambi kubwa na muhimu ya FRELIMO.
Chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini kilipeleka baadhi ya watu wake wa kwanza waliojitolea kujifunza kupigana Kongwa. Waliita kundi lao la kijeshi Umkhonto we Sizwe (MK), yaani Mkuki wa Taifa. Watu kutoka Afrika Kusini walianza kuingia Tanzania kwa wingi kuanzia mwaka 1962. Wengi walipitia Tanzania wakati wanaenda kupata mafunzo ya kivita.
Lakini ilikuwa mwaka 1963 ambako wengi wao walipita Tanzania na kwenda Urusi kwa mafunzo. Walianza kurudi Tanzania mwaka 1964 baada ya kufuzu. Ni muhimu kukumbusha kwamba hata hizo safari za kwenda nchi nyingine kupitia Tanzania, ziliwezeshwa kwa kupitia hati za kusafiria walizopewa na Serikali ya Tanzania. Hili lilifanywa si tu kwa Afrika Kusini, bali hata nchi nyingine za Afrika.
Baadhi ya wanajeshi wa MK wa Luthuli Detachment waliopigana Wankie Kampeni kule Zimbabwe pamoja na Zimbabwe African People’s Union (ZAPU) mwaka 1967, walikuwa Kongwa. Chris Hani alikuwa mmoja wa wanajeshi wachache waliofanikiwa kutoraka maadui katika operesheni hiyo na kukimbilia Botswana.
Vyama kutoka Angola na Zimbabwe vilipeleka wapiganaji wake Kongwa. Chama cha Popular Movement for the Liberation of Angola au kwa Kireno Movimento Popular de Libertação de Angola (MPLA) cha Angola kilipeleka wanajeshi wake Kongwa mwaka 1965.
MPLA ilitumia Kongwa kama sehemu ya kutoa mafunzo ya kivita kwa wanajeshi wake. MPLA haikuwa na wanajeshi wengi Kongwa. Pamoja na hayo, baadhi ya wapiganaji wa kwanza wa MPLA waliofungua uwanja mpya wa mapambano Angola eneo la Mashariki mwaka 1965 walikuwa Kongwa na baadaye Zambia.
Hata wanajeshi wa National Union for the Total Independence of Angola (UNITA) walikuwa 11, walikaa Kongwa na wanajeshi wa SWAPO mwaka 1965 baada ya kufuzu mafunzo yao China.
Wapiganaji wa Zimbabwe wa chama cha ZAPU ni miongoni wa wanajeshi waliofika Kongwa mwaka 1965. ZAPU haikuwa na wanajeshi wengi Kongwa; wanajeshi hao walihamishwa na kupelekwa Zambia. Baadhi ya wanajeshi hao walipigana pamoja na MK kwenye Wankie Kampeni ya mwaka 1967. Wanajeshi wa Zimbabwe African National Union (ZANU) pia walikuwapo Kongwa, na baadaye walipelekwa kwenye kambi ya Itumbi iliyopo Chunya, Mbeya.
Kongwa ni muhimu kwa sababu ilitoa nafasi kwa wanajeshi kutoka nchi tofauti za Afrika ya Kusini na Kati kupata sehemu ya kufanya mafunzo na mazoezi ya kivita. Lakini pia Kongwa ni muhimu kwa sababu ilitoa nafasi kwa wanajeshi kutoka sehemu tofauti za Afrika kubadilishana mawazo na kujuana. Hata wanajeshi waliotoka nchi moja, wengi walikuwa wanatoka makabila tofauti; Kongwa iliwapa nafasi ya kujifunza kujiunga pamoja.
Kwa mfano, watu wa makabila tofauti kutoka Namibia walijikuta wanaishi pamoja na hivyo kulazimika kujifunza kusaidiana.
Huu ni wakati mwafaka kujikumbusha mchango mkubwa uliotolewa na Tanzania kusaidia harakati za ukombozi wa Bara la Afrika. Kuna mengi tunaweza kuongeza tunapojadili mchango wa Tanzania, lakini kambi ya Kongwa ni moja ya mchango mkubwa uliotolewa na serikali na wananchi wa Tanzania. Na pia tukumbuke kuwa Kongwa haikuwa peke yake kwani baadaye kambi nyingine zilifunguliwa Mgagao, SOMAFCO, Nachingwea, Bagamoyo na Itumbi.
Mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Afrika ni mkubwa mno. Hili ni jambo moja linalotakiwa kumfanya kila Mtanzania alionee fahari. Na kwa kutoa mchango huu, tukumbuke kwamba Tanzania iliadhibiwa sana kiuchumi na kwa namna nyingine. Lakini hilo halikututingisha; tulisimama imara kama nchi na kuhakikisha zile haki za binadamu, kama uhuru, haukanyagwi.
Leo hii tunaweza kusema kwa tabasamu kubwa kwamba Kongwa ilikuwa ni mama wa majeshi tunayoyaona katika nchi za Kusini na Kati mwa Afrika!
Aluta Continua!
Mwandishi wa makala hii, Azaria Mbughuni, ni Assistant Professor wa Historia katika Chuo Kikuu cha Lane, Tennessee, Marekani. Anapatikana kupitia barua pepe: [email protected]