Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Katika kile kinachothibitisha kuwa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umefungua fursa za kiuchumi Machi 27, 2024 kampuni 180 za China na Tanzania zinatarajiwa kufanya kongamano la uwekezaji na biashara hapa nchini.
Kongamano hilo ni mwendelezo wa uhusiano mzuri wa kidiplomasia baina ya nchi hizo ambapo mwaka huu zinatimiza miaka 60 ya ushirikiano.
Hayo yamesemwa na Ofisa Uwekezaji na Msimamizi wa Dawati la China katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Diana Mwamanga leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uwepo wa kongamano hilo la kimataifa.
Mwamanga amesema katika kongamano hilo nchi ya China itakuwa na kampuni 60, huku Tanzania ikitarajiwa kuwa na kampuni 120 zinajihusisha na sekta mbalimbali.
“Machi 27, Tanzania chini ya Jemedari Rais Samia itaandika historia nyingine kwa kuandaa kongamano kubwa la wafanyabishara na wawekezaji zaidi 180 ambapo 60 wanatoka China,”amesema.
Mwamanga ametoa wito kwa kampuni za Tanzania kujitokeza kwa wingi katika kongamano hilo ambalo litakuwa na fursa nyingi za uwekezaji.
Ofisa huyo amesema kampuni hizo 60 zimelenga kuja kuangalia maeneo ya uwekezaji kwenye sekta ya afya, kilimo,, vifaa vya ujenzi madini, mazao ya kilimo na viwanda.
Mwamanga amesema kwa sasa China inashika nafasi ya kwanza kwa uwekezaji Tanzania na mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mzuri uliopo kati Tanzania.
“Tanzania ina amani, utulivu na vivutio vya uwekezaji hali inayoshawi nchi nyingine kuja kuwekeza, hivyo naomba kuchukua nafasi hii kuwaomba wawekezaji wa ndani wajitokeze ili kubadilisha mawazo Machi 27, 2024,” amesema.
Ofisa uwekezaji huyo amesema TIC imejipanga vizuri kuhakikisha wawekezaji kutoka pande zote za dunia wanakuja kuwekeza nchi, hali ambayo itawezesha lengo la kufikia uchumi mzuri linafikiwa mwaka 2025.
Kwa upande wake Meneja Maendeleo ya Wanachama Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Kelvin Ogodo amesema sekta binafsi imejipanga kikamilifu ili kuweza kunufaika na ujio huo wa wageni kutoka China.
“Sisi TCCIA, CTI, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), tumejipanga kushiriki kikamilifu kwenye kongamano hili muhimu kwenye sekta tunazosimamia,” amesema.
Ogodo amesema sekta binafsi imejipanga kushirikiana na taasisi yoyote ambayo inataka kuwekeza nchini ili kuchangia ukuaji wa uchumi.
Ofisa huyo ametoa rai kwa wafanyabiashara na wawekezaji kujitokeza kwa wingi katika kongamano hilo la aina yake.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara na Uwekezaji kutoka China, Janson Huang amesema kongamano hilo litasaidia kujenga ushirikiano na Tanzania hususani katika sekta ya viwanda, afya, ujenzi na kilimo na kwingineko.
Amesema kupitia ziara hiyo wawekezaji hao wataweza kupata taarifa na kuona fursa zilizopo moja kwa moja na sio kwa kuambiwa kama swali.
Huang amesema mwaka jana zaidi ya kampuni 100 zilishikiri kongamano kama hili ambalo litafanyika Machi 27 mwaka huu na matokeo yameanza kuwa mazuri, hadi sasa wawekezaji wawili wamekuja kuwekeza kwenye sekta ya dawa na viwanda vya nguo.
“Haya makongamano ya wawekezaji kutoka China na Tanzania yamekuwa na neema kwa nchi zetu. Uzuri wa hili la Machi 27 linafanyika katika kipindi cha nchi zetu kutimiza miaka 60 ya ushirikiano, naamini matokeo yatakuwa makubwa sana kwa siku zijazo,” amesema.