Vidonda vya tumbo na hatari zake (10)
Wiki iliyopita, Dk. Khamis Zephania alielezea dalili za vidonda vya tumbo yakiwamo maumivu na tofauti yake kulingana na rika. Sasa endelea kumfuatilia katika sehemu hii ya kumi…
Vidonda vya tumbo: Dalili za vidonda vilivyo katika mfuko wa chakula, marginal na stress, tofauti na zile za utumbo hazifuati mtindo wowote. Maumivu kutoka katika vidonda hivi yana kawaida ya kutokea mara tu baada ya kula.
Maumivu ya vidonda hivi pia yana kawaida ya kutokubali kwa ufanisi mzuri vizima asidi na baadhi ya dawa. Kula hakusaidii kuondoa maumivu ila huyaongeza.
Tofauti na vidonda vya duodeni, maumivu ya vidonda vya tumbo hayaishi mara yanapoanza.
Kipengele kingine kinacholeta tofauti ni kwamba, wakati katika vidonda vya tumbo maumivu huongezeka haraka baada ya mlo, katika vidonda vya duodeni inaweza kuchukua saa mbili hadi tatu.
Mtu anaweza kuuliza, “Kwanini kuna maumivu baada ya kula?” Hii hutokana na uchocheaji wa utemaji wa asidi ambayo hutiririka kwenye kidonda na kuchochea kipokezi cha maumivu. Katika vidonda vya duodeni, huchukua takribani saa mbili hadi tatu asidi kufika katika eneo la kidonda.
chakula: Kutosagika kwa chakula kunaweza kuwa ni dalili ya vidonda vya tumbo. Hata hivyo, kiutendaji kila mtu anaweza kuwa na tatizo la kutosagika kwa chakula tumboni mara kwa mara. Hapa tutagusia kidogo juu ya tatizo hili.
Dalili za kutosagika kwa chakula tumboni: Ni kusikia maumivu tumboni, kiungulia au maumivu yachomayo nyuma ya mfupa wa kidari, kujihisi mgonjwa au kutapika, kupiga mwayo na kutoa upepo, kuleta ladha ya uchachu mdomoni baada ya kula.
Kiungulia au kutosagika kwa asidi (acid indigestion) ni hisia za kuunguza, hutokezea nyuma ya mfupa wa kidari na mara nyingi husambaa hadi kwenye koo, taya au mdomo. Kwa sababu dalili za kiungulia hufanana na za maradhi ya moyo, hivyo kinaweza kupandisha kiwango cha mapigo ya moyo na kuleta ugonjwa wa moyo unaosababisha maumivu kifuani. Daktari lazima achunguze yote mawili kwa uangalifu.
Kama baada ya kula tutapata dalili yoyote miongoni mwa hizi tutaiita hali hiyo kuwa ni kutosagika kwa chakula tumboni (indigestion). Matabibu huita Dyspepsia lakini ni kitu kile kile. Dalili hizi hutokeza kama kuna kitu kimeleta tatizo katika koo au tumbo.
Sababu kuu za kutosagika kwa chakula tumboni: Pombe ni tatizo kubwa, uvimbe tumbo (Gastritis), uvutaji wa sigara, msongo wa mawazo, kula kupita kiasi, madawa (asprini na baadhi ya madawa yanayotolewa kwa ajili ya baridi yabisi), baadhi ya vyakula (vyakula vya mafuta, kama vile samaki wa kukaangwa, na chipsi, vinaweza kuwa ni tatizo).
Wakati mwingine matatizo ya kutosagika kwa chakula yana sababu kama vile, maradhi ya koromeo, kibofu nyongo (gall bladder); au maradhi ya ini, maambukizo ya bakteria.
Kupungua uzito: Moja ya dalili za vidonda vya tumbo ni kupungua uzito hata kama mtu anakula mlo bora. Kama una kidonda cha tumbo, hamu yako ya chakula huathiriwa, na matokeo ya hali hii ni uzito kupungua. Huku kichefuchefu na kutapika vikiwa ni dalili za vidonda vya tumbo, huongezea kupungua kwa uzito.
Kunyazi za tumbo hudhuriwa na tishu ya kovu lililojiunda ambalo huziba njia ya kuelekea tumboni. Hali hii husababisha kupoteza hamu ya kula na kupoteza uzito.
Vidonda vya tumbo husababisha uvimbe wa tishu (edema) ambao huelekea kuanzia tumboni hadi kwenye utumbo mdogo, na kuzuia chakula kutoka tumboni. Hii husababisha mtu kujisikia kimakosa kuwa tumbo wakati wote limejaa, na matokeo yake ni kukosa hamu ya kula. Mtu hukinai chakula licha ya kuwa hajala chakula cha kutosha.
Hata hivyo, kuna sababu nyingi kwanini unapungua uzito kama wewe ni mgonjwa wa vidonda vya tumbo.
Itaendelea