Misitu inavyoinufaisha Nanjilinji ‘A’ (3)

Mafanikio yaliyopatikana

Kijiji Nanjilinji ‘A’ kimedhihirisha kuwa iwapo wanavijiji watajipanga vizuri na kusimamia matumizi ya rasilimali ardhi na misitu ya asili katika vijiji, inawezekana kuboresha maisha yao. Kwa mtazamo wangu, Kijiji cha Nanjilinji ‘A’ kimekuwa mfano mzuri wa kuigwa na vijiji vingine vyenye rasilimali misitu, lakini misitu hiyo haitumiwi ipasavyo kwa faida ya wanakijiji. Kwa kipindi cha mwaka 2010/2011 kijiji kwa kushirikiana na MCDI kiliweza kupata soko la kuuza bidhaa za misitu hasa zitokanazo na mti aina ya mpingo.

Katika harakati za kupata soko, kampuni ya Sound & Fair ilijitokeza na kuahidi kununua mbao za mpingo na kuzisafirisha kwa ajili ya soko la Amerika na Ulaya. Kati ya makubaliano yaliyofikiwa moja ilikuwa ni bidhaa za miti zitakazonunuliwa zitoke katika eneo ambalo limehifadhiwa na linatunzwa ipasavyo; na kuwa mnunuzi anaweza akafuatilia na kujiridhisha kuwa ni kweli bidhaa alizonunua zinatoka sehemu yenye usimamizi madhubuti na wahusika wanafuata taratibu na sheria zilizopo (certified forest products).

 

Pia ilikubaliwa kuwa kwa utaratibu huu wanunuzi wataweza kukunua kwa bei inayoridhisha wauzaji na haitakuwa chini ya bei za mazao ya misitu zilizotangazwa na Serikali. Baada ya makubaliano hayo, kijiji kupitia Kamati ya Msitu na Walinzi wake kiliweka utaratibu mzuri wa kuvuna miti na pia kuweka kumbukumbu sahihi.

 

Vilevile, Mkutano Mkuu wa Kijiji ulipitisha azimio kwamba asilimia 50 ya mapato itumike kwa huduma za kijamii, asilimia 40 itumike kwa shughuli za kuendeleza misitu na kuhakikisha doria za mara kwa mara zinafanyika; na asilimia 10 iwe ni ushuru wa Halmashauri ya Wilaya kwa huduma wanazotoa kijijini hapo.

 

Taarifa tuliyopewa na viongozi wa kijiji wakiwamo wajumbe wa Kamati ya kusimamia msitu wakati wa ziara yetu hapo kijijini Mei 23, 2013 ilionesha kuwa Septemba 14, 2012 Kampuni ya Sound & Fair ilinunua meta za ujazo 50 kwa Sh 250,000 kila moja, hivyo kuwezesha kijiji kupata Sh 12,500,000.

 

Vilevile Oktoba 19, 2012 walinunua meta za ujazo 100 kwa Sh 200,000 na kupata Sh 20,000,000. Baada ya Sound & Fair kupasua mbao kuna magogo yaliyokuwa hayafai kwa shughuli za soko la Amerika na Ulaya. Hivyo Kamati ya Msitu iliyakusanya na Desemba 21, 2012 iliyauza kwa mteja mwingine kwa Sh 160,000 (bei iliyotangazwa na Serikali) na kupata Sh 2,240,000.

 

Januari 21, 2013 Kampuni ya Mingoyo Sawmill ilinunua magogo ya mpingo yenye meta za ujazo 49 kwa Sh 180,000 na kupata Sh 8,820,000. Vilevile kijiji kiliuza magogo ya aina nyingine za miti msenjele (Acacia nigrens), mpangapanga (Milletia Stuhlmanii), mninga (Pterocarpus angolensis) na mkongo (Afzelia quanzensis)) yenye meta za ujazo sita kwa bei ya Sh 160,000 na kupata Sh 975,600.

 

Kwa kipindi cha Septemba 2012 hadi Machi 2013 jumla kuu ya Sh 44,535,600 zilikuwa zimepatikana kutokana na mauzo ya jumla ya meta za ujazo 205 za bidhaa za misitu hasa kutokana na mpingo na baadhi ya aina nyingine chache za miti.

 

Kwa utaratibu waliojiwekea, kijiji kilipata Sh 22,267,800 (50%) kwa ajili ya kugharimia huduma za kijamii na Kamati ya Msitu ilipata Sh 17,814,240 (40%) na Halmashauri ya Kilwa kupata Sh 4,453,560 (10%).

Kwa kijiji Nanjilinji ‘A’ haya ni mafanikio mazuri waliyoyapata na yanatia moyo kuona kijiji kinaweza kujipatia mapato kutokana na rasilimali misitu waliyonayo katika eneo la kijiji.

 

Malipo kwa fedha zote zinazotokana na ununuzi wa bidhaa za misitu hufanyika kupitia akaunti ya kijiji kwenye benki na mnunuzi kuruhisiwa kuchukua alichokilipia baada ya kijiji kuhakiki kuwa fedha zimelipwa Benki. Huu ni utaratibu mzuri na kwa usalama wa mapato ya kijiji.

 

Matumizi ya fedha zilizopatikana

Matumizi ya fedha kutokana na mgawanyo wa mapato kama ulivyoainishwa hapo juu ni kama ifuatavyo:

(i) Hudua za kijamii (Sh 22,267,800): Fedha hizi zilitumiwa na Serikali ya Kijiji kuboresha huduma muhimu ikiwa ni pamoja na: (a) kukarabati visima vya maji, kununua pampu mbili za kusukuma maji na kuzifunga; (b) kujenga soko jipya (c) kuanza ujenzi shule ya msingi na choo na kuandaa mpango wa ujenzi wa nyumba ya mwalimu.

 

(ii) Usimamizi wa eneo la msitu (Sh 17,814,240): Kamati ya Usimamizi wa Msitu ilitumia fedha hizi kufanya yafuatayo: (a) kununua pikipiki mbili (Sh 4,000,000) kwa ajili ya kurahisisha doria za mara kwa mara (b) kulipa posho ya Sh 10,000 kwa siku kwa kila mlinzi wa msitu akiwa zamu kufanya ulinzi na doria (kawaida doria hufanyika mara mbili kwa mwezi na huhusisha wajumbe watano). Walinzi msitu hulipwa kiasi hicho kwa siku kutokana na kutumia muda mrefu kwa shughuli za usalama wa msitu kuliko kufanya kazi zao binafsi kujipatia riziki ya kila siku, na

 

(c) kugharimia safari za wajumbe wanapokweda nje ya kijiji (nauli na posho ya chakula au malazi inapomlazimu mjumbe kulala nje ya makazi yake) kwa shughuli za msitu kama masuala ya soko au kufuatilia malipo benki.

 

(iii) Malipo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa: Sh 4,453,560 zililipwa kwa Halmashauri ya Kilwa ikiwa ni mchango wa kijiji kutokana na mauzo ya mazao ya misitu katika Kijiji cha Nanjilinji ‘A’.

 

Pengine kijiji kama hiki kitahitaji msaada wa kiuhasibu (kitaalamu) ili wanaohusika na matumizi ya fedha waweze kuweka kumbukumbu sahihi na kuzitunza ipasavyo, kadhalika, hesabu kuweza kukaguliwa mara kwa mara kwa lengo la kuimarisha utendaji na kuhakikisha hakuna matumizi yasiyoendana na mpangokazi uliopitishwa na Serikali ya Kijiji na kukubaliwa na mkutano mkuu wa kijiji.

 

Dk. Felician Kilahama, Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki Mstaafu na Mwenyekiti wa Kamati ya Misitu Duniani-chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo-FAO, Rome, Italy.

 

Itaendelea