Vidonda vya tumbo na hatari zake (8)

Wiki iliyopita, tuliona Dk. Khamis Zephania pamoja na mambo mengine, akizungumzia milo mbalimbali ya watu na urithi wa vidonda vya tumbo. Sasa endelea kumfuatilia katika sehemu hii ya nane…

Kazi za usiku: Watu ambao hufanya kazi katika zamu za usiku wana uwezekano mkubwa wa kupata vidonda vya tumbo kuliko wanaofanya kazi za mchana. Watafiti wanahisi kuwa uvurugaji wa usingizi mara kwa mara unaweza kudhoofisha uwezo wa kinga ya mwili inayolinda dhidi ya bakteria zenye madhara.

 

Majeraha: Sababu nyingine ni hali zinazoweza kujitokeza kwa kudhuru moja kwa moja ukuta wa tumbo au ukuta wa duodeni, kama vile matibabu ya mionzi, kuungua na majeraha ya mwili.

 

Umri: Licha ya kuwa vidonda vya tumbo huweza kuwapata hata vijana wenye umri mdogo (kama ilivyo sana katika siku hizi), lakini watu wenye umri wa kuanzia miaka 50 ni rahisi zaidi kupata vidonda vya tumbo. Hii ni kwa sababu ugonjwa wa baridi yabisi umeenea sana kwa wakubwa, na kupunguza maumivu ya baridi yabisi inaweza kumaanisha kutumia dozi za aspirin au ibuprofen kila siku.

 

Kipengele kingine kinachochangia kinaweza kuwa ni kuzeeka kwa pylori (vali baina ya tumbo na duodeni) na hivyo kuruhusu nyongo iliyozidi kupenya ndani ya tumbo na kumomonyoa kunyanzi za tumbo.

 

Wanaume wana hatari zaidi ya kupata vidonda vya tumbo kuliko wanawake. Hatari ya vidonda vya duodeni huanzia miaka ya 25 na kuendelea hadi 75. Hatari ya vidonda vya tumbo huanzia miaka 55 hadi 65.

 

Tumeona kuwa vidonda vya tumbo ni mara chache kupatikana kwa watoto wadogo kuliko watu wazima, na kwamba kwa sababu wakubwa matumizi ya NSAIDs yako juu sana kwao kuliko watoto wadogo.

 

Hata hivyo, licha ya kwamba vidonda vya tumbo ni nadra kwa watoto wadogo, watoto katika umri wowote wanaweza kupata vidonda vya tumbo wanapokuwa wagonjwa sana, kama vile baada ya kuungua sana, majeraha, na ugonjwa. Vidonda hivi huitwa stress ulcers kama ambavyo tumekwisha zungumzia katika makala za awali. Vilevile, watoto ambao wazazi wao wana vidonda vya tumbo nao huweza kuvipata.

 

Kundi la damu: Pia, kwa sababu isiyoeleweleka, watu wenye aina ‘A’ ya damu wanaonekana kupata kwa urahisi vidonda vya tumbo vinavyoweza kuleta saratani. Vidonda vya duodeni vina tabia ya kutokea kwa watu wenye aina ya ‘O’ ya damu, kwa sababu hawazalishi kitu katika eneo la seli za damu ambacho kinaweza kulinda kunyanzi za duodeni.

 

Zollinger-Ellison Syndrome (ZES): Ni sababu kubwa ya mwisho ya vidonda vya tumbo. Katika hali hii, vivimbe (tumors) katika kongosho na duodeni (vinavyoitwa gastrinomas) huzalisha viwango vikubwa vya gastrin, homoni ambayo husisimua utemaji wa asidi ya tumbo. Vivimbe hivi mara nyingi ni vya saratani, hivyo uangalifu mkubwa kwa ugonjwa ni muhimu sana.

 

Ugonjwa huu ni nadra kutokea, na unapotokea mara nyingi huwapata watu wenye umri wa kuanzia miaka 45-50, na wanaume ndiyo huathirika mara kwa mara zaidi kuliko wanawake.

 

Ni vipi ZES hutambuliwa? Ugonjwa wa ZES lazima uhisiwe kwa wagonjwa wa vidonda vya tumbo ambao vidonda vyao si kwa sababu ya H.pylori na ambao hawana historia ya matumizi ya ‘NSAIDs.’ Kuharisha kunaweza kutokea kabla ya dalili za vidonda vya tumbo. Vidonda vinavyotokea katika sehemu ya pili, ya tatu au ya nne ya duodeni au jejunum (sehemu ya katikati ya utumbo mdogo) ni dalili za ZES.

 

Ugonjwa wa Gastroesophageal reflux disease (GERD) unawatokea sana wagonjwa wa ZES na mara nyingi ni mkali sana. Matatizo yanayotokana na GERD ni pamoja na vidonda na msongo wa mshipa wa umio. Katika hali nyingi, acid reflux na gastroesophageal reflux disease  huchangia kupatikana kwa vidonda. Baadhi ya tafiti zinasema kutumia antibiotics kwa ajili ya kuua H.pylori huweza kupelekea kulipuka kwa GERD.

 

Vidonda vya tumbo vinavyohusiana na ‘ZES’ mara nyingi ni vya kudumu na vina ugumu sana wa kutibika. Matibabu yanahusisha kuondoa vivimbe na kuzuia asidi. Hapo zamani, kuondoa mfuko wa chakula ndiyo ilikuwa njia pekee.

 

Sababu nyingine: Sababu zingine ni ugonjwa wa kisukari. Kisukari kinaweza kuongeza hatari yako ya kupata H. pylori. Pia mtu mwenye ugonjwa wa ini, figo na mapafu ni rahisi kupata vidonda vya tumbo. Maradhi ya ini, ugonjwa wa baridi yabisi (rheumatoid arthritis), ugonjwa wa figo na ugonjwa wa kuvimba mapafu na kupumua kwa shida (emphysema) ni miongoni mwa magonjwa ambayo yanaweza kuongeza urahisi wa kupatikana vidonda vya tumbo.

 

Dalili za vidonda vya tumbo

Si kawaida watu kuwa na vidonda vya tumbo na kusiwe na dalili. Dalili za vidonda vya tumbo hutofautiana mtu na mtu. Watu wengi hawajui kabisa kama wana vidonda vya tumbo, isipokuwa kama ghafla watajiona wakitapika damu, wengine huhisi maumivu au mchomo katika sehemu yao ya juu ya tumbo (fumbatio).

 

Baadhi ya wagonjwa hukuta kuwa wanapokula kwa hakika husaidia kuondoa tabu kwa muda. Wengine hukuta kwamba wanapokula ndiyo hufanya hali kuwa mbaya zaidi. Vinywaji vya striki, vyakula vya moto na vya kusisimua vinaweza kufanya maumivu kuwa makali zaidi.

 

Hata hivyo, ni muhimu kugusia kuwa watu wengi wenye maumivu ya tumbo si kuwa wana vidonda vya tumbo.

 

Mgonjwa wa vidonda vya tumbo anaweza kuonesha baadhi ya dalili zifuatazo: Kichefuchefu, kutapika, kuhisi mchomo ndani ya tumbo (abdomen), maumivu ndani ya kifua, kupiga mbweu mara kwa mara, kukosa hamu ya chakula, kupungua uzito, damu ndani ya kinyesi au matapishi, kutosagika chakula tumboni na kiungulia.

Itaendelea