Vidonda vya tumbo na hatari zake (7)
Kuchelewa sana kula: Kuna maelekezo mengi ya wataalamu juu ya muda mzuri wa kula. Kuchelewa sana kula huweza kuleta tatizo la kiafya ikiwa ni pamoja na vidonda vya tumbo kama mtu atakuwa tayari ana mwelekeo wa kupata vidonda. Vile vile kula wakati husikii njaa si jambo zuri kwa afya. Kula ukiwa huna njaa (au umeshiba) hudhoofisha utendaji kazi wa mifumo inayohusika na usagaji chakula.
Kupangilia muda mzuri wa kula kuna faida nyingi, moja ya faida zake ni kuupa mwili nguvu na afya nzuri. Ufuatao ni mpangilio uliopendekezwa na wataalamu wengi:
Staftahi (kifungua kinywa) – takribani saa 2 asubuhi: Unapaswa kula staftahi ndani ya dakika 30 hadi saa moja baada ya kuamka. Staftahi ni muhimu kwa ajili ya kurudishia viungo vyako sukari ndani ya damu baada ya saa 6 – 8 za usingizi. Hii italeta uwiano mzuri wa sukari na kukupa nguvu zaidi. Kula vyakula ambayo vina kabohaidreti changamano (complex carbohydrates), kama vile unga wa shayiri, njugu, nafaka zisizokobolewa, mchele wa rangi ya kahawia, matunda na mboga za majani.
Chakula cha mchana – takribani saa 6:00 mchana: Kula chakula cha mchana ndani ya saa 3 – 4 baada ya staftahi. Kama utachelewa sana muda huo, unaweza kuwa na njaa kubwa na badala yake utaanza kulidanganya tumbo kwa kula vikorokoro na vyakula vya mafuta mafuta.
Kwa ujumla, kuacha kula chakula cha mchana hukausha nguvu ya mwili wako. Muda huu ni muda wa shughuli nyingi na hivyo ni muhimu kwa ajili ya kufanya kazi katika siku yote nzima. Kula mlo wenye protini, kabohaidreti, vyakula vyenye mafuta mazuri na vyakula vya unyuzinyuzi. Virutubisho hivi muhimu vina nguvu sana na vitakupa nguvu yote unayohitaji katika kipindi cha saa nne hadi tano zijazo.
Chakula chepesi cha mchana mkubwa – takribani saa 9 za mchana: Chakula cha wakati huu hakitakiwi kiwe kikubwa kama cha mchana wa saa 6. Ni chakula chepesi cha kuondoa njaa tu. Rojorojo ya matunda, vyakula laini, mtindi wa matunda na supu ya mboga za majani ni moja ya mifano ya vyakula vya mchana mkubwa.
Matunda na mboga za majani zimesheheni vitamini na madini na vina kalori ndogo ambayo ni muhimu kwa udhibiti wa uzito. Tatizo la vyakula vyenye kalori ndogo ni kwamba vinaweza visikate njaa kwa muda mrefu. Hata hivyo, huu ni mlo mwepesi wa mchana mkubwa, hivyo kalori ndogo ni sahihi kwa wakati huu.
Chakula cha jioni – takribani saa 12 jioni: Chakula cha jioni kinapaswa kuliwa ndani ya saa 2 – 3 baada ya kile cha mchana mkubwa. Chakula cha jioni ni sawa na kile cha mchana lakini si kikubwa sana. Chakula hiki kinapaswa kuwa na protini, kabohaidreti changamano na mafuta mazuri.
Mchele wa rangi ya kahawia (brown rice), mkate, ngano, njugu na tambi, ni mifano mojawapo. Kwa nyama, samaki, kidari cha kuku ni nzuri pia. Kwa kitindamlo, kula matunda na mboga za majani kurudishia mwili wako kwa vitamini muhimu, madini na nyuzinyuzi.
Chakula cha usiku: Takriban saa 3 usiku au saa moja kabla ya kulala. Chakula hiki kinapaswa kuwa na kalori ndogo na virutubisho vingi. Kula matunda na mboga za majani na mtindi wenye mafuta kidogo. Kwa vinywaji, epuka kahawa, kunywa glasi ya maji au juisi ya matunda. Kula mlo wa uski chakula cha usiku saa moja kabla ya kulala, unakuwa hauendi kulala tumbo likiwa lina chakula.
Milo mitano midogo midogo kwa siku ni bora zaidi kuliko kula milo mikubwa 3 au 2 kwa sababu milo midogo ni rahisi kumeng’enywa na kiwango cha sukari, kitakaa sawia katika siku yote. Hii itasaidia kuzuia uchovu, kiungulia na michomo mwilini.
Urithi: Watu ambao familia zao zina historia ya vidonda vya tumbo wana kiwango kikubwa cha kupata vidonda vya tumbo. Tafiti za wataalamu zinasema, idadi kubwa ya watu wenye vidonda vya tumbo wana ndugu wa karibu wenye vidonda vya tumbo, hii ina maana urithi huchangia.
Saratani: Sababu ambayo ni nadra kutokea kwa vidonda vya tumbo, ni aina ya saratani (cancer) ambayo husababisha uzalishaji wa asidi nyingi. Dalili za vidonda vilivyosababishwa na saratani zinafanana na zile za vidonda ambavyo havijasababishwa na saratani.
Hata hivyo, vidonda vilivyosababishwa na saratani, mara nyingi havikubali matibabu ambayo hutumika kwa vidonda ambavyo havijasababishwa na saratani. Kansa ya kongosho pia huweza kusababisha vidonda vya tumbo.