Vidonda vya tumbo na hatari zake (7)
Wiki iliyopita, Dk. Ibrahim Zephania alizungumzia bakteria aina ya H. Pylori na madhara yake ndani ya tumbo la binadamu, na dawa ya vidonda vya tumbo. Sasa endelea kumfuatilia zaidi katika sehemu hii ya saba…
Sigara: Watu wanaovuta sigara/tumbaku ni rahisi kupata vidonda vya tumbo kuliko wasiovua, na vidonda vyao hupona polepole zaidi. Sigara huchoma kunyanzi za tumbo na kuzifanya ziwe rahisi kushambuliwa na asidi.
Pombe: Walevi wana hatari kubwa ya kupata vidonda vya tumbo. Pombe huchoma na kuwasha mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.
Unywaji wa pombe hata kama ni kidogo, hulifanya tumbo lako kuzalisha asidi nyingi kuliko kawaida, ambayo baadaye husababisha uvimbetumbo na muwako wa kunyanzi za tumbo (gastritis). Hali hii husababisha maumivu ya tumbo, kutapika, kuharisha; na kwa walevi wa kupindukia, hata kutoka damu.
Pombe ni kitu kibaya sana, licha ya kuwa rafiki na vidonda vya tumbo, ina madhara mengi kiafya, tuyagusie kidogo baadhi yake.
Bila shaka umeshamuona mlevi anavyotapika. Kutapika tu kwenyewe kwa mlevi ambako hakuna udhibiti kuna matatizo ya kiafya. Kama unatapika bila kujitambua, unaweza kuvuta matapishi yako katika mapafu na hivyo kujisababishia kifo.
Kutapika kwa nguvu kunaweza pia kupasua koromeo na hivyo kutapika damu. Licha ya kwamba hali hii inaweza kujirekebisha yenyewe, lakini inaweza kutishia maisha. Matatizo mengine yanayosababishwa na pombe ni kurudi kwa asidi (acid reflux), ambapo asidi hiyo huchoma koo lako.
Pombe yaweza kuleta tabu katika usagaji wa chakula, na kusharabu virutubisho muhimu. Hii ni kwa sababu pombe hupunguza kiwango cha vimeng’enya ambavyo kongosho hutoa kutusaidia kuvunjavunja mafuta na kabohaidreti tunazokula.
Pombe haishii hapo, inaweza kudhuru ini lako na kibofu cha mkojo. Katika matumizi marefu ya pombe, unaweza kuzalisha kansa ya mdomo, ulimi, koromeo, tumbo, kongosho na utumbo mpana.
Msongo wa akili: Unaweza kudhani kwamba matatizo ya kiafya ni matokeo ya virusi au bakteria tu. Kitu ambacho watu wengi hawajui ni kuwa msongo unaweza kuharibu mfumo wa kinga ya mwili (body immune system) na hivyo kukufanya uweze kuathirika kwa urahisi zaidi na vijidudu vya maradhi (germs). Udhaifu mwingi wa mwili hutokana na mfumo wako wa kingamaradhi kukosa uwezo wa kufanya kazi inavyotakiwa.
Inaaminika kwamba asilimia zaidi ya 80 ya watu wanaokwenda kuwaona madaktari, chanzo kikubwa cha maradhi yao ni msongo, ikiwa ni pamoja na pumu (asthma), maumivu ya mgongo, matatizo ya tumbo, vidonda vya tumbo, kuharisha, maumivu ya kichwa, kipandauso, shinikizo la damu la kupanda (high blood pressure), ugonjwa wa baridi yabisi, kisukari, kukaza kwa misuli na matatizo mbalimbali ya ubongo.
Msongo huathiri mfumo wa kingamaradhi na kuvuruga mfumo wa neva na akili. Msongo huongeza kiwango cha kemikali kupitia katika mtiririko wa damu ndani ya ubongo. Seli za ubongo husinyaa kutokana na msongo mwingi na kusababisha mfadhaiko.
Msongo unaweza kuleta mabadiliko makubwa katika tabia, hisia na utendaji wa mtu. Kibaya zaidi, msongo unaweza kuvuruga mifumo mbalimbali ya mwili, viungo vya mwili na tishu, ambapo unaweza kujikusanya pole pole ndani ya mwili bila ya mhusika kutambua, na mwishowe kumletea madhara makubwa ya kimwili na kiakili.
Kwa hakika, kama msongo utaachwa bila kuangaliwa, hatari yake ni kwamba utachangia kuleta matatizo mengi ya kiafya – mengi yakiwa yanayohatarisha uhai.
Msongo wa akili kwa muda mrefu husababisha vidonda kuwa vikali zaidi, na rahisi kupata vidonda vya tumbo kama tayari unaye H.pylori tumboni au vipengele vingine.
Msongo huongeza mtiririko wa asidi. Asidi hii iliyoongezeka inayotiririka ndani ya tumbo, ipo kwa ajili ya kugeuza chakula chochote kitakachokuwapo kuwa katika umbo la kumeng’enywa haraka iwezekanavyo. Lakini, kama kutakuwa hakuna chakula cha kushughulikiwa, asidi hii hulipua kunyanzi za tumbo na kuzalisha kidonda.
Katika miaka ya zamani, kabla ya kugunduliwa bakteria H.pylori kuwa ndiye msababishaji mkubwa wa vidonda vya tumbo, ilidhaniwa msongo mkali wa mawazo ndiyo uliokuwa msababishaji mkuu wa vidonda hivyo.
Itaendelea