Vidonda vya tumbo na hatari zake (6)

Katika sehemu ya tano ya makala haya yanayoelezea vidonda vya tumbo na hatari zake, Dk. Khamis Zephania, pamoja na mambo mengine alizungumzia maisha na kazi ya kiumbe kinachofahamika kama H. Pylori ambacho huishi ndani ya tumbo la binadamu. Sasa endelea kumfuatilia katika sehemu hii ya sita…

Mtindo wa maisha ikiwa ni pamoja na msongo sugu wa mawazo, unywaji wa kahawa, na uvutaji wa sigara hukufanya uwe rahisi kuathiriwa na H. Pylori kama unaye huyu kiumbe tumboni.  Si kwamba kila mwenye bakteria  H. Pylori lazima atapata vidonda vya tumbo. Hata hivyo, wataalamu bado hawajui kwa nini bakteria huyu hasababishi vidonda kwa watu wote (ambao wana H. pylori).

 

Ila, kuwapo kwa H. Pylori huzidisha mara 30 hatari ya kansa ya tumbo; na huonekana kwamba kansa ya tumbo haiwezi kutokea bila ya kutokuwapo kwake.

 

H. pylori vilevile anahusishwa na maradhi mengine ikiwa ni pamoja na maumivu ya kichwa ya kipanda uso, pia ugonjwa ambao husababisha baridi kali sana (Reynaud’s disease) na matatizo ya ngozi kama vile ugonjwa sugu wa mabaka ngozini (chronic hives).

 

Wagonjwa wa vidonda vya tumbo vilivyosababishwa na H. pylori wanahitaji matibabu ya kumng’oa kabisa bakteria huyu kutoka ndani ya tumbo kuepusha vidonda kurudi tena.

 

Baada ya matibabu, kipimo cha kutazama kama H.pylori ameondoka kinaweza kushauriwa. Kama kitafanywa, kinatakiwa kufanywa ndani ya wiki nne baada ya matibabu. Kama hatakuwa bado hajaondoka, dawa tofauti zinaweza kupendekezwa. Hata hivyo, wagonjwa wa vidonda vya duodeni, kithibitisho hiki siyo muhimu sana kwao kama dalili zote za ugonjwa zitakuwa zimeisha. Dalili zinapoisha ina maana kidonda na chanzo chake, vyote vimeondoka.

 

Dawa: Vidonda vya tumbo pia vinaweza kuzalishwa au kuzidishwa na kundi la dawa lijulikanalo kama, Non-steroidal ant-inflamatory drugs (kwa kifupi: NSAIDs). Hizi ni dawa zinazotumiwa kwa ajili ya maumivu ya kichwa, mzunguko wa hedhi na mengine madogo madogo. Mfano ni kama aspirin, ibuprofen, diclofenac n.k.

 

‘NSAIDs’ nyingi ni dawa ambazo mtu anaweza kununua bila maelekezo ya daktari. Wakati mwingine, dawa kama vile diclofenac, naproxen na meloxican zinaweza kutolewa kwa maelekezo ya daktari.

 

Matumizi marefu ya hizi dawa za kutuliza maumivu ni sababu kubwa ya pili ya vidonda vya tumbo. Dawa hizi huzuia prostagladins, vitu ambavyo husaidia kudumisha mtiririko wa damu na kulinda eneo dhidi ya jeraha. Hivyo, ‘NSAIDs’ huathiri mtiririko wa damu unaokwenda kwenye tumbo, kitendo ambacho hupunguza uwezo wa mwili wa kukarabati seli.

 

Baadhi ya watu ni rahisi kudhurika na ‘NSAIDs’ kuliko wengine. Hii ina maana kwamba, baadhi ya watu zinaweza kuwasababishia vidonda vya tumbo kwa urahisi zaidi kuliko wengine.  Non-steroidal ant-inflamatory drugs huteremsha uwezo wa tumbo kutengeneza tabaka la ulinzi (protective layer) kwa ute telezi na kuifanya kuwa rahisi zaidi kudhuriwa na asidi ya tumbo.

 

Kama ilivyo kwa bakteria H. pylori, mtindo wa maisha ikiwa ni pamoja na msongo sugu wa mawazo, unywaji wa kahawa, na uvutaji wa sigara pia huweza kukusababisha uwe rahisi kuathiriwa na ‘NSAIDs.’ Lakini vipengele hivi vyenyewe kama vyenyewe havisababishi vidonda vya tumbo.

 

Tafiti zinaonesha pia kuna muungano kati ya matumizi ya dawa ziitwazo selective serotonin re-uptake inhibitors (SSRIs) na vidonda vya tumbo.

 

Itaendelea