Katika toleo la 16 la makala haya, Dk. Khamis Zephania alieleza jinsi vidonda vya tumbo vinavyochunguzwa na matibabu yake. Sasa endelea…
Vidonda vya tumbo na hatari zake (17)
Dawa za viua vijasumu (antibiotics): Katika hatua kali ya ugonjwa, dawa za kemikali ni muhimu. Hata hivyo, mgonjwa anapaswa kupunguza matumizi ya dawa za kemikali, na ategemee zaidi matibabu asilia. Hii ni kwa sababu dawa nyingi za kemikali haziwezi kutibu kwenye chanzo cha mzizi wa tatizo, na mbaya zaidi huweza kuleta madhara mengi (side effects).
Madhara makubwa ya karibu antibiotics zote ni matatizo ya tumbo kama vile mkakamao wa misuli, kichefuchefu, kutapika na kuharisha. Matatizo ya mzio (allergy) yanaweza pia kutokana na ‘antibiotics.’ Lakini hizi ni dawa ambazo hasa hutokana na ‘penicillin’ au ‘sulfa.’ ‘Antibiotics’ huzidisha mara mbili hatari ya maambukizo ya fangasi za ukeni.
Baadhi ya dawa za vidonda vya tumbo kama zitatumiwa muda mrefu zinaweza kusababisha viashiria vya kansa ya tumbo. Dawa zinazotumika kwa ajili ya kutibu vidonda vya tumbo zinatolewa na daktari baada ya kuijua vizuri hali ya mgonjwa.
Dawa hizi ziko katika mafungu haya: Dawa ambazo hukinga (counteract) asidi inayotolewa tumboni; asidi ambazo huzuia (inhibit) utoaji wa asidi; dawa ambazo huchelewesha chakula kutoka tumboni; dawa ambazo husaidia mchakato wa uponyoji; dawa ambazo husaidia kinga ya ute telezi; dawa zinazopunguza wasiwasi na msongo. Dawa hizi hupewa mgonjwa kama anaonesha kiwango kikubwa cha msongo na wasiwasi.
Vizima asidi (antacids): Vizima asidi vingi vinapatikana bila ya kuandikiwa na daktari; na ndizo dawa za kwanza zilizoshauriwa kupunguza kiungulia na kutosagika kwa chakula (dyspepsia). Vizima asidi haviwezi kuzuia wala kuponya vidonda vya tumbo, isipokuwa vinaweza kuzuia asidi ya tumbo na kupunguza maumivu, lakini vinaweza kusababisha magonjwa mengine.
Kwa mfano, sodium bicarbonate, kiambato cha awali cha kizima asidi kina kiwango kikubwa cha sodium, ambacho hukuza ugonjwa wa figo au shinikizo la damu la kupanda (high blood pressure).
Hivyo, vizima asidi (antacids) huzimua asidi ya tumbo kwa michanganyiko mbalimbali kwa misombo (compounds) mitatu mikuu: Magnesium, calcium, au aluminium. Zinaweza kulinda tumbo kwa kuongeza bikaboneti na utemaji wa utelezi.
Inaaminika kwamba vizima asidi vya maji vinafanya kazi haraka sana na vina nguvu zaidi kuliko vidonge, ingawa baadhi ya shuhuda za kisayansi zinasema zote zinafanya kazi sawa sawa.
Madhara ya vizima asidi ni mengi, ni pamoja na kuharisha, kufunga choo, na baadhi kama zitatumiwa kwa muda mrefu hudhuru figo, nyingine zinaweza kuongeza vijiwe katika figo, na matatizo mengine mengi yanaweza kujitokeza.
Upasuaji: Zamani katika miaka ya nyuma, upasuaji ndiyo uliokuwa unatumika sana kutibu vidonda vya duodeni. Hii ilikuwa kabla ya kutambuliwa kwamba H. pylori ndiye aliyekuwa sababu ya vidonda vya duodeni, na kabla ya kuwapo dawa za kitaalamu zaidi za kupunguza asidi. Upasuaji kwa sasa huhitajika tu kama damu zitatoka nyingi na vipengele vingine vya hatari (tumekwisha kuvieleza).
Hivyo, watu ambao imekuwa ngumu kwao kutibiwa kwa dawa au ambao wamezalisha matatizo makubwa wanaweza kuhitaji kufanyiwa upasuaji, kwa wakati huu upasuaji unaofanywa ni pamoja na:
Vagotomy: Njia hii inahusisha ukataji wa sehemu za neva za vagus (neva ambayo hupitisha taarifa kutoka katika ubongo hadi kwenye tumbo). Upasuaji huu hufanywa ili kuingilia na kukata taarifa zinazotumwa, kwa hali ambayo hupunguza utemaji wa asidi.
Antrectomy: Hii ni operesheni ya kuondoa sehemu ya chini ya tumbo (antrum), ambayo huzalisha homoni inayochochea tumbo kutema maji ya usagaji chakula. Wakati mwingine, daktari anaweza pia kuondoa sehemu ya jirani ya tumbo ambayo hutema pepsini na asidi. Vagotomy mara nyingi hufanywa pamoja na antrectomy.
Pyloroplasty: Upasuaji huu unaweza kufanywa na vagotomy, ambapo vifunguaji ndani ya duodeni na utumbo mdogo (pylorus) hupanuliwa, na kuwezeshwa vilivyomo kupita kwa uhuru kutoka tumboni.
Laparoscopic: Ni njia ya mrija mwembamba mrefu uliofungwa lenzi ya kamera ambayo huruhusu daktari kupima viungo ndani ya uvungu wa fumbatio kuona dosari na kufanya oparesheni kupitia chale ndogo ndogo. Karibu watu 300,000 kote duniani hufanyiwa upasuaji kutokana na madhara yaletwayo na vidonda vya tumbo ambayo huzalisha magonjwa mengine.
Vyakula: Kipengele kikubwa katika matibabu ni kula mlo sahihi na tabia nzuri katika namna ya kula vyakula. Ni muhimu sana kula mlo wenye nyuzinyuzi. Ni muhimu pia kula mlo wenye mafuta kidogo.
Upungufu wa Vitamin K pia umehusiana na kupatikana kwa vidonda vya tumbo. Vitamin K huzuia kutoka damu, huweka mazingira mazuri ya kupona. Miili yetu hutengeneza vitamini hii ya kutosha, lakini watu ambao hawana vitamini hii huelekea kupata vidonda. Vitamin K hupatikana katika nyanya, jibini (chizi), viini vya yai, ini na katika mboga nyingi za majani zenye rangi ya kijani.
Tafiti zinaonesha kwamba Vitamin C, Vitamin E na Vitamin B6 ziko chini sana kwa watu wenye vidonda vya tumbo. Vitamin A ni muhimu sana kwa uponyaji wa ute telezi. Zinki kwa upande wake huongeza kasi ya uponyaji wa vidonda vya tumbo.
Pia ule mlo kidogo kidogo. Unapokula mlo kidogo kidogo unaepusha kuzalisha asidi nyingi ya mmeng’enyo wa chakula, lakini kula mara kwa mara kuzuia asidi hii kushambulia kunyanzi za tumbo.
Juisi ya kabichi ina msaada katika kutibu vidonda vya tumbo. Andaa juisi ya kabichi (kabeji) na tumia robo kikombe kila siku. Kunywa mara tu baada ya kuiandaa.
Epuka maziwa. Ingawa maziwa hutuliza tumbo na huzimua asidi ya tumbo, lakini pia husisimua uzalishaji wa asidi zaidi, ambayo baadaye itachoma eneo la kidonda.