Kwa muda wa wiki mbili sasa sijaandika katika safu hii. Nimepata simu nyingi, na ujumbe mfupi, wengi wa wasomaji wangu wakidhani kuna maswahibu yamenisibu. Nawahakikishia niko salama bin salimin na buheri wa afya.
Sikuweza kuandika katika kipindi cha wiki mbili zilizopita kwa sababu kuu mbili. Ya kwanza tulikuwa katika mafunzo endelevu mjini Dodoma yaliyolenga kutuandaa kubadili mwelekeo wa kampuni yetu (transformation) baada ya kupata ruzuku kutoka kwa Wakufunzi wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF).
Sitanii, mimi kama mtendaji mkuu wa Kampuni ya Jamhuri Media Limited, naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru kwa dhati TMF kwa kutupatia hii ruzuku ya mabadiliko ambayo imetolewa kwa vyombo sita kwa ujumla wake vitapatiwa Sh bilioni 2.
Vyombo vilivyonufaika na ruzuku hii kutoka TMF ni Gazeti la JAMHURI na Mwanahalisi, huku upande wa redio zilizopata zikiwa ni Standard FM ya Singida, CG FM ya Tabora, Ebony FM ya Iringa na Kili FM ya Kilimanjaro.
Ruzuku hii itatumika kufanya habari za uchunguzi.
Kwa upande wetu sisi kama JAMHURI, mradi mkubwa na wa kipekee tunaoufanya chini ya mradi huu unahusiana na sekta ya uzinduaji (extractive Industry); kwa maana ya madini, gesi na mafuta.
Tutagusa pia suala la elimu, na hatutasahau suala la utalii. Mpaka mradi huu unaisha tunalenga sheria ziwe zimebadilishwa, Watanzania wana uelewa mpana juu ya aina ya mikataba tunayopaswa kuwa nayo na Serikali isimame kidete kudai haki ya taifa hili kwa niaba ya Watanzania.
Sitanii, leo nimeandika mada hii kugusia maeneo makubwa mawili tu, nayo ni kodi ya majengo na elimu kwa mabinti wanaopata mimba wakiwa shuleni. Kwa muda mrefu nimekuwa nikipinga kodi ya majengo kutozwa kwa kila mtu bila kujali iwapo nyumba yake inaingiza pato au la.
Nimeandika makala kadhaa kupinga utaratibu huu na hasa nikitumia mfano wa kodi ya kichwa iliyofutwa mwaka 2005. Nimesema na narudia, hupaswi kulipa kodi kwa fedha ambayo hukupata. Au hupaswi uende kwa jirani kukopa fedha za kulipa kodi.
Dhana kwamba kama usingekuwa na nyumba binafsi ungekuwa unalipa kodi ya pango haikubaliki. Ina maana nchi yetu inafurahia kuona watu wake wanakuwa wapangaji milele?
Nashukuru hili sasa limepungua. Kwanza Serikali kidogo imenifurahisha.
Sitanii, imenifurahisha Serikali kwa kutangaza bayana kuwa vijijini hakuna mtu anayepaswa kulipia kodi ya majengo. Pia naamini kodi hii inapaswa kutozwa kwa mtu ambaye nyumba yake inafanya biashara kwa maana kuwa inaingiza pato.
Wapo watu waliishaanza kuwabana watu wa vijijini kutoa hadi Sh 50,000 kama kodi ya majengo. Nashukuru Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango ametangaza kuwa vijijini hawahusiki na kodi hii. Hii imeondoa kero. Wananchi vijijini ilikuwa wamewekwa kikaangoni.
Sitanii, ukiacha hili la kodi ya majengo, kuna suala alilotamka Mhe. Rais John Pombe Magufuli kuhusiana na watoto wanaopata mimba wakiwa shuleni. Niseme nakubaliana na Rais Magufuli katika kulinda maadili ya taifa letu. Si jambo jema watoto kupata mimba wakarejesa shuleni.
Inawezekana tamaduni za Wazungu zina ustaarabu tusioufahamu, kwamba watoto wao wanaweza kujilinda. Hapa kwetu tukiruhusu kiholela, tutajikuta nusu ya shule wanafunzi watoto wananyonyesha watoto. Nasema si kwa kiwango hicho. Kwetu hii haijakubalika vyema.
Hata hivyo, kwa unyenyekevu mkubwa naomba kuwasilisha ninalowaza. Si wasichana wote wanaopata ujauzito wanakuwa wameamua kwa hiyari yao kupata mimba. Wapo wanaobakwa. Mhe. Rais, hawa waliopata mimba kwa kubakwa nashauri tuwape nafasi maalum.
Wakati aliyembaka anafungwa miaka 30 jela, si vyema sana kumwadhibu binti huyu aliyebakwa. Tuangalie uwezekano wa kumpatia haki ya kurejea shule kutimiza ndoto zake zinazotaka kukatizwa na majahili. Siamini kama kwa kushauri hivyo nimekuhudhi Mhe. Rais. Nilishuhudia siku ya makinikia Rais uliomba ushauri kabla ya kumshughulikia Prof. Sospeter Muhongo, hivyo katika hili naomba kukushauri pia.
Nahitimisha makala hii, kwa kurejea mambo maatatu ya msingi niliyoandika leo. Kwamba nawashukuru TMF kwa kutupatia ufadhili wa ruzuku ya mabadiliko (transformation grant), pili nimefurahi kodi ya majengo kuwaondoa watu wa vijijini, ila tuangalie hata nyumba zisizo za biashara zisilipishwe na mwisho mabinti wanaobakwa, wapewe fursa ya kurejea shule. Mungu ibariki Tanzania.