*Miaka 20 tangu akose penalti fainali dhidi ya Cameroon
Dakar, Senegal
Aliou Cissé anasimama na kutazama pande zote za Stade du 26 Mars, moja ya viwanja vya soka vya Bamako nchini Mali, kisha anakimbia na kupiga penalti muhimu ya tano kwa taifa lake. Anakosa na kuwaacha Cameroon wakichukua ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2002.
Mechi hiyo ya fainali ilikuwa ndiyo fursa ya kwanza kwa Senegal kubeba ubingwa huo, lakini nahodha wao, Cisse, akawaangusha. Hii ilitokea baada ya dakika 120 kumalizika bila kufungana.
Tayari El Hadji Diof alishakosa penalti na alichotakiwa Cisse ni kufunga ili ubao usomeke 3-3; kazi iendelee.
Imemchukua Cisse miaka 20 kurekebisha makosa aliyoyafanya na hatimaye kuwapa Wasenegali kile walichokuwa wakikitamani; ubingwa wa Afrika.
Akiwa na miaka 45, Cissé anakuwa kocha wa pili kijana kushinda tuzo hiyo nyuma ya Herve Renard wa Zambia aliyeshinda mwaka 2012.
Pia yupo juu kwa makocha wa Kiafrika katika mashindano haya ambayo makocha wanaletwa Afrika kutoka Ulaya na Amerika Kusini.
Machozi ya furaha yamemtoka Cissé baada ya ushindi wa Senegal dhidi ya Misri wiki moja iliyopita, huku akilazimika kushuhudia tena mikwaju ya penalti ikipigwa.
Kwa kawaida kocha huyu huonekana mtulivu, asiye na papara na ni vigumu kwa waandishi wa habari kufahamu ni nini kilichomo kichwani mwake.
Kocha asiye na mzaha
Fainali za mwaka huu ni za tano kwa Cissé; mbili kama mchezaji, 2000 na 2002 na tatu mfululizo akiwa kocha.
Hii ni kudhihirisha sababu za FA ya Senegal kumng’ang’ania mtu aliyekuwa akipambana na lawama na ukosoaji mkubwa, mara nyingi kutoka kwa wachezaji wenzake wa zamani; na sasa ameleta mafanikio.
Wote wawili; Khalilou Fadiga, aliyekuwapo Cameroon katika jopo la ufundi la CAF na El Hadji Diouf – ambaye Cisse alimpa nafasi ya kuwa mmoja wa washauri wa wachezaji – walionekana wakishangilia kwa pamoja baada ya mechi ya fainali, ambao awali walikuwa wakosoaji wakubwa wa Cisse.
“Hii timu inao uwezo wa kushinda Kombe la Mataifa ya Afrika, lakini hilo haliwezekani iwapo Aliou Cissé atabaki kuwa kocha wa timu,” amewahi kusema Diouf miaka mitatu iliyopita.
Kwamba Cissé mwenyewe aliweza kuona mbele zaidi ya wengine ni ushuhuda wa jinsi alivyo.
Ukosoaji huo haukumhamasisha Cissé pekee bali pia wachezaji.
“Ninadhani huyu jamaa anastahili mafanikio anayoyapata kwa kuwa sijawahi kuona kocha anayekosolewa kama yeye maishani mwangu, lakini kamwe hakati tamaa,” anasema Sadio Mane baada ya ushindi wa Senegal wa 3-1 dhidi ya Burkina Faso kwenye nusu fainali.
“Tunachotaka ni kushinda kwa ajili ya taifa letu na kwa ajili yake, kwa kuwa anastahili kwa yote aliyoyapitia akiwa mchezaji na sasa kocha,” anasema Mane.
Si kwamba wachezaji humpenda Cissé muda wote. Wamewahi kumpachika jina la utani la ‘Jammeh’, Rais wa zamani wa taifa jirani la Gambia, Yahya Jammeh, kutokana na ukali wake.
Cissé hana masihara katika masuala ya nidhamu, akisisitiza katika kufanya kazi kwa bidii, kutunza muda na kuwa makini mazoezini. Utani ni kitu kimojawapo asichokipenda kabisa.
‘Mtambo’ uliokulia vitongoji vya Paris
Cissé alizaliwa Ziguinchor lakini akahamia Ufaransa akiwa na umri wa miaka tisa, alikokulia hatua chache kutoka nyumbani kwa Djamel Belmadi, kocha aliyewahi kushinda taji la Mataifa ya Afrika akiwa na Algeria, kusini mwa Paris.
Anasema: “Nikiwa mtoto nilikuwa nikienda Parc des Princes (moja ya viwanja vya soka maarufu Ufaransa) kuwaona akina Safet Susic, Valdo… na wachezaji wakubwa kibao. Ndoto yangu ilikuwa kuchezea Paris St-Germain. Kila mtoto alitamani hivyo lakini sikupata fursa hiyo.”
Badala yake Cissé akaibukia kwenye ‘akademi’ ya Lille na baadaye kuanza soka la ushindani akiwa na Sedan.
Hatimaye akajiunga na PSG mwaka 1998. “Huko nikacheza na wachezaji wakubwa kama Jay-Jay Okocha na Ronaldinho. Nikipata nafasi ya kujifunza mengi kwa kuwa nilikuwa kijana aliyepata nafasi ya kucheza mechi kadhaa na klabu kubwa,” anasema.
Kocha wa zamani wa Senegal, Bruno Metsu, akamwita timu ya taifa na kuwa nahodha wa kikosi kilichoishitua dunia kwa kuwafunga mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia, Ufaransa, kwenye mechi ya ufunguzi mwaka 2002.
Kikosi hicho kilikwenda hadi robo fainali ya fainali zilizochezwa Japan na Korea Kusini, ikiwa timu ya pili ya Afrika kufika hatua hiyo.
Akahamia Birmingham City na baadaye Portsmouth na mara tu alipohamia England akapatwa na majanga makubwa ya kufiwa na ndugu zake 12 kwenye ajali ya kivuko iliyotokea pwani ya Afrika Magharibi.
Cissé alirejea Sedan mwaka 2006 alikomaliza soka akichezea Nimes kwenye mashindano ya Ligue 2. Hakuwahi kuwa nyota ila akafahamika tu kama ‘mtambo wa kazi’.
Achukua mikoba ya Simba wa Teranga
Baada ya mafunzo ya ukocha, Cissé akajiunga na FA ya Senegal kama kocha msaidizi wa timu ya Olimpiki chini ya Karim Sega Diouf, kwa ajili ya michezo iliyofanyika London mwaka 2012.
Kisha akafanya kazi chini ya Alain Giresse wakiwa na timu ya taifa, na Machi 2015 akachukua mikoba ya timu hiyo baada ya kutolewa nje katika raundi ya kwanza ya michuano ya Equatorial Guinea, wakati Senegal wakipewa nafasi kubwa ya kusonga mbele.
Tangu hapo Cissé hajarudi nyuma tena, akashinda mechi ya kirafiki ya kwanza kama kocha mkuu dhidi ya Ghana na sasa ni mkongwe akiwa ameiongoza timu ya taifa katika mechi 71.
Senegal wamefuzu mara tatu mfululizo kwenye fainali za Mataifa ya Afrika pamoja na fainali zilizopita za Kombe la Dunia kule Russia.
Rekodi yake akiwa na Simba wa Teranga ni ushindi katika michezo 46, sare 16 huku akifungwa mara tisa tu.
Akiwa amepoteza katika mechi ya fainali dhidi ya Algeria mwaka 2019 kisha kunyakua ubingwa huo wiki iliyopita kwa kuwafunga Misri, Cissé anakisifu kikosi chake kwa uimara na kumaliza subira ya taifa ya muda mrefu.
“Huu ni ushindi kwa watu wote wa Senegal, kwa kuwa tangu Uhuru tumekuwa tukipambana kupata ushindi huu. Leo na sisi tutawekewa nyota kwenye jezi zetu,” anasema.
Pamoja na yote, ushindi huu sasa unapaswa kuelekezwa kwenye mechi ya kusaka tiketi ya Kombe la Dunia dhidi ya Misri mwezi ujao.