Mshambuliaji wa Chelsea Eden Hazard anaweza kufunga mabao 40 msimu huu na kujishindia tuzo ya mfungaji mabao bora Ligi ya Premia, kwa mujibu wa meneja wa klabu hiyo Maurizio Sarri.

Kwa mujibu wa BBC, Hazard alifunga mabao matatu dhidi ya Cardiff Jumamosi na kuwawezesha The Blues kupata ushindi wa 4-1.

Kufikia sasa amefunga mabao matano katika mechi tano zilizochezwa, moja kushinda mchezaji anayemfuata.

Baada ya mechi hiyo ya Jumamosi, Sarri alisema Mbelgiji huyo huenda akawa ndiye mchezaji bora zaidi Ulaya.

Alisema zamani alikuwa anaamini alikuwa miongoni mwa wachezaji bora zaidi Ulaya lakini kwa sasa anaamini huenda ndiye bora zaidi.

“Tumezungumza naye na kumwambia anaweza kufunga mabao 40,” alisema Sarri.

“Kuna baadhi ya mambo anayoweza kuboresha, lakini anaweza.”

Miongoni mwa anayotaka Hazard aboreshe, ni kutumia nguvu zake nyingi katika maeneo ya wapinzani uwanjani badala ya eneo la timu yake.

Kimsingi anamtaka ashambulie zaidi.

Hazard alijiunga na Chelsea mwaka 2012 na amewafungia jumla ya mabao 94 lakini hajawahi kufunga mabao 20 akichezea klabu mechi za ushindani msimu mmoja.

Mabao ya juu zaidi aliyofunga ilikuwa ni msimu wa 2014-15 alipofunga mabao 19, na misimu miwili iliyopita alifunga amabo 17 kila msimu.

Mshambuliaji wa Liverpool Mohamed Salah alishinda tuzo ya mfungaji mabao bora msimu uliopita baada ya kufunga mabao 32 Ligi ya Premia, na jumla ya mabao 44 mashindano yote.