Mvutano mkali umeibuka baina ya Chama Kikuu cha Ushirika Kilimanjaro (KNCU) na Chama cha Ushirika wa Mazao (AMCOS) cha Lyamungo kuhusu umiliki wa shamba la kahawa la Lyamungo kutokana na kila upande kudai ni mmiliki halali.

Shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 112 lililopo Lyamungo, Wilaya ya Hai limekuwa katika mgogoro usiokwisha kwa muda wa miaka 16 hadi sasa, hivyo kudhoofisha shughuli za uzalishaji katika shamba hilo.

Mwenyekiti wa Lyamungo AMCOS, Gabriel Ulomi, amesema katika taarifa yake kuwa shamba hilo lilinunuliwa kutoka kwa raia wa Ugiriki, Philip Filios, mwaka 1965 na kilichokuwa chama cha ushirika kilichoitwa New Machame Lyamungo Cooperative Society.

Amesema chama hicho ambacho kwa sasa ndicho kinaitwa Lyamungo AMCOS, kilipewa stakabadhi ya malipo namba 1150 kutoka Kampuni ya udalali ya Mrs Z. Ramzan baada ya shamba hilo kununuliwa kwa njia ya mnada.

“Mwaka 2003 wanachama na wananchi wa Lyamungo walipigwa butwaa walipoona gazetini kuwa shamba lao litauzwa kwa njia ya mnada chini ya kampuni ya udalali kutokana na deni la Sh milioni 500 lililokopwa na KNCU kutoka Benki ya KCBL”, amesema Ulomi.

Katika taarifa yake kwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya, mwenyekiti huyo amesema baada ya kuona hivyo wanachama na wananchi walifanikiwa kuzuia uuzwaji wa shamba hilo baada ya kulizunguka shamba lote na baadaye kuweka zuio mahakamani.

Alimweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa licha ya jitihada za kuzuia uuzwaji wa shamba hilo, KNCU walitekeleza azima yao ya kuliuza kwa kutumia picha za video kuonyesha shamba hilo kwa kampuni ya uwakala wa mbegu, ‘zoezi’ ambalo lilifanyika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.

Inaelezwa kuwa KNCU walikuwa wadhamini na walezi wa New Machame Lyamungo Cooperative Society baada ya chama hicho kuchukua mkopo kutoka taasisi ya National Credit Agency, hivyo kubaki na hati ya shamba hilo wakiamini imo katika mikono salama.

Mwenyekiti huyo amesema baada ya kufuatilia walibaini kuwa KNCU walibadilisha hati ya shamba hilo kabla ya kuitumia kukopa fedha Benki ya Ushirika ya KCBL bila wao kushirikishwa juu ya ubadilishwaji wa hati hiyo.

Hata hivyo licha ya KNCU kukopa fedha hizo, ilishindwa kurejesha mkopo huo na chama hicho cha Lyamungo kilipeleka kilio serikalini kuomba deni hilo libebwe na serikali, kilio ambacho kilisikika na serikali kujitwisha mzigo wa deni hilo.

Ametaja madhara ya mgogoro huo kuwa ni pamoja na chama hicho kushindwa kuendeleza shamba hilo, ikiwamo kufanya uwekezaji nje ya zao la kahawa uliokuwa uhuhusishe upanuzi wa kiwanda cha kutengeneza matofali.

Msimamo wa KNCU

Wakati Lyamungo AMCOS wakidai shamba hilo ni mali yao halali, KNCU nayo kwa upande wake wanasisitiza shamba hilo ni mali yao halali na kupuuza madai ya chama hicho kwamba walibadili jina la hati ya shamba hilo na kwenda kukopea fedha benki.

Kaimu Meneja wa KNCU, Kakozi Ibrahim, amezungumza na JAMHURI  na kusisitiza kuwa kwa mujibu wa nyaraka ambazo wanazo, shamba hilo ni mali yao.

Amesema wakati akikabidhiwa ofisi hiyo kukaimu nafasi hiyo, miongoni mwa nyaraka alizokabidhiwa ni hati ya shamba la Lyamungo na kwamba chama hicho ni miongoni mwa wanachama 92 wanaounda KNCU, hivyo mgogoro huo ni kati ya ushirika na ushirika.

“Lyamungo ni sehemu ya KNCU, na unapoitaja KNCU na Lyamungo wamo, na ukumbuke kuwa KNCU inayo mashamba katika kila wilaya, sasa tukiruhusu kila mwanaushirika avamie shamba lililo karibu yake na kudai ni mali yake hatutafika,” amesema.

Hata hivyo meneja huyo amedai kuwa suala la shamba la Lyamungo lilikwisha kufika hadi Mahakama Kuu na iliamuliwa chama hicho kifuate sheria ya ushirika kukata rufaa kwa waziri mwenye dhamana na ushirika.

Mwaka 2005 aliyekuwa Waziri wa Ushirika wakati huo, Sir George Kahama, katika barua yake ya Oktoba 21, 2005 alikazia uamuzi wa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika wakati huo kwamba shamba hilo ni mali ya KNCU.

Mwaka 2007 aliyekuwa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk. A. K. Kashuliza, alikiandikia barua chama hicho cha Lyamungo na kukipa siku 21 kuondoa zuio lake mahakamani lakini hadi sasa chama hicho hakijafanya hivyo.

Katika barua yake ya Agosti 23, mwaka 2007 yenye Kumb. Na. FA. 64/207/04/79 kwenda kwa mwenyekiti wa bodi ya uongozi ya chama hicho, mrajisi huyo alionyesha kusikitishwa na hatua ya chama hicho kukataa kutekeleza maagizo hayo ya serikali.

“Hii ina maana kwamba kati yenu kuna kundi la watu ambao wanapinga amri halali ya serikali na wangependa kuendeleza migogoro inayokwamisha juhudi za maendeleo ya wananchi wa Kilimanjaro,” inasema barua hiyo.

Pamoja na mrajisi huyo kutishia kuchukua hatua kama uongozi wa chama hicho usingetoa zuio hilo mahakamani, ni mwaka wa 12 sasa tangu agizo hilo litolewe chama hicho kimeshindwa kuondoa zuio hilo.