Na Zulfa Mfinanga, Jamhuri Media,
Arusha

Wadau wa wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) ambayo imeanza leo jijini Arusha wamesema licha ya kuihamasisha jamii kupokea teknolojia mpya ya akili bandia lakini watahakikisha haiendi kinyume na maadili ya Mtanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari, leo Oktoba 23, 2023 jijini hapa Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society Francis Kiwanga amesema licha ya teknolojia hiyo kuja na fursa lakini pia ina athari zake hivyo wao kama wadau wa maendeleo wanaitaka jamii kuondoa hofu kwani watakikisha mila na tamaduni za nchi zinalindwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society Francis Kiwanga.

“Wengi tumeipokea kwa hofu hii akili bandia, lakini niseme kuwa katika mijadala yetu pia tutajadili athari zake, hivyo tutachagua teknolojia inayotufaa ambayo tutaenda nayo kwani kazi za AZAKI ni kuhakikisha wananchi wanaelewa umuhimu wa teknolojia, wanaitumia katika kuwaletea maendeleo na pia kukemea athari zake” amesema Kiwanga.

Kiwanga amesema katika wiki ya AZAKI mambo mbalimbali yatajadiliwa yakiwemo kutumia teknolojia katika kutatua changamoto ya maji nchini, mabadiliko ya tabia ya nchi ni jinsi gani teknolojia ikitumika inaweza kusaidia kilimo kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Mada nyingine ni ujumuishwaji na uwezashaji kidigitali, matumizi ya takwimu katika kuleta manufaa katika jamii, teknolojia na utetezi katika jamii, elimu na mafunzo ya kidigitali nchini Tanzania, teknolojia kwa maendeleo endelevu pamoja na kuimarisha usalama mtandaoni.

Akizungumzia faida za teknolojia mpya ya akili bandia, mwakilishi wa shirika la Apple Inc la nchini Marekani ambaye ni Mtanzania, Aboubakar Ally amesema mabadiliko ya kiteknolojia duniani hayaepukiki hivyo kuitaka jamii kuwa tayari kupokea mabadiliko hayo.

Mwakilishi wa Shirika la Apple Inc. la nchini Marekani ambaye ni raia wa Tanzania Aboubakar Ally.

Amesema mifumo ya komputa imeanza kubadilika na sasa inafanya kazi kwa hisia huku akiwatoa hofu watanzania juu ya kupotea kwa ajira kwani teknolojia inakuja na fursa……”niwatoe hofu juu ya teknolojia hii mpya, kikubwa ni watu kuwa na uthubutu, utayari, kutenga muda wa kutosha na kutumia akili ili kuhakikisha teknolojia haiwaachi nyuma” amesema Ally.