Baada ya kusimama kwa zaidi ya miezi miwili sasa, kindumbwendumbwe cha Ligi Kuu Tanzania Bara, kinarejea tena Jumamosi wiki hii, huku timu za Yanga na Simba zilizokuwa mazoezini nje ya nchi, zikimulikwa zaidi.

Yanga iliyorejea nchini wiki iliyopita, ilipiga kambi ya katika mji wa kitalii wa Antalya, Uturuki, kwa siku 14, huku Simba ikijichimbia nchini Oman.

 

Hata hivyo, kupiga kambi nje ya nchi pekee hakutoshi kuwezesha mahasimu hao wakuu wa soka nchini kufanya maajabu katika mzunguko wa pili wa ligi hiyo ikiwa hazikufanya maandalizi mazuri.

 

Yanga inarejea dimbani ikiwa inaongoza katika mzunguko wa kwanza ikiwa na pointi 29, ikifuatiwa na Azam FC (pointi 24) na mabingwa watetezi wa ubingwa wa ligi hiyo, Simba yenye pointi 23.

 

Zinafuatiwa na Mtibwa na Coastal Union zenye pointi 22 kila moja, Kagera Sugar (21), Ruvu Shooting Stars (20), JKT Mgambo (17), JKT Ruvu (15), JKT Oljoro na Tanzania Prisons (14) kila moja, Toto African (12), African Lyon (9) na Polisi Morogoro inaburuza mkia ikiwa na pointi nne.

 

Simba ndiyo timu pekee inayorejea katika ligi hiyo ikiwa inanolewa na kocha mpya Mfaransa Patrick Liewig, aliyechukua nafasi hiyo kutoka kwa Mserbia Milovan Cirkociv aliyetimuliwa.