na Mwandishi Wetu JanhuriMedia, Dar es Salaam
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema maboresho mapya ya Kitita cha Mafao kwa wanachama wake utekelezaji utaanza rasmi Machi 1,2024.
Hayo yamebainishwa leo Februari 28,2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw.Bernad Konga wakati akizungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Amesema, Kitita cha Mafao ni orodha ya huduma za matibabu ambazo zinatolewa kwa wanufaika wa NHIF na bei zake nchini.
Konga amefafanua kuwa,maboresho ya mwisho ya Kitita cha Mafao kinachotumika sasa yalifanyika Juni, 2016.
“Ni takribani miaka nane sasa,hivyo kuwepo umuhimu wa kufanya marejeo yake kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa wanachama na kuongeza huduma ambazo hazikuwepo.”
Amesema, miongoni mwa manufaa ya kitita ni pamoja na wanachama wanaotumia dawa za shinikizo la damu na sukari sasa wanaweza kupata dawa ngazi za chini.
Pia, Konga amefafanua kuwa,wanachama wanaopata huduma ya uchujaji damu gharama imeshushwa chini.
“Na huduma za kibingwa na bingwa bobezi kama matibabu ya moyo, saratani, figo zitapatikana kwenye ngazi za kanda pia na sio lazima mwanachama aende mpaka hospitali za ngazi taifa,”amesema Konga.
Vilevile amebainisha kuwa, dawa mpya zaidi 247 zimeongezwa kwenye kitita, hivyo changamoto ya kukosa dawa kituoni imeondolewa.
Ameongeza kuwa, maboresho hayo yamekuja na nafuu kwa mwananchi katika gharama za ushauri, dawa na matibabu.
Konga amesema gharama za maboresho hayo hazimgusi mwanachama bali ni kati ya NHIF na watoa huduma ili kuboresha zaidi huduma karibu na wananchi nchini.
Mkurugenzi Mkuu huyo amesema,maeneo muhimu yaliyofanyiwa maboresho ili kuleta unafuu huo wa gharama ni ada ya usajili na ushauri wa daktari huduma za dawa na tiba za upasuaji na vipimo.
Konga ameongeza kuwa, mfuko huo unaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau kuhusu kitita hicho na pale maboresho yatakapofanyika wataendelea kutoa taarifa.