Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na mgombea wa nafasi ya uenyekiti ndani ya chama hicho, Tundu Lissu, wakati wa mchakato wa kampeni zake amebainisha kuwapo kwa watumishi wa Mungu kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), waliowakutanisha kwa siri yeye na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.
Kwa waliofuatilia mnyukano wa kugombea nafasi ya uenyekiti ndani ya CHADEMA watajua kuwa ubinafsi na uchafu mwingi wa chama umewekwa bayana, viongozi wake wakuu wamevuana nguo na kuyaweka hadharani yale waliyoyafanya sirini kwa muda mrefu.
Inashtusha kwa sababu hili si jambo la kawaida katika siasa za nchi yetu, lakini inaogopesha kwa sababu ni vigumu kujua masilahi ya makundi haya mawili katika mustakabali wa taifa.
Katikati ya upatanisho wa siri, yupo Padri Dk. Charles Kitima, Katibu wa TEC. Anayetaka kumfahamu vema Dk. Kitima anapaswa kutafuta kipindi kilichorushwa mwaka 2013 na Star TV cha Tuongee Asubuhi.
Ilikuwa baada ya mlipuko wa kinachodaiwa kuwa bomu kwenye mkutano wa CHADEMA uliofanyika viwanja vya Olasiti jijini Arusha. Watu kadhaa walipoteza maisha.
Kwenye kipindi hicho, Dk. Kitima akiwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) mkoani Mwanza, alidai kuwa wahusika wa jambo hilo ni waumini wa imani tofauti na yake, wenye msimamo mkali.
Wakati huo hata Jeshi la Polisi lilikuwa halijafanya uchunguzi wa kina wa tukio hilo, lakini Padri Kitima hakuona shida kuwataja waumini wa dini nyingine kama wahusika ingawa alisema: “Si wote.”
Mimi ni mmoja wa watu wanaoheshimu kazi za taasisi za dini katika kujenga jamii ya watu waungwana, wenye maadili na inayosaidia jamii.
TEC na taasisi nyingine zilizo chini ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na wengine kama wa Ismailia ni wadau muhimu katika maendeleo ya jamii ya Watanzania.
Ninatamani sana kuziona taasisi hizi zikiendelea na mchango wao ambao kwa kiasi kikubwa bado unahitajika katika taifa letu. Hata hivyo hili la maaskofu kukutana kanisani na viongozi wa CHADEMA si jambo la kuachwa lipite hivi hivi.
Kuna mambo kadhaa ya msingi ya kuyatazama. Jarida la Standard Christian la mwaka 2022, mwandishi Ben Cachiaras, ameandika kuhusu aina mbili za viongozi wa dini waliopo sasa.
Kundi la kwanza ni la viongozi ambao Ukristo wao unatangulia mapenzi yao kwa vyama vya siasa, halafu kuna wale ambao mapenzi yao kwa vyama huzidi Ukristo wao.
Hatari ambayo Cachiaras aliiona takriban miaka miwili iliyopita inatoka zaidi kwa viongozi wa dini – soma maaskofu, mapadri, masheikh, wachungaji ambao kwanza ni mashabiki wa vyama kuliko majukumu yao ya kidini.
Hawa ni viongozi ambao kila jambo la kijamii wanalitazama kwanza kwa mrengo wa kisiasa na si kwa namna ambavyo dini yao – au Yesu Kristo kwenye Ukristo, angekuwa ameshauri.
Maneno haya ya Cachiaras yanaakisi pia ujumbe uliotolewa na Baba Mtakatifu, Papa Francis, mwezi uliopita, akiwa katika Kisiwa cha Corsica, ambapo aliwataka makuhani wa Kikatoliki kujihadhari na vikundi vya kiroho vinavyosababisha mgawanyiko wa kisiasa.
Kwa Papa Francis, kazi kubwa ya viongozi wa Kanisa na Kanisa kwa ujumla, ni kuleta amani na maelewano katika jamii na si kuchochea migawanyiko, kuegemea upande mmoja katika mgogoro na kutoa kauli au maandishi ambayo hubomoa zaidi kuliko kujenga.
Hata kama Padri Kitima anahubiri kuhusu upendo kwa Watanzania au mapenzi yake kwa nchi, ukweli ni kwamba ni mtu anayeonekana kama vile haamini kwamba watu wa imani tofauti na yake wanatakiwa kuongoza taifa letu.
Ndiyo sababu amewaalika Mbowe na Lissu kwenye ‘mimbari’ kuzungumza nao ili waelewane. Wawe kitu kimoja.
Huenda Padri Kitima ana ndoto yake ya Tanzania aitakayo. Wakati John Tendwa alipostaafu kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa na nafasi yake kuchukuliwa na Francis Mutungi, Padri Kitima aliiambia BBC akisema: “Watanzania wanatakiwa kuondokana na mfumo wa kijima wa kung’ang’ania chama kimoja.”
Ingawa yeye ni kasisi wa kanisa na kwenye ibada na mazungumzo yake huzungumza kama mtu asiye na upendeleo, ninaamini kuwa ndani kabisa ya moyo wake anaamini kuwa CCM kuendelea kubaki madarakani ni ujima.
Kwa nini naamini hivi? Kwa sababu katika mnyukano kati ya Mbowe na Lissu, hakuna hata kiashiria kinachoonyesha kuwa kuna mmoja anayeweza kuliumiza Kanisa kwa msimamo wake.
Kama msimamo wake ni kwamba CHADEMA inatakiwa iwe imara na kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani, basi maana yake ni kwamba yeye na baadhi ya maaskofu wanachotaka ni madaraka.
Kwamba wanaona masilahi yao yatabebwa zaidi endapo CHADEMA itaingia madarakani kuliko chama kingine chochote, achilia mbali CCM.
Na kwa sababu yeye hakuwahi kumwita Ibrahim Lipumba wakati akigombana na Maalim Seif, au James Mbatia dhidi ya kina Joseph Selasini pale NCCR Mageuzi, ina maana TEC ina masilahi na CHADEMA.
Ni masilahi au biashara gani ambayo TEC imeahidiwa na CHADEMA? Kwenye upatanishi unaoendelea, TEC inataka nini kwa chama hicho endapo kitaingia madarakani?
Idadi ya Watanzania wenye imani mbili tofauti haitofautiani sana. Kama TEC imeamua kuwa na CHADEMA, Waislamu na Wakristo wasiokuwa Wakatoliki na watu wasiofuata imani za dini za kigeni, wamewekwa kwenye kundi gani kwenye makubaliano hayo?
Vyama vya siasa, kama ilivyo kwa binadamu, vinazaliwa na vinakufa kwa sababu tofauti. Je, maaskofu walioshiriki kwenye upatanishi wa Lissu na Mbowe wanahofia nini endapo mwisho wa CHADEMA hii tuijuayo utakuwa umefika?
Kanisa linakuwa imara zaidi pale ambapo linajikita katika majukumu yake linayoyajua zaidi – kueneza dini na kusaidia jamii, lakini huwa na rekodi mbaya linapoingia kwenye siasa za ushindani.
Siasa ni eneo ambalo wanasiasa wamelifanyia kazi kwa miaka mingi na wanajua namna ya kuogelea. Kwa vyovyote vile, maelezo ya Lissu yanashtua kwa sababu yanaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya Watanzania watakuwa raia wa daraja la pili kwenye ‘dili’ ambalo CHADEMA na TEC wameingia.
Na taarifa hii imefungua boksi jipya kuhusu nini hasa lilikuwa lengo la matamshi ya Kanisa katika kipindi cha miezi 18 iliyopita.
Kwenye suala zima la ujio wa Kampuni ya DP World, TEC, hususan Padri Kitima, ilikuwa mstari wa mbele kwenye ukosoaji, wakifanya kazi kwa karibu na viongozi wa CHADEMA.
Je, sasa tujue kwamba suala lile pengine hoja haikuwa ya kisiasa bali ya kimasilahi; kwamba kampuni iliyotakiwa na TEC/CHADEMA kupata zabuni ilishindwa? Kwamba tatizo halikuwa mkataba bali nani alipewa zabuni ile?
Na kama sasa tumejua kwamba CHADEMA na TEC ni ndugu, tutakuja kuwaamini vipi maaskofu watakapokuja na ukosoaji wa jambo ambalo pia linakosolewa na CHADEMA?
Je, CHADEMA ndiyo mdomo wa TEC au TEC ndiyo mdomo wa CHADEMA? Na kama hivi ndivyo ilivyo, sisi wengine ambao si wana CHADEMA wala Wakristo Wakatoliki, mustakabali wetu kama Watanzania ukoje mbele ya macho yao?
Angalizo:
Haya ni maoni ya mwandishi wa makala hii, si msimamo wa Gazeti la JAMHURI. – Mhariri
Mwisho