Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Serikali imewahakikishia wawekezaji kuwa Tanzania ni sehemu salama hivyo waje kuwekeza.

Wito huo umetolewa leo Oktoba 12, 2024 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula wakati akifungua Mkutano wa jukwaa la uwekezaji katika sekta ya Utalii Nchini Tanzania lililofanyika katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es salaam,ikiwa ni sehemu ya Onesho la 8 la Utalii la Kimataifa la Kiswahili( S!TE 2024).

Amesema kuwa, kupitia mkutano huo wamekutana na wawekezaji pamoja na wanaojihusisha na sekta ya utalii ili kuwaelezea fursa zilizopo nchini, hivyo kuwakaribisha waje kushirikiana na Tanzania kwenye sekta hiyo.

“Kupitia mkutano huu tumekuja kuwahakikishia wawekezaji kwamba Tanzania ni eneo salama ambalo wanaweza kuwekeza wakawa na uhakika wa kufanya biashara na kupata faida.

“Kama mnavyofahamu Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kufungua sekta ya Utalii, kutangaza vivutio vya utalii vya nchi yetu na Sasa tumepata watalii wengi sana wanakuja kutembelea nchi yetu. Sasa mbali na kuja kutembelea lakini kuna uwekezaji unahitajika ufanyike katika Nchi yetu, uwekezaji ambao utaboresha miundombinu ya sekta ya Utalii, kuwezesha kuwepo hoteli za kutosha katika sekta ya Utalii,” amesema Kitandula.

“Kama mnavyofahamu ukuaji wa sekta hii ulivyo sasa, karibu asilimia 25 ya mapato ya kigeni yanatokana na sekta hii lakini bado fursa ni kubwa ya kuvutia watu waje kuwekeza ili sekta hii iweze kunufaisha nchi yetu kiuchumi.

“Ni sekta ambayo tukiitumia vizuri inaweza kutusaidia kutoa ajira, kwahiyo tunawaita wawekezaji waje kuwekeza kwenye mahoteli ili kufungua fursa za ajira,” amesema Kitandula.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru amesema Mkakati wa Wizara ya Maliasili na Utalii ni kuzalisha mazao ya Utalii, Kujenga Mazingira bora ya kutangaza utalii na kuainisha fursa mbalimbali za uwekezaji.

“Ndani ya S!TE kuna wale ambao wamekuja kuangalia fursa za uwekezaji pamoja na mazao ya utalii yaliyopo katika sekta hii. Mazao ni mengi, kama ambavyo mnajua utalii sio tu wa wanyamapori kuna Utalii wa fukwe, mikutano, michezo na kadhalika.

“Kwahiyo tumejipanga kama Bodi ya Utalii, wageni hawa waliokuja kuwapeleka katika maeneo mbalimbali kusini mwa Tanzania, Magharibi mwa Tanzania, Pwani ya Mashariki, na Zanzibar wakashuhudie mazao mbalimbali ya Utalii na fursa za uwekezaji,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Masoko kutoka Hoteli ya Dar es Salaam Serena, Seraphin Lusala amesema bado kuna haja ya Serikali kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya hotel nchini kwani kukua kwa utalii na kuongezeka kwa watalii wengi kunahitaji pia kuwepo kwa hoteli nyingi nchini zenye hadhi ya kimataifa.

“Katika kujaribu kuleta wawekezaji wengi zaidi katika sekta ya mahoteli inabidi kuwapa uelewa zaidi mambo ya hoteli na faida zake. Kuna wawekezaji wengi hawajui faida ambazo zinatolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), wakizijua itawapa moyo zaidi kuwekeza kwenye hoteli.

“Mji kama Dar es Salaam, tukipata ukumbi mkubwa wa mikutano wa watu kama 3000 au 4000 wakati mwingine kunakuwa hakuna vyumba vya watu kulala. Hivyo Serikali ingeongeza uelewa wa watu wenye uwezo wa kuwekeza kwenye mahoteli kwani ni sehemu ambayo inahitaji uwekezaji mkubwa,” amesema

Please follow and like us:
Pin Share