Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inajipanga kuingiza taarifa za daftari la kudumu la wapiga kura kwenye mfumo wa Kitambulisho cha Taifa ili ifikapo mwaka 2025 kitambulisho hicho kitumike kupigia kura.
Mpango huo umebainishwa na Mkurugenzi wa Habari na Elimu ya Mpiga Kura wa NEC, Giveness Aswile, wakati alipozungumza na Gazeti la JAMHURI kuhusu tathmini ya zoezi la kuboresha daftari hilo katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani lililokamilika hivi karibuni.
Ameeleza kuwa mpango huo ni mwitikio wa wito wa serikali wa kupunguza idadi ya vitambulisho kwa mwananchi.
Baadhi ya vitambulisho ambavyo hutolewa kwa Mtanzania hivi sasa ni kadi ya mpiga kura, Kitambulisho cha Taifa, kadi ya bima ya afya, leseni ya udereva na hati ya kusafiria ya kielektroniki.
Ili kuondoa utitiri wa kadi hizo, wataalamu wa teknolojia wanaeleza kuwa taarifa za kadi hizo zote zinaweza kuingizwa kwenye kadi moja na zikatumika bila taarifa zake kuingiliana kimifumo.
Aswile anasema kwa sasa zoezi hilo haliwezi kufanikiwa kwa sababu Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) bado haijakamilisha utoaji wa vitambulisho vya taifa kwa wananchi.
“Tume haiwezi kupeleka taarifa zake ziingizwe kwenye mfumo wa NIDA kwa wakati huu, huko kwa wenzetu bado zoezi la kutoa vitambulisho limekuwa gumu. Huu mpango ni mzuri, wananchi wawe wavumilivu, kuwa na kitambulisho kimoja ndiyo nia ya serikali, tunachotakiwa kufanya kwa sasa ni kuwapa ushirikiano wa kutosha NIDA, wao wakifanikiwa na sisi tutafanikisha bila shaka,” anaeleza.
Aidha, anasema tume imevuka malengo katika uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura.
Anasema awali tume ilikuwa na malengo ya kuboresha daftari hilo kwa asilimia 17 lakini mpaka sasa tathmini inaonyesha imefanikisha zoezi hilo kwa zaidi ya asilimia 27.
Anaongeza kuwa katika maeneo ambako uboreshaji wa daftari umefanyika kumekuwa na mwitikio mkubwa wa watu kuhakiki taarifa zao huku kukiwa na idadi kubwa ya vijana wanaojiandikisha kwa mara ya kwanza katika daftari hilo.
Mkoa wa Dar es Salaam uliwekwa mwishoni kwenye uboreshaji wa daftari hilo ili kurahisisha zoezi la tathmini nzima ya zoezi hilo kwa ujumla na kubaini changamoto mbalimbali zinazotakiwa kufanyiwa kazi kabla ya Uchaguzi Mkuu.
Hata hivyo, anaeleza kuwa katika baadhi ya maeneo wamebaini watu kukosa elimu ya mpiga kura.
“Kuna watu hawakujitokeza kuhakiki taarifa zao kwa hoja kwamba walijiandikisha mwezi Novemba mwaka jana. Tukiwaelimisha kuwa mwaka jana ulikuwa ni uchaguzi mwingine ambao ni tofauti na huu tunaoandaa, wanatuelewa na zoezi linaendelea,” anasema.
Uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ulihusisha kuandikisha wapiga kura wapya ambao wamefikisha umri wa miaka 18 au watafikisha umri huo siku ya kupiga kura na kuondoa majina ya waliokosa sifa, ikiwamo waliofariki dunia na kuhamisha taarifa za watu waliohama.