Na Richard Mtambi, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Maadhimisho ya Tatu ya Siku ya Kiswahili Duniani 2024, yalifanyika Julai 3, 2024 nchini Tanzania, Afrika Mashariki, Afrika na duniani kote lugha ya Kiswahili inakozungumzwa.
Lengo la Maadhimisho haya ni kuitikia wito wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) la kuitangaza Julai 7, ya kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani. Uamuzi huo ulitangazwa Novemba 2021, katika Mkutano wa 41 wa Nchi Wanachama wa Shirika hilo uliofanyika Jijini Paris, Ufaransa, ambapo Maadhimisho ya kwanza yalifanyika Julai 7, 2022 na ya pili Julai 7, 2023.
Aidha, katika maadhimisho ya mwaka huu, Kiswahili kimepiga hatua zaidi baada ya Julai 7 ya kila mwaka kutambuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa Siku ya Kiswahili Kimataifa hapo Julai 1, 2024. Uamuzi huo uliokuwa unasubiriwa kwa hamu na wadau wa lugha ya Kiswahili ulifanywa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa nchini Marekani.
Nchini Tanzania Maadhimisho hayo yalianza rasmi Juni 29, 2024 Jijini Arusha kwa Mbio za Masafa za Kiswahili zilizoandaliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kwa kushirikiana na Kampuni ya African Sports Agency (ASA). Mbio hizo za Masafa za Kiswahili zilikuwa na malengo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuleta ari na mwamko kwa Tanzania, Afrika na Duniani kote ili kuyapa hadhi Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani.
Aidha, Mbio hizo zililenga kuchochea na kuendeleza juhudi za kutangaza utalii wa Tanzania ambazo zilianzishwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia filamu aliyoianzisha ya Royal Tour. Fauka ya hayo, Mbio hizo pia zimewasaidia washiriki kuimarisha afya ya akili na mwili, ikizingatiwa kuwa katika zama hizi watu wengi wanakabiliwa na magonjwa mbalimbali yasiyo ya kuambukiza kutokana na tabiabwete.
Vilevile, Julai 3, 2024, kulikuwa na Mjadala wa Kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mjadala huo uliandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kupitia Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), BAKITA na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA).
Malengo maalumu ya kuwapo kwa mjadala huo yalikuwa ni kuonesha kukua na kuenea kwa lugha ya Kiswahili ambapo kulikuwa na kushirikishana taarifa zinazohusiana na ufundishaji na maendeleo ya lugha ya Kiswahili kwa ujumla katika nchi za Ufaransa, Urusi, Italia, Misri, Austria, Ghana, Burundi, Zimbabwe na Uganda.
Akifungua Mjadala huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, alisema kuwa Wizara ya Mambo ya Nje itaendelea kutafuta fursa za Kiswahili za nje ya nchi na kuwawezesha wataalamu wa Kiswahili wa hapa nchini kupata fursa hizo.
Aidha, aliwataka wale wote wenye ujuzi mbalimbali wa taaluma ya lugha ya Kiswahili kujisajili katika kanzidata ya BAKITA na BAKIZA ili iwe rahisi kuwatumia pale Serikali kupitia Wizara yake inapopata mahitaji ya wataalamu kutoka nchi za nje.
Shughuli nyingine zilizofanyika kuelekea siku ya kilele, tarehe 7 Julai, 2024 zilikuwa ni pamoja na Programu ya Kalam Salaam, ambayo ilihusisha mapitio ya kazi za fasihi, tarehe 4 Julai, 2024. Tukio hilo liliandaliwa na BAKITA kwa kushirikiana na Kituo cha Sanaa na Utamaduni cha Alliance Francaise. Julai 5, 2024 kulikuwa na matembezi ya wanafunzi ambayo yalipokewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Albert Chalamila. Pamoja na matembezi hayo kulikuwa na utoaji wa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika mashindano ya uandishi wa insha nchini.
Fauka ya hayo, Julai 6, 2024, BAKITA kwa kushirikiana na wadau wengine wa Kiswahili liliandaa Mjadala wa Wazi wa Mwanamke Hazina, ambao ulikuwa na lengo la kuonesha namna mwanamke alivyopitia katika hatua mbalimbali za maisha kutoka kutwezwa utu wake hadi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uongozi, siasa, uchumi, ujasiriamali, sanaa, michezo, ulinzi na usalama na shughuli nyingine za kijamii.
Mgeni rasmi katika tukio hilo alikuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Tabia Maulid Mwita ambaye katika hotuba yake alisema kuwa, Serikali zote mbili zinaunga mkono jitihada za kumkwamua mwanamke kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii na kuwa zitakuwa mstari wa mbele katika kuandaa na kutekeleza mikakati muhimu itakayofanikisha wanawake kupata mafanikio zaidi duniani kote. Katika siku zote hizo za matukio ya Maadhimisho haya kulikuwa na maonesho na mauzo ya machapisho na bidhaa za Kiswahili na utamaduni wa Mtanzania kwa ujumla.
Maadhimisho ya mwaka huu yamehusisha majadiliano kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya lugha ya Kiswahili kama vile uzoefu wa nchi za nje katika ufundishaji wa Kiswahili, fursa zinazotokana na lugha ya Kiswahili, changamoto za kukiendeleza zaidi Kiswahili na utatuzi wa changamoto hizo. Aidha, washiriki wameweka mikakati ya kukieneza zaidi Kiswahili ikiwa ni pamoja na ubidhaishaji wa lugha hiyo. Shughuli za kabla ya kilele, zimewashirikisha wanazuoni na wataalamu mbalimbali wa lugha ya Kiswahili, wawakilishi wa mabalozi, wageni kutoka nje ya nchi, wanasiasa, waandishi, wachapishaji, wasanii, vijana wa makundi mbalimbali na wanafunzi wa ngazi zote za elimu nchini.
Akitoa ujumbe katika Maadhimisho hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wa dunia kukitumia Kiswahili katika kukuza utangamano na amani miongoni mwao. Amesema kuwa Kiswahili kina nafasi kubwa katika kuwaleta watu pamoja na kufundisha maadili, “Natoa rai kwa viongozi wenzangu kote ulimwenguni kukitumia Kiswahili katika kukuza utangamano, kujenga na kulinda amani na mshikamano, Kiswahili ni fursa ya kufanikisha malengo ya maendeleo ya nchi zetu, bara letu la Afrika na dunia kwa ujumla,” alisema Rais Samia.
Aidha, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro ametoa wito wa matumizi ya lugha ya Kiswahili katika maeneo mengine muhimu, ikiwa ni pamoja na katika matumizi ya akili mnemba. Dkt. “Tanzania na dunia kwa ujumla tunatakiwa kufanya ubunifu wa teknolojia za akili mnemba na mitandao ya kijamii inayotumia lugha ya Kiswahili, wakati lugha hiyo ikiwa inaenea kwa kasi kubwa”.
Vilevile, anawaagiza BAKITA na BAKIZA kuhakikisha kuwa machapisho yote ya Kiswahili yanachapishwa hapa nchini na kuwa mabaraza yatafsiri machapisho yote muhimu ya Kiingereza, vikiwemo vitabu na mashairi kwa Kiswahili ili watu waweze kuyasoma na kuyaelewa.
Waziri Ndumbaro anasema kuwa lugha ya Kiswahili ifungamanishwe na mitandao ya kijamii, teknolojia na vijana kwa vile msamiati mwingi hutoka kwenye kundi la vijana. “Tunataka Kiswahili kiwe lugha rasmi ya Saba ya Umoja wa Mataifa, kwa sasa kuna lugha sita ambapo katika lugha zote hizo hakuna yenye asili ya Afrika, hivyo, Waafrika ambao ni kundi kubwa la watu hawana uwakilishi katika lugha,” anasema Dkt. Ndumbaro.
Anaongeza kuwa Maadhimisho hayo pia yanafanywa katika Balozi za Tanzania katika nchi za Marekani, Italia, Ufaransa, Komoro, Malawi, Misri na Afrika Kusini, wakati Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki inafanya Maadhimisho hayo Jijini Mombasa, Kenya ambapo Wizara imewakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wake Dkt. Suleiman Serera.
Akizungumza siku ya kilele cha Maadhimisho hayo, Katibu Mtendaji wa BAKITA, Consolata Mushi aasema kuwa, kila kundi lililoshiriki Maadhimisho hayo limepata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo yake kuhusu maendeleo ya lugha ya Kiswahili na kubainisha kuwa BAKITA na BAKIZA chini ya usimamizi wa wizara mbili zenye dhamana ya utamaduni watayashughulikia kikamilifu maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa ili lugha ya Kiswahili ipige hatua zaidi na kuwaletea watu mapato ikiwa ni pamoja na kuchangia katika pato la taifa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Gerson Msigwa alisema kuwa kupitia Mkakati wa Taifa wa Kubidhaisha Kiswahili, Tanzania itapeleka walimu wa Kiswahili duniani kote kutokana na watu kuhitaji kujifunza lugha ya Kiswahili. Alisema kuwa, Tanzania imepanga kuandaa machapisho mbalimbali zikiwemo kamusi kwani machapisho hayo yatahitajika kwa kiasi kikubwa duniani kote katika vituo 100 vitakavyoanzishwa duniani vya ujifunzaji wa lugha ya Kiswahili, “Nitoe rai kwa vijana walioko vyuoni na shuleni msikibeze Kiswahili kwani ni lugha yenye fursa nyingi, hivyo, bobeeni huko kwani kuna mahitaji makubwa,” alisema Msigwa.
Kaulimbiu ya Maadhimisho hayo ni “Kiswahili na Fursa za Maendeleo Duniani,” ikiwa na lengo la kuona kuwa wataalamu mbalimbali wa lugha ya Kiswahili wanapata fursa za Kiswahili zilizoko duniani kote. Miongoni mwa fursa hizo ni ukalimani, tafsiri, kufundisha Kiswahili kwa wageni na kufundisha Kiswahili katika shule za msingi, sekondari na vyuoni. Aidha, fursa nyingine ni kupitia shughuli za sanaa, uandishi wa vitabu na pia uandishi na utangazaji wa habari.
Maadhimisho ya Tatu ya Siku ya Kiswahili Duniani yamefana sana kutokana na shughuli mbalimbali kuhusu maendeleo ya lugha ya Kiswahili zilizofanyika kwa wiki nzima na kuhudhuriwa na washiriki kutoka ndani na nje ya nchi wakiwamo wawakilishi kutoka UNESCO na washiriki kutoka katika nchi za Ufaransa, Urusi, Italia, Misri, Austria, Ghana, Burundi, Zimbabwe na Uganda.
Tujivunie na Kukienzi Kiswahili, Moja ya Tunu za Taifa Letu
Mwandishi wa Makala haya ni Mhariri Mkuu wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA)
Simu: 0713 616 421
Baruapepe : [email protected]