Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
SERIKALI imesema magonjwa ya kisukari na shinikizo la juu la damu ni kati ya magonjwa 10 yanayowasumbua zaidi Watanzania.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema hayo mwishoni mwa wiki baada ya kufanya mazoezi yakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
“Shinikizo la Juu la Damu (High Blood Pressure) pamoja na kisukari ni kati ya magonjwa 10 yanayowasumbua Watanzania, wajibu wetu wizara ni kuhakikisha tunawakinga wananchi wasipate magonjwa, ndio maana tumeiomba serikali kuu kupitia kwa Waziri Mkuu kufungwa kwa barabara hii ili kupisha mazoezi,” alisema Ummy.
Aliongeza: “Mwaka 2022 kati ya magonjwa 10 yaliyowasumbua Watanzania moja lililojitokeza ni shinikizo la juu la damu, bajeti ya mwaka 2022/2023 likaongezeka na kisukari katika magonjwa 10 yanayowasumbua Watanza
nia…”
Ummy alisema mazoezi yanasaidia kukinga magonjwa hususani kisukari na shinikizo la juu la damu kwa zaidi ya asilimia 50 hivyo wananchi wafanye mazoezi.
“Wizara ya afya itaendelea kuweka nguvu katika kuwakinga wananchi na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kuwahimiza kufanya mazoezi na kuzingatia mtindo bora wa maisha,” alisema. Ummy alisema Wizara ya Afya itaviunga mkono vikundi vyote vya mazoezi vya Mkoa wa Dar es Salaam.
Majaliwa alisema mazoezi hayo yanayoratibiwa na Wizara ya Afya ni moja ya afua iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Mnakumbuka programu hii iliyoanzishwa na Rais wetu Samia Suluhu Hassan na yeye mwenyewe kushiriki na kuwahamasisha Watanzania kushiriki mazoezi, katika kipindi cha miaka mitatu ya Dk Samia moja ya mambo ya kujivunia ni mafanikio kwenye sekta ya michezo,” alisema.