Na Wilson Malima Lusaka Zambia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwasili nchini Zambia kwa ziara ya kikazi ya siku tatu na kupokelewa na mwenyeji wake Rais Hakainde Hichilema katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Keneth Kaunda jijini Lusaka.
Ikiwa ni mwaliko wa Rais wa Taifa hilo kuwa mgeni rasmi katika sherehe za kuazimisha miaka 59 ya uhuru wa Zambia, Rais Samia aliungana na mwenyeji wake kuweka mashada ya maua katika mnara wa Mashujaa uliopo jijini Lusaka pia katika kaburi la baba wa taifa hilo Hayati Keneth Kaunda kama ishara ya kuwaenzi waliojitoa kupambania uhuru.
Rais Samia na ujumbe wake aliungana na maelfu ya Wazambia pamoja na wageni wengine mashuhuli wakiwemo mabalozi, katika viwanja vya Ikulu ya taifa hilo kusherehekea, kutafakari pamoja na kutathimini miaka 59 ya uhuru wa taifa la Zambia na mchango wake katika kushiriki kuyakomboa mataifa mengine ya Afrika. Siku hiyo huazimishwa Oktoba 24, kila mwaka tangu Zambia ijipatie uhuru kutoka kwa Uingereza 1964.
Kupitia sherehe hizo, wakati wa hotuba yake Rais Samia alipata wasaa wa kugongelea misumali katika uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Zambia, kwa kuzingatia kwamba Kijografia Tanzania ni lango la Zambia pamoja na mataifa mengine ya ukanda kusini mwa Afrika kupitia bandari yake.
Mbali na kuongeza nguzo nyingine katika ushirikiano baina ya mataifa haya mawili, ikiwa ni kuwahakikishia mazingira mazuri kibiashara ikiwemo usafirishaji huru wa bidhaa na watu kupitia mipaka yake, Rais Samia aliwazawadia pia Wazambia eneo la bandari kavu hekta 20 lililopo Kwala mkoani Pwani kwa ajili ya kuhifadhia mizigo inayotpita katika bandari ya Dar es Salaam.
“Kwa nia ya kuwa na watu katikati ya mipango yetu na kulingana na azma yetu ya kurahisisha zaidi biashara kati ya nchi zetu mbili, Serikali yangu imefanya uamuzi wa kutenga eneo la ardhi hekta 20 katika Bandari Kavu ya Kwala mkoani Pwani kwa ajili ya mizigo inayopelekwa Zambia.” Amesema Rais Samia na kuongeza kuwa;
“Zambia itawezeshwa kuhifadhi mizigo yake kwa muda mrefu zaidi bila malipo ambao usiopungua siku 45. Hatua hii itapunguza msongamano na ucheleweshaji, na hivyo kupunguza gharama za kufanya biashara nchini Zambia. Kwa maana hiyo, tunatazamia kwamba hatua hii itakuza zaidi biashara kati ya nchi zetu mbili na kuunda fursa zaidi za kibiashara kwa Watu wetu.”
Rais Samia alieleza bayana maboresho makubwa kwenye mitambo yaliyopo na yanayoendelea kufanyika katika bandari ya Dar es Salaam na kuwataka wafanyabiashara wa Zambia kuchangamkia fursa hiyo adhimu.
Si hivyo tu, Rais Samia aliitumia vizuri heshima aliyopewa na Hichilema, baada ya hafla ya sherehe za uhuru aliwaongoza wafanyabishara na wawekezaji aliombatana nao katika ziara hiyo kukutana na wenzao wa Zambia katika dhifa ya jioni, kujadili fursa mbalimbali na maeneo ya kimkakati mbayo pande zote mbili zinaweza kunufaika ili kuinua uchumi kupitia uwekezaji na ushirikiano kibiashara.
Mbele ya mawaziiri kadhaa na wafanyabiashara wa pande zote mbili, kwa pamoja Rais Samia na mwenyeji wake Rais Hichilema walihimiza hatua madhubuti kuchukuliwa mara moja dhidi ya mipango mikakati pamoja na maazimio ya pamoja yaliyofikiwa na si kuishia kwenye maneno tu ili kuweza kufikia maendeleo ya malengo waliyojiwekea.
Rais Samia alisisitiza kuwa ushirikiano ulioasisiwa na watangulizi wao wa mataifa hayo mawili ulijiikita zaidi katika kupambania uhuru wa kisisa na sasa kwa pamoja wanauendeleza kupitia miradi mbalimbali ya kimaendeleo na ushirikiano kibishara ili kupata uhuru kamili kiuchumi na kimaendeleo.
Awali Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji aliwahimiza wafanyabiashara kuwa wabunifu zaidi na kuacha biashara ya kimazoea ikiwa ni pamoja na kuruhusu matumizi ya Tehama katika ufanyaji biashara ili kuokoa ghrama za uendeshaji na kujipatia faida nzuri.
“Kama tunavyojua ulimwengu Unabadilika haraka sana ikiwa ni pamoja na jinsi tunavyofanya biashara, duniani kote biashara sasa hazifanywi tena kwa mikono ila ni kwa njia za kielektroniki na mfumo huo unakua kwa kasi kutokana na maendeleo ya Tehama hivyo tunatakiwa kuhakikisha kuwa hatuachwi nyuma”Amesema Dkt. Kijaji
Siyo tu katika kuokoa gharama na kupata faida, Dkt. KIjaji pia alliwaeleza wafanyabiashara kugeukia bishara mtandao ili kusaidia kupunguza changamoto zinazojitokeza ikiwa ni pamoja na kuokoa muda baina ya wafanyabiashara wa pande zote mbili.
“Tunatakiwa kubadilisha njia za kufanya biashara ili kupunguza gharama za miamala kwa taasisi zetu za kibiashara na kuharakisha usafirishaji wa bidhaa na huduma kati ya nchi zetu pia, nahimiza wafanyabiashara wote kuanza kufikiria kimkakati kuhusu Biashara ya Mtandaoni na kuichukulia kwa uzito wake. Ni matarajio yetu kwamba Itatusaidia kushinda changamoto za biashara kama zile zilizoletwa milipuko wa Covid 19 ikiwemob machafuko yanayoendelea katika sehemu mbali mbali ulimwenguni.”
Kwa upande wa wafanya biashara walioambatana na Rais Samia, walieleza matunda ya ziara hiyo kwamba inakwenda kutatua changamoto nyingi zilizopo na kuimarisha ushirikiano wa mataifa haya mawili, huku matarajio yao makubwa yakiwa ni kuona changamoto zinazojitokeza katika mipaka zikipatiwa ufumbuzi kutokana na kwamba Zambia ni mdau mkubwa wa bandari ya Dar ea Salaam.
Eliasi Lukumai ni Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TATOA) alieleza kuwa licha ya kuwepo vituo vya ukaguzi mipakani, bado kuna changamoto kubwa ya kiusalama na kuomba miundombinu iongezwe kutokana na wingi wa mizigo pamoja na magari yanayopita katika barabara hizo.
“Kumekuwa na matatizo ya kiusalama kwamba magari yanaibiwa madini ya copper na na ile copper inapotea lakini pia kumekuwa na changamoto pale boarder jinsi ya kupitisha magari yet, yaani kuvusha magari yanayovuka boarder kwani kwa siku kuna tajribani gari 900 mpaka 1200 zinazovuka boarder hii kwendaZambia, Congo na nchi zingine ambazo zinapitia boarder hii ya Tunduma” amesema Lukumai.
Mbali na hayo yote Rais Samia aliongoza ujumbe wake katika mazungumzo na Rais wa Zambia ambapo wawili hao walishudia utiwaji saini wa mikataba za makubaliano na ushirikiano katika Ikulu ya Zambia..
Hati nne za makubaliano ya ushirikiano zilizosainiwa ni pamoja na Mradi wa usafirishaji wa Gesi Asilia kutoka Tanzania kwenda Zambia, na Makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia katika Sayansi na teknolojia.
Vilevile kwa upande wa mikataba jumla ya mikaba mnne ilisainiwa kati ya Tanzania na Zambia; Mkataba wa Utekelezaji kati ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jeshi la Ulinzi la Zambia kuhusu programu ya kubadilishana Wanafunzi wa Kozi ya Ukamanda na Unadhimu.
Mkataba wa Utekelezaji kati ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jeshi la Ulinzi la Zambia kuhusu programu ya kubadilishana Wakufunzi wa Kozi ya Ukamanda na Unadhimu.
Mkataba wa Utekelezaji kati ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jeshi la Ulinzi la Zambia kuhusu programu ya kubadilishana Wanafunzi wa Kozi ya Afisa-Cadet.
Pia,Mkataba wa Utekelezaji kati ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jeshi la Ulinzi la Zambia kuhusu ushirikiano katika Huduma za Tiba.
Rais Samia alitamatisha ziara yake Oktoba 25, 2023 kwa kulihutubia bunge la Jamhuri ya Zambia na kuandika historia ambayo haitafutika mioyoni mwa Wazambia pamoja na Watanzania kwa kuwa Rais wa Kwanza Mwanamke kuhutubia bunge hilo pia miongoni mwa marais wanne kuwahi kufanya hivyo ambapo kitendo hicho kilitafsriwa na wanadiplomasia kuwa ni heshima kubwa sana.
Siku tatu za Rais Samia ziarani Zambia zitakaa katika kumbukumbu ya maelfu ya miaka kuanzia sasa na hata vizazi vijavyo pia zenye maana kubwa katika ushirikiano wa mataifa haya mawili .
Uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Zambia ni wa mda mrefu ulioasisiwa na Mwalimu Nyerere pamoja na Kenneth Kaunda wa Zambia na kuyafanya mataifa haya kuwa washirika wa wakongwe zaidi ambao kwa pamoja walisimama mstari wa mbele katika kuyasaidia mataifa ya jirani kama vile Afrika Kusini kupata uhuru wao.
mwenendo wa ukuaji wa Biashara kati ya Tanzania na Zambia umeendelea kuongezeka kwa miaka ya hivi karibuni ambapo mwaka 2016 Tanzania iliuza nchini Zambia bidhaa zenye thamani ya sh.bilioni 70,815.40 na kiasi hicho kimeongezeka hadi kufikia sh. bilioni 183,648.5 kwa mwaka 2022.
Zambia ni muagizaji wa bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania, hususani mashine, vifaa vya ujenzi na vyakula vilivyosindikwa pamoja na nishati.
Ikiwa ni nchi isiyo na bandari bidhaa zake nyingi husafirishwa na kuingizwa nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam. Bidhaa hizo ni pamoja na magari ambayo husafirishwa kutoka Dar es Salaam hadi Zambia pia madini ya Shaba husafirishwa kutoka Zambia hadi bandarini.
Bomba la mafuta la TAZAMA lililojegwa miongo mitano iliyopita mwaka 1968 lenye urefu wa kilomita 1,710 na uwezo wa kubeba lita tani Milion 1.1kwa mwaka ambalo linatarajia kupanuliwa ifikapo 2024 ili kusafirisha mafuta yaliyochakatwa na siyo ghafi tena litaongeza kasi ya usafirishaji wa nishati hiyo.
Bomba hilo linamilikwa na serikali zote mbili kwa upande wa Zambia asilimia 76.7 na Tanzania ni asilimia 33.3.Pia mataifa haya yako mbioni kujenga bomba la gesi asilia kutoka Tanzania hadi Zambia.
Vilevile Tanzania na Zambia zinashirikiana katika usafiri wa reli yaTAZARA ya njia moja yenye urefu wa kilomita 1,860 iliyojengwa kati ya 1970 na 1975 ikiwa ni ufadhili wa Serikali ya watu wa China.
Reli hiyo ilijengwa ili kusafirisha shaba ya Zambia na bidhaa nyingine hadi Bandari ya Dar es salaam, pia malengo mengine ilikuwa ni kupunguza utegemezi wa kiuchumi wa Zambia kwa Rhodesia na Afrika Kusini, ambayo ilitawaliwa na serikali ya wazungu
Licha ya changamoto mbalimbali za uendeshaji tangu kuanzishwa kwake na siku zote kumekuwa jitahida katika kupata faida, hata hivyo, kupitia ziara ya Rais Samia juhudi za wazi kuhakikisha kuendelezwa kwa TAZARA zimeonekana.
Ziara ya Rais Samia Zambia ni ya kwanza kikazi kwa Rais wa awamu ya sita tangu alipoalikwa kuhudhuria sherehe za upisho wa Rais Hichilema,
Februari 24, 2015 Rais wa awamu ya tano Jakaya Kikwete naye aliafanya ziara ya kiserikali ya siku mbili mjini Lusaka, ambako alifanya mazungumzo ya faragha na aliyekuwa Rais wa taifa hilo Edgar Lungu.
Novemba 27, 2016 Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Zambia Edgar Lungu alifanya ziara ya kiserikali ya siku mbili jijini Dar-es-salaam, ambapo alifanya mazungumzo baina ya nchi mbili na John Magufuli.
Agosti 03, 2022 Rais wa Sasa wa Zambia Hakainde Hichilema alifanya ziara ya kiserikali ya siku moja jijini Dar es Salaam, ambapo alifanya mazungumzo baina ya nchi mbili na Rais Samia Suluhu Hassan
Oktoba 23, 2023 Rais Samia amefanya ziara ya kiserikali ya siku mbili mjini Lusaka, ambako alifanya mazungumzo na Rais Hakainde Hichilema.