Rais Dk. John Magufuli, ameanza kutoa mwelekeo wa Tanzania mpya aliyokusudia kuijenga.
Uamuzi wake wa kufanya ziara ya kushitukiza katika Wizara ya Fedha, umewafanya watumishi wengi wa Serikali waanze kuhaha.
Pamoja na mafanikio hayo aliyoyapata saa chache tangu aapishwe mwelekeo kamili wa aina ya Serikali atakayoiongoza atautoa atakapokuwa akizindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kulihutubia Taifa, wiki ijayo.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI katika ofisi kadhaa za umma umebaini kuwa maofisa utawala/utumishi katika wizara, idara na taasisi mbalimbali za umma wameanza kubadilika kwa kuwapo maeneo ya kazi, tofauti na mazoea yaliyokuwapo.
Katika baadhi ya ofisi ambako mahudhurio si jambo lililopewa umuhimu, kumekuwapo mwamko wa ghafla wa watumishi kuanza kusaini vitabu vya mahudhurio.
Miongoni mwa sehemu zinazotajwa kuyapokea mabadiliko hayo kwa kasi ni ofisi ya Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katika mabadiliko hayo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, ametajwa kuondolewa.
Rweyemamu amezungumza na JAMHURI na kuthibitisha kuwa ni kweli ameondoka Ikulu, lakini si kwa kufukuzwa au kuachishwa, isipokuwa ni kutokana na mkataba na umri wake kutomruhusu kuendelea na kazi.
“Mkataba wangu hausitishwa, umeisha bwana. Umeisha, umeisha, umeisha. Ninachojua mimi mkataba niliosaini unaisha Jumanne tarehe 10 (Novemba 10, 2015),” amesema.
Alipoulizwa kuwekwa kwake kando kwenye masuala ya Ikulu siku Rais Magufuli, alipoapishwa, alisema: “Uwanja wa Taifa nilikuwepo, mimi ndiyo nili-conduct ile lunch ya mchana…,” alisema Rweyemamu ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari.
Ameshika wadhifa huo Ikulu kwa miaka minane.
Katika hatua nyingine inayoonyesha mabadiliko ya kasi ya utendaji kazi, magari matano mapya aina ya Toyota Land Cruiser, mali ya Wizara ya Maliasili na Utalii, yaliyokwama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa zaidi ya mwaka mmoja, hatimaye leo yanatarajiwa kuondolewa uwanjani hapo.
Magari hayo yalitolewa msaada na mmoja wa wafadhili kwa ajili ya kuisaidia Wizara ya Maliasili na Utalii katika shughuli mbalimbali hasa kwenye mapambano dhidi ya ujangili nchini.
Kulikuwapo madai ya kwamba mmoja wa viongozi wa Wizara hiyo aliyemaliza muda wake, alikuwa na mpango wa kuyahodhi ili yatumike katika shughuli zake za utalii.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Adelhelm Meru, ameulizwa na JAMHURI na kujibu kwa maandishi kuwa: “Tatizo lilikuwa kodi, tayari tumeshailipa; yatatoka Jumanne (leo).”
Katika hatua nyingine, uamuzi wa Rais wa kuzuia safari za viongozi na watumishi wa umma nje ya nchi umepokewa kwa shangwe kubwa na wananchi wengi.
Chumba cha Habari cha Gazeti la JAMHURI kimepokea simu na ujumbe wa maandishi mwingi kutoka kwa wasomaji ambao wote wamepongeza hatua hiyo ya Rais.
Duru za uchunguzi zinaonyesha kuwa wakati wa kulihutubia Bunge, Rais Magufuli, atatumia fursa hiyo kueleza mambo mengi yanayolenga kuongeza kasi kwenye utendaji kazi kwa watumishi wa umma, lengo kuu likiwa kujenga Tanzania mpya.
Miongoni mwa mambo ambayo atayazungumza ni uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma na wananchi wenyewe, msisitizo mkubwa ukiwa kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa.
Rais Magufuli, ataeleza mikakati aliyokusudia kuisimamia ili kuongeza mapato ya Taifa na yatakayoiwezesha Serikali ya Awamu ya Tano kutekeleza ahadi zilizotolewa kwa wananchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Ahadi hizo ni zile zilizoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 na nyingine alizotoa kwenye mikutano kulingana na mahitaji mbalimbali ya jamii.
Kwa upande wa utendaji kazi serikalini na kwenye idara na taasisi zake, Rais Magufuli anatarajiwa kuwahimiza wakuu wa idara na taasisi kusimamia mahudhurio ya watumishi katika maeneo yao ya kazi; na wakati huo huo kutumia muda mrefu kuwahudumia wananchi badala ya kukaa ofisini.
Msingi mkuu wa hoja hiyo ni kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu”.
Atazungumzia mpango wa Serikali wa kubana matumizi; akilenga kubainisha azma ya Serikali yake ya kupunguza safari za viongozi na watumishi wa umma nje ya nchi, kupunguza matumizi ya magari ya kifahari, matumizi ya fedha zinazotumika kwenye malipo yanayotokana na semina, warsha, makongamano na mikutano isiyokuwa na tija kwa nchi na wananchi.
Kwenye magari, atasisitiza matumizi sahihi ya magari ya Serikali, na kukomesha wizi wa mafuta, vipuri na fedha nyingi zinazopotea kwenye matengenezo ya magari ya Serikali kwa kutumia karakana binafsi, badala ya TAMESA.
Ataagiza kuwapo kwa mpango wa wazi wa aina na idadi ya semina, makongamano, warsha na mikutano; huku msisitizo mkubwa ukiwa kuwataka viongozi na watumishi kutumia kumbi za ofisi badala ya hoteli za kifahari ambako malipo huwa makubwa mno.
Mtoa taarifa anasema Rais Magufuli alichokusudia kukifanya ni mkusanyiko wa mazuri ya watangulizi wake wa awamu zote nne waliyoyatumia kuhakikisha Serikali inabana matumizi.
Kwa miaka ya karibuni, mawaziri kadhaa wamekuwa wakikodi kumbi za hoteli za kifahari kwa ajili ya mikutano, ikiwamo ya waandishi wa habari. Malipo kwa shughuli kama hizo yamekuwa yakigharimu hadi Sh milioni 8 kwa saa tatu hadi nne.
Pia wizara, idara na taasisi mbalimbali zimekuwa zikitoka mji mmoja na kwenda mji mwingine kwa ajili ya kufanya mikutano, semina, warsha na makongamano. Kwenye safari hizo kumekuwapo malipo makubwa kwa washiriki.
Kwenye upunguzaji matumizi ya Serikali, anakusudia kulezea muundo wa Baraza la Mawaziri atakalounda. Amenuia kuunda Baraza dogo lenye mawaziri mahiri wanaoendana na kasi yake ya uchapaji kazi.
Rais Magufuli, anatarajiwa kuzungumzia suala la usalama wa nchi, akiwahakikishia Watanzania kuwa wataendelea kuwa salama kama ilivyokuwa kwa awamu zilizotangulia. Lakini pia mtoa taarifa wetu anasema Rais atagusia suala la ufungaji vituo vya polisi saa 12 jioni; na kuwataka wachape kazi kwa saa 24 ili wananchi wasiwe na hofu ya usalama wao na kwa hiyo washiriki shughuli za uzalishaji bila wasiwasi.
Kwenye suala hilo la usalama, Rais Magufuli, atawataka wahamiaji haramu na watu wengine wanaoishi nchini kinyume cha sheria kujisalimisha kwa kukamilisha taratibu za uhamiaji, au kurejea walikotoka.
Hapo anakusudiwa kuzungumzia suala la uvamizi wa wafugaji kutoka nchi jirani wanaoingiza mifugo yao kwenye maeneo ya mapori na hifadhi. Maeneo yaliyolengwa ni yale ya mipakani.
Kuhusu miundombinu, Rais Magufuli, anatarajiwa kuzungumzia mikakati ya usafirishaji shehena ndani na nje ya nchi, lengo kubwa likiwa kujenga reli ya kisasa.
“Kusudio lake ni kutaka kuona mizigo mingi inasafirishwa kwa reli na meli ili kutoa nafuu kwa barabara zinazoendelea kuharibika kwa kasi na pia kupunguza bei za bidhaa. Kwa sasa asilimia 98.5 ya mizigo yote nchini inasafirishwa kwa njia ya barabara.
“Amekusudia kuhakikisha reli mpya zinajengwa na kufufua zile ambazo zimekufa kutokana na kutelekezwa au kutokana na uchakavu.
“Kwa kufanya hivyo anaamini barabara zitadumu miaka mingi na hivyo kuokoa fedha za nchi,” amesema mtoa taarifa wetu.
Kuhusu viwanda, Rais Magufuli, anatarajiwa kutangaza mikakati ya kuhakikisha viwanda vipya vinajengwa na kufufua vile vilivyokufa.
“Hapo kazi kubwa ya kwanza anayoifanya ni kupata taarifa ya wataalamu ya kujua kwanini viwanda vimekufa na kwanini vingine vinasuasua kwenye uzalishaji,” kimesema chanzo chetu.
Wakati wa kampeni, Dk. Magufuli alisisitiza kuwa atahakikisha Tanzania inakuwa ya viwanda ili kuongeza mapato ya nchi, lakini wakati huo huo ni kuhakikisha vijana wengi wanapata ajira.
Suala la viwanda ataliweka sambamba na suala la kilimo ambako anatarajiwa kutangaza mipango mipya ya kuinua kilimo kwa kuhakikisha wakulima wanapata tija kwa mazao yao; hasa kwa kufuta kabisa utaratibu wa Serikali na wa wafanyabiashara kuwakopa wakulima.
Suala la elimu-kwa maana ya utoaji elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, na mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu; ni miongoni mwa mambo atakayoyatolea mwongozo. Kwenye mikopo, anatarajiwa kutangaza uamuzi wa kuongeza fedha ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi zaidi ya 50,000 wa mwaka wa kwanza walioomba mikopo kwa mwaka wa masomo wa 2015/2016.
Malipo bora kwa walimu na watumishi wengine wa umma, ni baadhi tu ya vionjo vichache kati ya vingi ambayo Rais atavizungumzia, lakini msisitizo wake mkubwa ukiwa kwa kila mmoja kujituma kweli kweli kufanya kazi bila kuchoka.
Wavamizi wa hifadhi za barabara atawagusa kwa kuwataka waliovamia waondoke wenyewe ili kupisha upanuzi wa barabara, na wale wanaostahili fidia, Serikali itawalipa kadri sheria inavyoagiza.
Msongamano wa magari katika miji na majiji nchini ni miongoni mwa mambo atakayoyazungumza; na atabainisha mipango na muda utakaotumiwa na Serikali yake katika kukabiliana na adha hiyo. Kwenye mkakati huo, atagusia pia uwezekano wa baadhi ya majiji kama Dar es Salaam kuwa na mfumo wake wa uongozi unaojitegemea ili kuondoa mgongano au mwingiliano wa majukumu ambao mara kadhaa umesababisha kazi nyingi zikwame kutokana na wahusika kurushiana mpira.
Vita dhidi ya rushwa ni eneo jingine ambalo Rais Magufuli, amenuia kulitangaza rasmi kwa Watanzania na atawataka wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja.
Atarejea ahadi yake ya uundwaji wa Mahakama maalumu kwa ajili ya kuwashughulikia mafisadi na wahujumu uchumi ambao anaamini wamesababisha kukwama kwa mambo mengi ya kimaendeleo hapa nchini.
Mtoa taarifa wetu amesema Rais pia atafananua mikakati ya Serikali yake katika matumizi ya mapato yatakayotokana na madini na gesi, na pia atatangaza mikakati ya utunzaji mazingira ambayo kwa sasa yameathiriwa mno kwa shughuli za kibinadamu.
“Itakuwa hotuba ya karne yenye kutoa mwelekeo wa Tanzania mpya, si hotuba ya kukosa kuisikiliza,” kimesema chanzo chetu.