Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kisarawe
Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani inatarajia kufanya tamasha kubwa la Utalii liitwalo BATA MSITUNI INTERNATIONAL FESTIVAL, litakalofanyika katika hifadhi ya msitu ya Pugu -Kazimzumbwi septemba 3-8 mwaka huu.
Tamasha hilo litahusisha nchi tatu ikiwemo Tanzania, Kenya na Afrika ya Kusini ambapo watu 3,000 wanalengwa kuhudhuria.
Mkuu wa wilaya ya Kisarawe,Petro Magoti akizungumza na waandishi wa habari katika kikao na waandishi kilichofanyika Pugu -Kazimzumbwi alieleza, lengo la Tamasha hilo ni kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambae amefungua milango ya utalii kwa kuweka mazingira bora ya kuvutia watalii.
Alieleza, eneo hilo la utalii wa ndani Pugu -Kazimzumbwi lina ukubwa wa hekta zaidi ya 8,000 ,eneo ambalo ni kubwa na sasa wanatarajia kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii watakaohitaji kuingia mkataba wa kuwekeza Zoo, kujenga hotel na kuweka miundombinu mizuri.
Magoti alifafanua, watapata fursa ya kutangaza vivutio na tamaduni za Kisarawe.
“Kuanzia sasa watu wa mikoa jirani watafute pesa waje wajionee Utalii wa ndani uliopo Kisarawe, kujifunza na kujionea tamaduni za wazaramo,ngoma zao ikiwemo Msewe,Vanga na mdundiko ngoma zote hizo zitakuwepo”
Vilevile alieleza, festival hiyo itaambatana na mihogo festival, samaki
Festival,uvuvi, mashindano ya makasia, riadha msituni, mashindano ya baiskeli na pikipiki.
Nae Meneja wa TFS Kisarawe,Mhifadhi Baraka Mtewa alieleza, Pugu -Kazimzumbwi ni sehemu ya kusogea kujionea mandhuri nzuri, vivutio ikiwemo uoto wa asili, miti mbalimbali ikiwemo mpugupugu na historia zake, boti katika bwawa kubwa la Utalii lenye square meter 21,000.
Alieleza watu watafanya uvuvi na kupiga makasia,kupanda mlima msituni,vyakula,vinywaji, mahema ya kulala na usalama umezingatiwa.
Hata hivyo Mtewa aliwataka wananchi watunze na kulinda hifadhi za misitu kwa manufaa ya Taifa na kulinda uoto wa asili.
Mratibu wa tamasha Innocent Kabaitilaki alieleza, kwasasa taratibu za maandalizi zinaendelea na kufikia Agost mwishoni mengi yatakuwa yamekamilika
Alieleza kutakuwa na ngoma za asili, wasanii wakubwa kutoka Afrika Kusini na Tanzania na amewaomba wananchi wasikose tamasha hilo.
Innocent alitaja, viingilio katika tamasha la Bata Msituni festival ni kuanzia 50,000 kwa watu wa kila siku,150,000 na wageni kutoka nje ya nchi ni 250,000-300,000.